
Kaulimbiu ya mwaka huu, ya Siku ya Kimataifa ya Ndege Wahamao imekuwa “Kila Ndege Ni Muhimu, Uangalizi Wako kwao Una Umuhimu ,” ikiaangazia hitaji la haraka la kulinda ndege wahamaji pamoja na mifumo ya ikolojia wanayoitegemea.
UN News imezungumza na Catherine Quayle, Mkurugenzi wa Mawasiliano katika shirika la Wild Bird Fund mjini New York.
Kwa watu wanaoishi mijini, mara nyingi huonekana kana kwamba wanyamapori wako mbali je ndege wahamaji wanakuwaje bado sehemu ya maisha yetu ya kila siku?
Catherine Quayle: Ikiwa unaishi mahali penye miti na kijani kidogo, hata katikati ya Manhattan, unaweza kusikia ndege wanapoimba unapoamka. Nyimbo zao hubadilika kulingana na misimu ya mwaka. Huhitaji hata kutoka nyumbani ili kushuhudia utofauti wa viumbe hai nje ya dirisha lako. Ndege pia huhama mara nyingi usiku. Jioni unaweza kuona shakwe au korongo wakihama kwenda kupumzika. Ukiangalia juu mapema asubuhi au jioni, utaona ndege bila hata kutoka nyumbani.
Mji wa New York upo kwenye njia ya Alantiki ya ndege wahamao au kwa lugha ya Kiingereza Atlantic Flyway.
Ni ndege wangapi hupita juu yetu wakati wa kilele cha uhamaji?
Catherine Quayle: Kituo cha taarifa za ndege BirdCast, chombo kutoka maabara ya Cornell ya elimu ya ndege (Lab of Ornithology), hutumia rada za hali ya hewa kufuatilia uhamaji wa ndege, ikionesha ni wangapi wanaruka na lini.
Katika usiku wa kilele cha uhamaji, ndege bilioni kadhaa wanaweza kuwa angani kote Marekani kwa wakati mmoja. Juu ya mji wa New York pekee, hadi ndege milioni moja wanaweza kupita katika usiku mmoja, lakini watu wengi hawafahamu kwa sababu hutokea usiku.
Ni changamoto zipi ambazo ndege hukumbana nazo wanapohama?
Catherine Quayle:Moja ya changamoto kubwa ni kupotea kwa makazi yao. Ndege huhama ili kupata chakula maalumu kinachopatikana katika nyakati tofauti za mwaka. Kwa vizazi vingi wamejifunza sehemu za kwenda, kwa mfano Amerika ya Kati wakati wa majira ya baridi. Lakini ikiwa maeneo hayo yamekatwa miti, kujengwa majengo, kufunikwa kwa lami au kuharibiwa, ndege wengi hawataweza kuishi wanapofika maeneo hayo ya majira ya baridi au ya kuzaliana.
Tishio jingine kubwa mjini New York ni kugongana na madirisha ya majengo. Hali hii inaaminika kuwa mbaya zaidi kuliko miaka 50 iliyopita kwa sababu usanifu wa kisasa unatumia vioo vingi sana. Nyuso kubwa za vioo na madirisha ya kioo tupu ni maarufu sana, lakini ni hatari kubwa kwa ndege.
Je, kuna aina fulani za majengo au maeneo yaliyo hatari zaidi kwa ndege?
Catherine Quayle:Majengo marefu ni hatari kwa sababu mwanga mkali huvutia ndege, na kuwavuta katika maeneo kama katikati ya Manhattan wakati wa uhamaji, ambapo vioo huakisi miti ya karibu. Mchanganyiko wa mwanga na vioo ni hatari sana.
Lakini hata nyumba za kawaida zinaweza kuwa hatari. Mwangaza unaoakisiwa, hasa karibu na vyakula vya ndege au miti, mara nyingi husababisha migongano. Kwa kweli, nyumba husababisha migongano mingi zaidi, isipokuwa huwa haionekani sana kwa sababu ni ndege mmoja au wawili kwa wakati mmoja, tofauti na katikati ya Manhattan ambapo unaweza kuona ndege mia moja.
Ndege wahamiaji wako katika hatari zaidi kwa sababu huwasili usiku wakiwa wamechoka, wamechanganyikiwa, na katika maeneo wasiyoyafahamu.
Ni mambo gani tunaweza kufanya kila siku kusaidia uhifadhi wa ndege?
Catherine Quayle:Unaweza kuzima taa za nje usiku ili anga liwe giza zaidi na ndege wasivutiwe na mwanga. Katika jamii ndogo, watu wakizima taa zao hufanya tofauti kubwa. Moja ya mambo bora zaidi unaweza kufanya ni kupanda mimea ya asili katika bustani yako. Fanya utafiti mdogo kuhusu mimea ya asili katika eneo lako, na tumia sehemu ya eneo lako la nje kupanda mimea hiyo ili kuvutia wadudu na ndege.
Je, una simulizi ya uokoaji ambayo huiwazia?
Catherine Quayle:Ninapotembelea bustani ya karibu kutazama ndege, hupita karibu na majengo kadhaa ambapo migongano ya ndege na vioo hutokea mara nyingi. Wakati wa msimu wa uhamaji, mimi huangalia kama kuna ndege waliojeruhiwa.
Katika safari moja, niliona ndege barabarani chini ya daraja la vioo kati ya majengo miundo kama hiyo ni hatari sana kwa sababu ndege hawatarajii na mara nyingi hugonga vioo.Nilikimbia chini ya kilima na kumbeba ndege huyo, sekunde chache baadaye gari lilipita juu ya sehemu aliyokuwa amelala. Ndege huyo alikuwa Scarlet Tanager mwenye manyoya mazuri ya manjano. Baadaye alitibiwa na kuachiliwa, na bila shaka angegongwa kama nisingemchukua.
Kwa watu ambao hawajioni kama wapenda ndege, ni jambo gani dogo wanaweza kuanza kufanya?
Catherine Quayle:Anza kwa kutambua ndege waliopo karibu yako kile unachoona na kusikia unapokuwa nje. Kadri utakavyowazingatia, ndivyo hamu yako itakavyoongezeka. Unaweza hata kuanza kutumia darubini au kujiunga na matembezi ya kutazama ndege.
Wakati wa msimu wa uhamaji, matembezi mengi ya bure ya kutazama ndege huandaliwa katika bustani za maeneo mbalimbali, mara nyingi yakiongozwa na wataalamu, na huwa ya kufurahisha sana.
Mara ya kwanza nilipoingia bustani ya Central Park miaka mingi iliyopita nikiwa na darubini na kuanza kuona ndege wengi ambao sikuwa nimewahi kugundua kabla, nilishangazwa sana. Nilifurahi mno na sikuweza kuacha kufanya hivyo. Nimeendelea hadi leo na hiyo ilikuwa miaka 25 iliyopita.