
Dar es Salaam. Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imezindua rasmi Mkakati wa Ufadhili wa Kilimo Himilivu dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi na Uhifadhi wa Mazingira wa mwaka 2025–2027, hatua inayolenga kusaidia wakulima na wafanyabiashara wa sekta ya kilimo kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mkakati huo wa TADB Green Agri-Finance Strategy 2025–2027 unalenga kuimarisha kilimo endelevu, kuongeza uzalishaji na kusaidia juhudi za taifa katika kukabiliana na athari za tabianchi sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Hamad f Masauni amesema mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuathiri uzalishaji wa chakula, usalama wa maji na maisha ya wananchi wengi, hali inayohitaji uwekezaji mkubwa katika kilimo himilivu na endelevu.
“Sera ya kilimo endelevu na uhifadhi wa mazingira lazima ziende sambamba. Taasisi za kifedha zina jukumu kubwa katika kusaidia uwekezaji wa kijani na kuwawezesha wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Masauni.
Amesema mkakati huo unaunga mkono juhudi za Serikali katika kujenga uchumi endelevu, kuimarisha usalama wa chakula na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Aidha, amesema kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za kifedha, washirika wa maendeleo pamoja na taasisi za utafiti ili kusaidia upatikanaji wa fedha za miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Agricultural Development Bank, Frank Nyabundege amesema mkakati huo ni sehemu ya dhamira ya benki hiyo kusaidia mageuzi ya sekta ya kilimo nchini.
Amesema kupitia mkakati huo, TADB itaongeza uwekezaji katika miradi ya umwagiliaji, matumizi ya nishati mbadala, teknolojia za kilimo himilivu, uhifadhi wa maji pamoja na uwekezaji endelevu katika sekta za mifugo, uvuvi na mazao.
“Kama benki ya maendeleo ya kilimo nchini, tuna wajibu wa kuendelea kusaidia wakulima na wafanyabiashara wa sekta ya kilimo. Kupitia mkakati huu, tunataka kuongeza uzalishaji, kulinda mazingira na kuboresha maisha ya wananchi wanaotegemea kilimo,” amesema Nyabundege.
Amesema sekta ya kilimo bado ndiyo mhimili mkuu wa uchumi wa Tanzania na chanzo kikubwa cha ajira kwa wananchi wengi, lakini imeendelea kuathiriwa na changamoto za ukame, mafuriko na mabadiliko yasiyotabirika ya hali ya hewa.
Nyabundege amesema katika kipindi cha zaidi ya miaka 10, TADB imetoa zaidi ya Sh1.42 trilioni kwa ajili ya uwezeshaji wa sekta ya kilimo, huku zaidi ya Sh67 bilioni zikielekezwa katika miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa benki hiyo, zaidi ya wakulima wadogo milioni 2.6 wamenufaika na mikopo pamoja na huduma mbalimbali za kifedha, huku zaidi ya miradi 812 ya kilimo ikiwezeshwa nchini kote.
Pia ameishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri yanayoiwezesha benki kutekeleza majukumu yake ya maendeleo.
Uzinduzi huo uliwakutanisha viongozi wa Serikali, taasisi za kifedha, washirika wa maendeleo, watafiti, sekta binafsi, wakulima pamoja na mashirika ya kiraia kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha sekta ya kilimo na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.