
Mtoto mjinga hachekwi, bali hufundishwa.
Ujinga si kosa la mtu kuzaliwa nalo, bali ni hali inayotokana na kukosa nafasi ya kupata elimu na malezi sahihi. Watanzania wengi hasa wenye umri wa kati na wazee kwa sasa, walikosa elimu ya awali kutokana na sababu mbalimbali.
Wengine walibaguliwa na wakoloni, wengine walikumbwa na umasikini uliowafanya wazazi washindwe kuwapeleka shule na wengine walizuiwa na mila potofu pamoja na mifumo ya kitamaduni iliyokuwa ikipinga elimu kwa baadhi ya wanajamii.
Kutokana na hali hiyo, maisha yao yalikuwa magumu sana. Wengi wao walikulia kwenye mazingira ya kufanya kazi ngumu bila maarifa ya kutosha ya kuboresha maisha yao.
Walikosa uwezo wa kusoma, kuandika na hata kuelewa haki zao za msingi. Hata hivyo, walipopevuka na kuanzisha familia zao, waliweka azimio la kuhakikisha watoto wao hawapiti kwenye mateso waliyoyapitia wao.
Walitambua kuwa elimu ndiyo ufunguo wa maisha bora na maendeleo ya kweli.
Baada ya Tanzania kupata uhuru, Serikali ilifanya jitihada kubwa kupambana na adui ujinga. Kulikuwa na kampeni mbalimbali za kuhamasisha elimu kwa wote, ujenzi wa shule za msingi na utoaji wa elimu ya watu wazima maarufu kama elimu ya ngumbaru. Jitihada hizi zilisaidia kuongeza kiwango cha elimu nchini na kuwafanya wananchi wengi kupata uwezo wa kusoma na kuandika, na kuweza kujitambua. Kwa kiwango fulani, taifa lilianza kupata ahueni dhidi ya ujinga.
Hata hivyo, bado kuna changamoto kubwa kuhusu aina ya elimu tunayohitaji katika dunia ya sasa. Kupata elimu ya darasani pekee haitoshi kama wananchi hawapati maarifa ya namna ya kutumia elimu hiyo katika maisha yao ya kila siku.
Tunaweza kujilinganisha na mtu aliyekuwa na njaa kwa siku kadhaa halafu akaletewa chakula kingi kwa wakati mmoja.
Badala ya kula kwa utaratibu, anakula kwa pupa na kuishia kuvimbiwa kabla hata hajashiba. Vivyo hivyo, Watanzania wengi wamekutana ghafla na mabadiliko makubwa ya kiteknolojia bila maandalizi ya kutosha. Leo hii teknolojia imeufanya ulimwengu kuwa kama kijiji. Mtu akiwa nyumbani kwake anaweza kufanya biashara na watu wa Dubai, China au Ulaya kupitia simu ya mkononi.
Tunaweza kutumia mitandao ya kijamii, kufanya manunuzi mtandaoni na hata kutuma fedha kwa sekunde chache.
Haya ni maendeleo makubwa sana ambayo yanapaswa kutumika kuinua maisha ya wananchi. Lakini swali la msingi ni je, wananchi wana elimu ya kutosha kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia na fedha?
Watu wengi wanaweza kupata fedha lakini wakashindwa kuzitumia kwa busara kutokana na ukosefu wa elimu ya kifedha.
Mfano, mtu anaweza kununua gari la kifahari kwa lengo la kuonekana ana maisha mazuri, wakati ukweli ni kwamba hana uwezo wa kulihudumia wala si hitaji muhimu kwake. Matokeo yake anaingia kwenye madeni na kuharibu mzunguko wake wa fedha.
Hii inaonesha kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana kwa kuwa na fedha pekee, bali kwa kuwa na maarifa ya namna ya kuzitumia fedha hizo kwa tija.
Kutokana na maendeleo ya teknolojia, pia kumekuwa na ongezeko kubwa la matapeli wa kimtandao na wa kianalojia.
Kila siku watu wanakutana na ujumbe wa kitapeli unaowataka kutuma fedha kwenye namba fulani kwa ahadi za kupata utajiri wa haraka.
Wengine wanajifanya waganga wa fedha za majini, na wapo wanaokumbana na manabii wanaodai kufufua wafu, kufuta madeni na kesi zao kwa njia za miujiza. Huko kote mwananchi anatakiwa atangulize fedha kupata huduma hizo.
Mara nyingi habari zinazoonekana kwenye vyombo vya habari ni sehemu ndogo tu ya matatizo yaliyopo kwenye jamii.
Kumekuwa na matukio ya watu kujifanya wasaidizi wa viongozi wakubwa wa Serikali, wengine wakijifanya watendaji wanaotoa zabuni au ajira za uongo.
Wapo pia wanaowatapeli vijana kwa ahadi za kuwaingiza jeshini au kuwapatia kazi serikalini. Haya yote yanaonesha ni kwa kiasi gani elimu sahihi inahitajika.
Katika dunia ya sasa yenye ushindani mkubwa, elimu sahihi ni silaha muhimu ya kujilinda dhidi ya udanganyifu na pia ni msingi wa maendeleo ya taifa.
Watanzania wanapaswa kupewa elimu inayowajengea uwezo wa kufikiri kwa kina, kufanya maamuzi sahihi na kutumia teknolojia kwa manufaa yao.
Elimu hiyo isiishie darasani pekee, bali iwaandae wananchi kukabiliana na changamoto za maisha ya kisasa.
Aidha, ujio wa viongozi wa mataifa mbalimbali na wawekezaji nchini, itakuwa fursa kubwa kwa Watanzania ikiwa wananchi watakuwa na elimu ya ushindani.
Bila elimu hiyo, Watanzania wataendelea kuwa watazamaji wakati wageni wakitumia rasilimali zilizopo kujinufaisha.
Taifa linaweza kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili, lakini kama wananchi wake hawana maarifa ya kuzitumia ipasavyo, utajiri huo hautaleta maendeleo kwao.
Kwa hiyo, ni jukumu la Serikali, wazazi, walimu na jamii kwa ujumla kuhakikisha elimu bora na sahihi inawafikia wananchi wote.
Serikali ioneshe kwa vitendo kuwa udanganyifu wa aina yoyote ni uhalifu.