
Dar es Salaam. Kampuni ya utoaji wa bima ya afya kwa waajiri, Discovery Health – Global Health Solutions, imetangaza mikakati mipya ya kuboresha huduma za afya kwa wafanyakazi katika sekta mbalimbali nchini Tanzania, hatua inayolenga kuongeza ustawi wa wafanyakazi na kusaidia waajiri kudhibiti gharama za matibabu.
Kampuni hiyo, ambayo awali ilikuwa ikijulikana kwa jina la Vitality Health International (Africa), imebadilisha rasmi jina lake na sasa itafahamika kama Discovery Health – Global Health Solutions mwanzoni mwa mwaka huu.
Mabadiliko hayo yanaelezwa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha huduma za afya kwa waajiri na wafanyakazi katika bara la Afrika kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kidijitali, usimamizi wa afya na programu za ustawi wa wafanyakazi.
Mkurugenzi Mkuu wa Discovery Health – Global Health Solutions, Emma Knox, amesema licha ya mabadiliko ya jina, dhamira ya kampuni hiyo ya kuboresha afya za watu na kulinda maisha yao itaendelea kuwa msingi mkuu wa shughuli zake.
Amesema kampuni hiyo inalenga kwenda zaidi ya mfumo wa kawaida wa bima ya afya kwa kujenga mfumo jumuishi unaounganisha huduma za bima, ustawi wa wafanyakazi na teknolojia za kisasa za afya.
“Tunataka kwenda zaidi ya bima ya afya ya kawaida kwa kujenga mfumo jumuishi wa afya kwa waajiri kote Afrika.
Mfumo huu utaunganisha bima ya afya, programu ya ustawi ya Vitality pamoja na uwezo mkubwa wa kiutawala na kimatibabu,” alisema Knox.
Katika kuimarisha huduma zake nchini Tanzania, kampuni hiyo imetangaza mikakati mbalimbali ikiwemo kuendelea kushirikiana na kampuni za bima za ndani ili kutoa huduma bora zinazokidhi mahitaji ya waajiri na wafanyakazi.
Alisema kuwa itaongeza huduma za kinga na ustawi wa afya kupitia programu za mazoezi, lishe bora na uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kusaidia wafanyakazi kuwa na maisha yenye afya na kuongeza tija kazini.
“Discovery Health pia inapanga kutoa vifurushi vya bima vinavyomudu gharama kwa makundi tofauti ya wafanyakazi na kampuni, huku ikiongeza matumizi ya huduma za kidijitali na telemedicine ili kurahisisha upatikanaji wa matibabu nchini,” alisema.
Alifafanua kuwa kupitia matumizi ya teknolojia na uchambuzi wa taarifa za afya, kampuni hiyo inalenga kubaini mapema hatari za magonjwa na kusaidia kupunguza gharama za matibabu kwa waajiri na taasisi mbalimbali.
Mbali na hilo, kampuni hiyo itatoa motisha kwa wafanyakazi watakaoshiriki katika programu za afya na ustawi sehemu za kazi pamoja na kuendesha kampeni za elimu ya afya ili kuongeza uelewa kuhusu maisha bora na kinga dhidi ya magonjwa.
“Pia tutaweka mkazo katika kushughulikia changamoto za afya zinazoikabili Tanzania, ikiwemo malaria, magonjwa sugu pamoja na afya ya mama na motto,” alisema.
Alisema kuwa nchini Tanzania, Discovery Health – Global Health Solutions itaendelea kushirikiana na Strategis Insurance, kampuni ya bima ya ndani ambayo imekuwa mshirika wake tangu mwaka 2024.
Ushirikiano huo unatajwa kuwa muhimu katika kuhakikisha huduma zinazotolewa zinaendana na mazingira ya soko la Tanzania pamoja na mahitaji ya waajiri wa ndani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Strategis Insurance, Dk Malav Manek, amesema ushirikiano huo utaendelea kusaidia utoaji wa bidhaa bunifu za bima ya afya nchini.
“Tunaamini ushirikiano huu utaongeza ubora wa huduma kwa wateja wetu huku ukichangia maendeleo ya sekta ya afya na bima nchini Tanzania,” amesema Dk Manek.
Mbali na huduma za kawaida za bima ya afya, Discovery Health pia imeanzisha huduma ya Administration Services Only (ASO), mfumo wa usimamizi wa afya unaolenga kusaidia kampuni kubwa kusimamia huduma za afya kwa ufanisi zaidi.
Discovery Health ni moja ya kampuni kubwa za usimamizi wa mifuko ya matibabu na huduma za managed care nchini Afrika Kusini, ikiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 34 katika sekta hiyo.
Kwa sasa kampuni hiyo inatoa huduma za usimamizi wa afya kwa zaidi ya wanachama milioni 3.6 barani Afrika, huku ikitumia mifumo ya kisasa ya kidijitali, sayansi ya data na utaalamu wa kitabibu kuboresha huduma za afya na kudhibiti gharama za matibabu kwa waajiri na taasisi mbalimbali.