Unguja. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amesisitiza umoja ndani ya chama hicho na kuvunja makundi yaliyokuwepo kipindi cha uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, akisema yanapaswa kufutwa baada ya uchaguzi.
Ametoa kauli hiyo leo Mei 13, 2026 alipokuwa Mkoa wa Kusini Pemba katika muendelezo wa ziara yake yenye lengo la kutoa shukrani na kupongezana baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu mwaka jana.
Dk Mwinyi ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, amesema kipindi cha uchaguzi makundi lazima yawepo kwa sababu wagombea ni wengi na kila mtu ana wafuasi wake, ila baada ya uchaguzi kundi linatakiwa kuwa moja la Chama cha Mapinduzi.
“Makundi kipindi cha uchaguzi yanaruhusiwa kwa sababu tuna demokrasia ndani ya chama, watu watagombea wengi, kila mtu atakuwa na wafuasi wake, lakini baada ya uchaguzi tunawajibu wa kuondoa na kufuta makundi yote na kubaki kundi moja la Chama cha Mapinduzi,” amesema.
Amesema umoja na mshikamano ndiyo jambo linalotakiwa ndani ya chama hicho ili kiendelee kutekeleza ilani yake ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Hivyo, Rais Mwinyi amesisitiza kutoruhusu makundi ndani ya CCM na kuwataka viongozi wote wa chama hicho kwa ngazi zote kukemea wale wote wanaosababisha makundi hayo.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, akizungumza na viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kusini Pemba katika mkutano wa kutoa shukrani baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ulioambatana na ufunguzi wa Jengo la CCM Ng’ombeni pamoja na Ukumbi wa Mikutano wa Hijaz Complex, hafla iliyofanyika Ng’ombeni, Mkoa wa Kusini Pemba
“Wewe umeshashinda, umeshakuwa mwakilishi au mbunge au diwani, unataka kundi kuliendeleza la nini? Jambo hilo linakidhoofisha chama, lazima tuwe wamoja,” amesisitiza Dk Mwinyi.
Amesema kuna baadhi ya wabunge wanapokwenda katika majimbo yao wakitaka kutoa kitu, huwapa wale waliowaunga mkono na kuwaacha wale wengine ambao hawakuwa upande wake kipindi cha uchaguzi.
“Hii haina afya kabisa, kwa sababu haya ndiyo yanayoendeleza makundi. Ukishashinda basi watu wote wanatakiwa kuwa upande wako, msianze kubagua,” amesema Mwinyi.
Amesema mwaka 2027 kuna uchaguzi ndani ya chama na kusema kuwa makundi yatakuwepo kwa sababu wagombea ni wengi, lakini baada ya kumalizika uchaguzi makundi yote yaungane na liwe kundi moja la Chama cha Mapinduzi.
“Huku tunapokwenda kwenye uchaguzi wa chama, uchaguzi huu ni wa aina yake kwa sababu utapelekea mwaka 2030 kutakuwa na mabadiliko ya uongozi kwa Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano, maana yake watu wanajipanga kwa nafasi hizo,” amesema.
Amesema hakuna ubaya katika kujipanga, bali wanachama wanapaswa kutokuendeleza makundi ndani ya chama.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohammed Said Mohammed (Dimwa), amesema ushindi mkubwa alioupata Dk Mwinyi ni matokeo ya imani ya wananchi kutokana na ilani ya mwaka 2020/2025 ilivyotekelezwa kwa kishindo.
Kwa mujibu wake, Dk Mwinyi ni kiongozi anayeweka maslahi ya wananchi wake mbele na ustawi wa wananchi wa Zanzibar kupitia sera na maamuzi yenye kuleta matumaini mapya kwa wananchi wake.
Aidha amesema Mkoa wa Kusini Pemba ni wa mfano katika suala zima la mshikamano wa watu wake, na kuhakikisha kuwa wananchi wanashirikiana na chama chao na Serikali katika kuleta maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba, Yussu Ali Juma, amesema kuchaguliwa kwa Dk Mwinyi hakukuwa ndoto kwani ameshinda kwa kishindo kutokana na utekelezaji mkubwa wa Ilani alioufanya.
Amempongeza kwa maendeleo makubwa aliyoyafanya katika Mkoa wa Kusini Pemba ambapo mambo makubwa yamefanyika katika mkoa huo kwa kipindi kifupi cha uongozi wa Dk Mwinyi.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba, Kajoro Viororoka, amesema hali ya kisiasa ndani ya mkoa ni shwari na shughuli mbalimbali za chama zinaendelea na wana ushirikiano mzuri baina ya jumuiya za vyama.
Amesema hali ya kiuchumi katika CCM Mkoa wa Kusini Pemba kisiwani ni nzuri na wana vyanzo mbalimbali vya uchumi.
Aidha amesema wanajivunia maendeleo yaliyofanyika katika uongozi wa Dk Mwinyi kama vile ujenzi wa uwanja wa ndege unaoendelea, vituo vya afya, skuli, barabara za lami na maendeleo mengine mengi.