
Arusha. Hali ya sintofahamu imeigubika familia ya Scola Peter Chuwa (45), mkazi wa Mtaa wa Ndarivoi jijini Arusha, baada ya kutoweka kwa zaidi ya siku 90 sasa bila kufahamika alipo.
Scola anadaiwa kutoweka Februari 8, 2026 majira ya saa tisa alasiri baada ya kuaga nyumbani kuwa anakwenda kwenye msiba wa jirani.
Taarifa za kupotea kwake ziliripotiwa katika Kituo cha Polisi Unga Ltd na kufunguliwa jalada lenye namba UNG/RB/277/26 kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, mume wa mwanamke huyo, Solomon Kivuyo, amesema mke wake aliondoka nyumbani siku hiyo akieleza kuwa anakwenda kushiriki msiba wa jirani, lakini tangu wakati huo hajawahi kurejea nyumbani.
Amesema juhudi mbalimbali za kumtafuta kupitia ndugu, jamaa na marafiki zimekuwa hazijazaa matunda, huku akieleza kuwa mkewe aliacha hata simu yake ya mkononi nyumbani kabla ya kuondoka.
“Kwa sasa tunaishi kwa wasiwasi mkubwa kwa sababu hatujui kama ni mzima au amepatwa na jambo baya.
“Tumejaribu kuwasiliana na ndugu na marafiki zake mbalimbali lakini hakuna mwenye taarifa zozote kuhusu alipo,” amesema.
Kivuyo amesema tukio hilo limewaathiri kisaikolojia wanafamilia wote, hususan watoto wao wanne ambao wameendelea kumuulizia mama yao bila mafanikio.
“Hali hii imetupa mashaka makubwa sisi wanafamilia, hasa ndugu na watoto wetu. Tunaomba wananchi wenye taarifa zozote zinazoweza kusaidia kupatikana kwa mke wangu watoe ushirikiano kwa familia au vyombo vya usalama,” amesema.
Aidha, amemuomba mkewe kurejea nyumbani iwapo atapata taarifa hizo, akieleza kuwa familia yake inaendelea kumsubiri.
Tukio hilo linatokea wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha likiendelea na uchunguzi wa matukio mengine ya watu wanaodaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.
Miongoni mwa matukio hayo ni ya wasichana wawili, Kareen Didas (23) na Nakivona Toroka maarufu Rahma (22), ambao walidaiwa kutoweka tangu Juni 20, 2025 baada ya kuondoka kwenda kwenye sherehe ya usiku.
Familia ya Scola imeendelea kuomba vyombo vya usalama kuongeza juhudi za uchunguzi ili kusaidia kupatikana kwake na kudhibiti matukio ya watu kutoweka katika mazingira yasiyoeleweka.