Arusha. Wanahisa wa Benki ya CRDB wanatarajiwa kukutana jijini Arusha kujadili mafanikio ya kifedha ya benki hiyo, ikiwemo ongezeko la faida baada ya kodi iliyofikia Sh728.6 bilioni kutoka Sh551 bilioni zilizorekodiwa mwaka 2024.

Wanahisa hao pia watajadili pendekezo la Bodi ya Wakurugenzi la kuongeza gawio kutoka Sh65 kwa kila hisa mwaka 2024 hadi Sh90 kwa kila hisa mwaka huu, sawa na ongezeko la asilimia 38.

Majadiliano hayo yatafanyika katika mkutano mkuu wa 31 wa mwaka wa wanahisa wa benki hiyo unaotarajiwa kufanyika Mei 15 na 16, 2026 jijini Arusha.

Mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa na Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omary, ukiendeshwa chini ya kaulimbiu ya “Vijana na Uwekezaji katika Hisa.”

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 13, 2026 jijini Arusha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB, Profesa Neema Mori, amesema mkutano huo utatanguliwa na semina ya wanahisa itakayofanyika Mei 15 kabla ya kujadili ajenda kuu 12.

Amesema miongoni mwa ajenda zitakazowasilishwa ni taarifa ya Bodi ya Wakurugenzi, taarifa za hesabu zilizokaguliwa pamoja na pendekezo la gawio la Sh90 kwa kila hisa kwa mwaka wa fedha 2025/26.

“Pendekezo hilo la gawio linaonyesha ongezeko la asilimia 38 ukilinganisha na Sh65 zilizotolewa mwaka 2024,” amesema Profesa Mori.

Ameeleza kuwa ongezeko hilo limetokana na mwenendo mzuri wa biashara ya benki hiyo pamoja na ukuaji wa faida zake.

“Katika mwaka wa fedha uliomalizika mwaka jana, benki ilipata faida baada ya kodi ya Sh728.6 bilioni ikilinganishwa na Sh551 bilioni mwaka 2024,” amesema.

Profesa Mori ameongeza kuwa wanahisa pia watafanya uchaguzi wa mjumbe huru wa bodi, uteuzi wa wakaguzi wa hesabu pamoja na kujadili maendeleo ya jumla ya benki hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa CRDB, Dk Abdulmajid Nsekela, amesema kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu inalenga kuwahamasisha vijana kuwekeza kupitia soko la hisa.

“Tumesherehekea miaka 30 mwaka jana na sasa tunaangalia miaka 30 ijayo huku tukijiuliza ni nani watakaoipeleka mbele CRDB katika safari yake ya baadaye,” amesema Dk Nsekela.

Amesema benki hiyo inatambua kuwa vijana wa leo si wateja pekee, bali ni sehemu muhimu ya nguvu kazi ya Taifa, viongozi wa maono ya kesho pamoja na kizazi kipya cha wawekezaji.

“Ndiyo maana tumewapa kipaumbele kuanzia semina ya uwekezaji na ununuzi wa hisa,” amesema.

Dk Nsekela amesema CRDB inaamini ushiriki wa vijana katika uwekezaji wa hisa ni muhimu katika kujenga uhuru wa kifedha, utajiri endelevu pamoja na uwezeshaji wa kiuchumi wa muda mrefu.

Aidha, amewahimiza vijana wa Tanzania kutumia fursa za uwekezaji katika soko la hisa pamoja na mifumo ya kidijitali ili kujenga maisha bora ya kifedha kwa siku zijazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *