
Iringa. Kilichokuwa kikionekana kama udhaifu wa kawaida katika ukusanyaji wa ushuru wa vibali vya usafirishaji wa mifugo ndani ya Wilaya ya Iringa, sasa kimeibua taswira ya namna mianya ya rushwa na usimamizi hafifu ilivyokuwa unaomeza mapato ya kwa muda mrefu bila kubainika kirahisi.
Baada ya uchambuzi wa kina uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)katika minada ya mifugo ya Kimande na Nyang’oro, mapato ya ushuru wa vibali vya usafirishaji wa mifugo yameongezeka hadi kufikia Sh44 milioni ndani ya kipindi cha Januari hadi Machi 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 14, 2026 Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Victor Swela, amesema ongezeko hilo limetokana na maboresho yaliyofanywa baada ya kubaini mianya mbalimbali iliyokuwa ikichangia upotevu wa mapato ya Serikali.
“Takukuru ilifanya uchambuzi wa mfumo wa makusanyo ya mapato katika minada ya mifugo ya Kimande na Nyang’oro ili kubaini mianya ya rushwa na mapungufu yaliyokuwa yakisababisha upotevu wa mapato ya Serikali. Kupitia hatua hizo, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imefanikiwa kuongeza mapato hadi kufikia Sh44 milioni,” amesema Swela.
Kwa mujibu wa Swela, kabla ya taasisi hiyo kuingilia kati, katika kipindi cha Juni hadi Julai 2025 mapato ya minada hiyo yalikuwa yakifikia wastani wa Sh3.5 milioni kwa mwezi kwa minada yote miwili, hali iliyokuwa ikiibua maswali kuhusu kiwango halisi cha mapato kilichopaswa kukusanywa.
Amesema baada ya uchambuzi huo na maboresho kufanyika, mapato yaliongezeka hadi wastani wa Sh7.9 milioni kwa mwezi, jambo lililoonyesha wazi kuwa kulikuwa na mianya mikubwa ya upotevu wa fedha iliyohitaji kudhibitiwa haraka.
Katika uchunguzi huo, Takukuru ilibaini changamoto mbalimbali ikiwemo udanganyifu, ukwepaji na utoroshaji wa mifugo kutokana na maeneo ya minada kutokuwa na uzio wa kudhibiti mifugo inayoingia na kutoka.
Changamoto nyingine zilizobainika ni pamoja na ubovu wa miundombinu ya maboma ya minada na vyoo, urasimu katika utoaji wa vibali vya kusafirisha mifugo kutoka kwa watendaji wa vijiji pamoja na ucheleweshaji wa wakusanya mapato kufika maeneo ya minada.
Swela amesema baadhi ya wafugaji walikuwa wakikumbana na usumbufu usio wa lazima wakati wa kupata vibali vya kusafirisha mifugo, hali iliyokuwa ikitoa mwanya wa vitendo vya rushwa na ucheleweshaji wa huduma.
Kutokana na hali hiyo, Takukuru ilitoa mapendekezo mbalimbali kwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa lengo la kuboresha mfumo wa ukusanyaji mapato na kuziba mianya ya rushwa.
Amesema tayari halmashauri hiyo imetenga Sh22 milioni katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kujenga uzio katika mnada wa Kimande, kuweka paa kwenye banda la kukatia ushuru pamoja na kuboresha vyoo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mifugo na Kilimo Wilaya ya Iringa, Methew Sanga, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, amesema taarifa ya Takukuru imeonyesha namna usimamizi wa mapato ulivyokuwa na changamoto, huku wakiahidi kuongeza usimamizi na kuboresha miundombinu ya minada hiyo.
“Tumeweka mikakati ya kuongeza zaidi mapato katika mwaka wa fedha 2027/2028 kwa kuboresha miundombinu ya minada na kuongeza usimamizi wa ukusanyaji mapato,” amesema Sanga.
Mbali na minada ya mifugo, Takukuru Mkoa wa Iringa pia imeendelea kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri mbalimbali.
Swela amesema katika kipindi cha Januari hadi Machi 2026 taasisi hiyo ilifuatilia utekelezaji wa miradi 28 yenye thamani ya zaidi ya Sh13 bilioni ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Katika ufuatiliaji huo, amesema walibaini changamoto ya kuchelewa kuanza kwa baadhi ya miradi kutokana na ukosefu wa wazabuni na mafundi wenye uelewa wa matumizi ya mfumo wa manunuzi wa NeST, hasa katika maeneo ya pembezoni mwa miji.
Kutokana na changamoto hiyo, Takukuru ilishauri utoaji wa mafunzo kwa mafundi na wadau mbalimbali kuhusu matumizi ya mfumo huo kwa kushirikiana na Mamlaka Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA).
Katika hatua nyingine, Takukuru Mkoa wa Iringa imesema imeendelea kutoa elimu ya kupinga rushwa kwa wananchi, ambapo zaidi ya wananchi 23,426 wamefikiwa kupitia semina, mikutano ya hadhara, maonesho pamoja na klabu za kupinga rushwa.
Baadhi ya wananchi wamepongeza hatua zilizochukuliwa na Takukuru wakisema zimeanza kuleta mabadiliko katika sekta ya mifugo na ukusanyaji wa mapato.
Mkazi wa Iringa Vijijini, Juma Mwakipesile, amesema hapo awali wafugaji wengi walikuwa wakipata hasara kutokana na mazingira yasiyo rafiki katika minada hiyo.
Naye mfugaji wa kijiji cha Kimande, Paulo Mligo, amesema ucheleweshaji wa vibali na ukosefu wa usimamizi mzuri ulikuwa ukichangia baadhi ya wafugaji kutumia njia zisizo rasmi kusafirisha mifugo.
“Wafugaji wengi wanahitaji huduma za haraka na za haki. Mfumo ukiwa wazi na wa haki kila mtu atanufaika bila usumbufu,” amesema Mligo.
Katika upande wa uchunguzi na mashitaka, Swela amesema Takukuru Mkoa wa Iringa imepokea malalamiko 34 katika kipindi hicho, ambapo 33 yalihusu vitendo vya rushwa huku uchunguzi ukiendelea katika hatua mbalimbali.
Aidha, kesi moja imefunguliwa mahakamani huku nyingine ikiendelea kusikilizwa.