
Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imekuwa ikishuhudia mabadiliko makubwa katika namna watu wanavyopata kipato, hasa miongoni mwa vijana waliokumbatia teknolojia.
Kuibuka kwa kile kinachoitwa “digital hustle” yaani kufanya kazi mtandaoni kama uandishi wa maudhui, usanifu wa picha, programu, utafiti, tafsiri, na huduma za kidijitali kumeibua mjadala mpya.
Mjadala wenyewe ni je, wafanyakazi huru wa mtandaoni (online freelancers) ndio sura mpya ya tabaka la kati nchini? Kwa muda mrefu, dhana ya tabaka la kati Tanzania imehusishwa na ajira rasmi serikalini au sekta binafsi, mishahara ya uhakika, na maisha yenye uthabiti wa kifedha.
Hiyo ni ishara kuwa mapinduzi ya kidijitali yameanza kuvunja mipaka hii, yakitoa fursa kwa watu kujijengea kipato bila kufungwa na ofisi au mwajiri mmoja. Vijana wengi sasa wanapata wateja kutoka nje ya nchi kupitia majukwaa mbalimbali, wakilipwa kwa dola au sarafu nyingine za kigeni, hali inayowawezesha kupata kipato kinachozidi hata mishahara ya baadhi ya ajira rasmi za ndani.
Hii imewawezesha kumudu gharama za maisha mijini, kuwekeza katika mali kama viwanja na nyumba, na hata kusaidia familia zao vijijini sifa ambazo kwa kawaida zilihusishwa na tabaka la kati. Hata hivyo, pamoja na mafanikio haya, kuna changamoto zinazotia shaka uimara wa kundi hili jipya.
Kwanza, kipato cha ‘freelancing’ mara nyingi si cha uhakika; kinaweza kubadilika kulingana na upatikanaji wa kazi, ushindani wa kimataifa, na mabadiliko ya mahitaji ya soko.
Pili, wengi wa wafanyakazi hawa hawana ulinzi wa kijamii kama bima ya afya, mafao ya kustaafu, au mikataba ya kudumu, jambo linalowaweka katika hatari ya kuyumba kiuchumi pindi wanapokumbwa na matatizo ya kiafya au kushuka kwa kazi.
Tatu, bado kuna changamoto za miundombinu kama intaneti isiyo na uhakika katika baadhi ya maeneo, gharama za vifaa, na uelewa mdogo wa sera na kodi zinazohusu kipato cha mtandaoni.
Hata hivyo, mchango wa ‘digital hustle’ katika uchumi hauwezi kupuuzwa. Inaongeza ajira zisizo rasmi lakini zenye tija, inaleta fedha za kigeni nchini, na inakuza ujuzi wa kidijitali ambao ni muhimu katika dunia ya sasa.
Zaidi ya hayo, imepanua wigo wa fursa kwa makundi ambayo hapo awali yalikuwa na vikwazo vya ajira, kama wanawake wanaolea watoto nyumbani au vijana waliopo maeneo ya mbali.
Hata hivyo ili kundi hili liweze kuwa tabaka la kati imara na endelevu, ni muhimu kuwa na maboresho ya miundombinu ya Tehama, kutoa elimu ya kifedha na ujasiriamali wa kidijitali, kuweka mifumo rafiki ya kodi, kuhamasisha ubunifu na utofauti wa ujuzi ili ‘freelancers’ wasitegemee soko moja au aina moja ya kazi.
Kwa mtazamo mpana, wafanyakazi huru wa mtandaoni wana kila dalili ya kuwa sehemu muhimu ya tabaka la kati la Tanzania, lakini bado wako katika hatua ya mpito.
Mafanikio yao yatategemea si tu juhudi binafsi, bali pia mazingira wezeshi ya sera na uchumi. Ikiwa fursa hizi zitaimarishwa ipasavyo, “digital hustle” inaweza kuwa si tu njia ya kujipatia kipato, bali daraja jipya la kupanda kiuchumi kwa maelfu ya Watanzania.