
Geita. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Geita imepokea na kufanya uchunguzi wa malalamiko 75 yaliyotolewa na wananchi katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Mei 14, 2026, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Geita, James Ruge amefafanua kuwa miongoni mwa malalamiko hayo, 62 ambayo ni sawa na asilimia 82 yalihusu makosa ya rushwa huku malalamiko 13 sawa na asilimia 18 hayakuhusu rushwa.
“Taarifa zilizohusu rushwa zilianzishiwa uchunguzi, wakati zile zisizohusu rushwa ushauri ulitolewa na nyingine tuliwasilisha kwenye taasisi za mamlaka husika ili zifanyiwe kazi.”
Aidha, katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka kuanzia Januari hadi Machi 2026, kesi tatu zilizohusiana na taasisi hiyo zilitolewa uamuzi huku Jamhuri ikishinda zote. Pia katika kipindi hicho kesi mpya zimefunguliwa mahakamani.
Pia taasisi hiyo imesaidia kurejeshwa kwa zaidi ya Sh15.81 milioni ambazo ni fedha za maendeleo ambapo baadhi yake zilikuwa zimefanyiwa ubadhirifu, malipo yaliyokuwa yamefanyika kinyume cha utaratibu pamoja na fedha za makusanyo ya ushuru ambazo zilikuwa hazijalipwa kwenye maeneo husika.
Katika hatua nyingine, Takukuru mkoani humo ilitekeleza agizo lililotolewa na Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba aliyeagiza kufanyika kwa uchunguzi kwenye mradi wa ujenzi wa Chuo cha Veta kilichopo Wilaya ya Nyang’wale mkoani humo.
Dk Nchemba alitoa agizo hilo Machi 4, 2026 katika Soko la Machinga jijini Dodoma alipokuwa amesimama kuzungumza na wafanyabiashara katika soko hilo wakati akitokea mkoani Arusha kwenye ziara ya kikazi.
Dk Mwigulu alisema, “Nikiwa Arusha nilimsikiliza fundi yule aliyekuwa anajenga VETA kule Nyang’wale, nimetuma vyanzo vyangu. Watu wanatengeneza dili la kula fedha, wanatafuta makandarasi wao ili wagawane fedha.”
Pia Dk Mwigulu aliongeza kuwa, “Sasa Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Geita nenda kachunguze, niipate hiyo taarifa, hatua zichukuliwe.”
Kufuatia agizo hilo, Ruge amesema agizo hilo limetekelezwa kwa taasisi hiyo kufanya uchunguzi uliowezesha mradi huo kuendelea kutekelezwa ambapo kwa sasa ujenzi umefikia asilimia 87. Pia amesema ufuatiliaji katika mradi huo unaendelea ili ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyohitajika.
Aidha, Takukuru imewaomba wananchi mkoani humo kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa kuhusu viashiria na vitendo vya rushwa kwa maslahi ya maendeleo endelevu ya nchi.