RMO aagiza ukusanyaji fedha kulipa madeni ya MSDRMO aagiza ukusanyaji fedha kulipa madeni ya MSD

Dodoma. Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (RMO), Dk Thomas Rutachunzibwa ameziagiza taasisi za afya kukusanya fedha ili zilipe madeni ya Bohari ya Dawa (MSD) kwa wakati, huku akiwataka wanaoagiza dawa kuzingatia mahitaji halisi ya vituo vyao.

Dk Rutachunzibwa amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto ya dawa kuagizwa kwa wingi na kushindwa kutumika kwa wakati, hali iliyobainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha wateja na wadau wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Kati.

“Tumewaita pamoja na wataalamu wa fedha kwa ajili ya kuwekana sawa, ili tuweze kununua dawa lazima tuwe na fedha, hivyo nawasihi makatibu wa afya na wataalamu wote kuangalia mahitaji halisi yanayoletwa na wafamasia,” alisema Dk Rutachunzibwa.

Washiriki katika kikao cha Wadau wa madawa.

Naye Mkurugenzi wa Ugavi wa MSD, Hassan Ibrahim amesema wataalamu wa sekta ya afya wana wajibu wa kushirikiana ili kutatua changamoto zinazojitokeza katika mnyororo wa ugavi wa dawa na vifaa tiba.

Ibrahim amesema ni muhimu kundi hilo wakaongea lugha moja katika kutatua changamoto na kuzifanyia kazi kwa pamoja, lakini wawe na uwezo wa kujadiliana na kusaidiana kuzitatua.

Aidha, aliwataka wataalamu hao kuwekeza zaidi katika matumizi ya Tehama ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya teknolojia.

Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma, Mwanashehe Jumaa, amesema mkutano huo unalenga kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wakati lakini kuimarisha ushirikiano wa wadau wote wanaohusika katika mnyororo wa ugavi.

Jumaa amesema MSD ina utaratibu wa kukutana na wadau wake kila mwaka, hivyo wamewaita wateja wao wanaohudumiwa katika mikoa ya Dodoma na Singida kwa lengo la kupata mrejesho kutoka kwa wateja na kuboresha mawasiliano na mahusiano.

Amesema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni miundombinu mibovu inayosababisha ugumu wa usambazaji wa dawa na vifaa tiba, hasa katika kipindi hiki cha mvua nyingi.

Akitoa taarifa ya usuluhishi wa vifaa tiba, Mfamasia kutoka Mkoa wa Singida, Elikana Mbando, amesema mkoa huo ulifanya usuluhishi wa vifaa tiba kuanzia mwaka 2023 hadi 2026 wenye thamani ya Sh3.4 bilioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *