Ndani ya Boksi: Kuna Kiba, kuna Mondi, kuna nyama choma Ndani ya Boksi: Kuna Kiba, kuna Mondi, kuna nyama choma 

Dar es  Salaam. Kiba aliupa kisogo muziki wake. Kabla hajainuka upya na kukaza mpaka leo. Kabla hajajulikana kama King Kiba zaidi ya Alikiba. Ujio wake wa pili ukazalisha jina la King Kiba, ili kuweka utofauti wa yeye na matoleo mapya ya wanamuziki kama Mondi Bin Laden. 

Kifupi tunaweza kusema Mondi, alimfukua Kiba. Akamsimamisha upya ‘dairekti au indairekti’. Hata mafanikio ya Alikiba ni tofauti na mafanikio ya King Kiba. Yule Ally alikuwa na mafanikio ya kawaida, ya magari, kula na kuvaa vizuri, ila King Kiba akawa noma zaidi.

Huu ndio ushindani bora zaidi wa muziki. Huu ndio ushindani wenye faida zaidi wa mastaa wakubwa. Huu ndio ushindani wenye harufu ya pesa zaidi. Badala ya damu au ngeu usoni. Kiba alimuhamasisha Mondi kutoka mtaani, na Mondi alimuinua Kiba toka usingizini. 

Wengi walitamani kuwa Alikiba, miongoni mwao ni Diamond. Na kuna wengi waliguswa na kasi ya mafanikio ya Diamond, miongoni mwao ni Alikiba. Hawa wawili ni wazi kwamba walitegemeana na sasa wanategemeana kwa kiasi kikubwa. 

Madogo hao wamevuka mipaka ya muziki mzuri tu. Hushindana hata kwa uwekezaji na maisha kwa ujumla. Ushindani uliogeuka neema kubwa sana kwa maisha yao. Hawa siyo mabosi wa kizazi ya wanamuziki tu, ni mabosi kwa watu wa nje ya muziki. 

Nini maana yake? Msanii yeyote angeweza kuwa Alikiba kama tu angemtazama Mond kiushindani. Na yeyote angeweza kuwa Mond kama Kiba angekuwa kioo chake. Kwa sababu wakati anapukuta vumbi ili akae, alikuwa na ngoma moja inayosumbua mitaani.

Alikiba akiwa na Shudelele, kuna Q Chillah alikuwa Tanita na TID alikuwa na Asha. Poteza muda vuta memori ya ngoma hizo. Ina maana Chillah au TID, yeyote kati yao angeamua kumvagaa Mondi leo wangekuwa pale alipo Kiba. Unajua kwanini? Tuendelee.

Kabla ya Kiba kurudi upya, Mondi alitawala gemu hili. Alimfunika Belle 9, Rich Mavoko, Barnaba na Marlaw pamoja na Suma Lee na Hakunaga yake. Wabongo hapo wakaanza kusaka mtu wa kumpa changamoto Mondi. Kwa sababu ndio wanachotaka.

Wabongo hawapendi mtu mmoja akawa yeye tu pale juu. Watataka tu kusaka mtu wa kumkanyagia au kumzima. Ndio maana Alikiba alipoibuka upya akasomba kijiji nyuma yake. Ilikuwa kiu ya muda mrefu ya watu kuona Diamond anapata upinzani. 

Ni nyakati zile Diamond alikuwa juu kama mbalamwezi. Magazeti hayaendi kitaa bila sura yake na Wema. Alikuwa akiibuka sehemu anavuruga utaratibu, kama kile kilichotokea kwenye msiba wa Kanumba. Mondi alilifanya eneo la msiba ligeuke shangwe.

Hata uwe unajua namna gani au kufunika kiasi gani. Wabongo ni kawaida yao kuona unakutana na upinzani. Hawapendi uwe juu kila siku wewe peke yako. Hiki ndicho kilichomsimamisha Kiba mpaka leo. Hata wimbo wa Mwana, siyo viwango vya Mondi ila basi tu. 

Wakatembea na Alikiba licha ya kutoa wimbo wa kawaida mbele ya pini za Mondi. Mwana ukawa mkubwa kwa kulazimisha hata kuuweka eneo moja na mapini ya Mondi. Wimbo mkubwa wa Kiba kwa Mondi ulikuwa Seduce Me, zingine zilibebwa na oya oya.

Lakini ndo mwanamuziki pekee aliyebeba ndoto za waliotamani kuona Mondi hakai peke yake kileleni. Matokeo yake Ben Pol na wengine pamoja na ukali wa pini zao, ulifubaishwa na ushindani wa Mondi na Kiba. Hata Darassa na ukali wake alikaa katikati yao.

Mondi kwa miaka 15 yupo juu kileleni. Akiongoza wenzake kwa kila kitu. Ngoma kali, shoo kali, video kali, madem wakali, ndinga kali na kila kitu. Hajayumba hata mara moja, kawa na muendelezo bora wa kazi na madili ‘nanstop’ kwa miaka yote tangu pini lake la Kamwambie.

‘Hakunaga’ mwanamuziki yeyote kabla, aliyekaa kileleni kiasi hiki. Miaka kwa mfululizo anaongoza kwa namba zote za kimuziki na biashara ya muziki. Pamoja na misukosuko mingi amekomaa bila kuyumba kiuwezo wa sanaa na uwezo wa kipesa. Anapaa deile.

Kuna watu wanakuja na kupotea. Kuna vitu vinakuja na kupotea. Na kuna vitu hugeuka historia. Miaka 15 sasa, Nyama Choma Festival imeendelea kuwa moja ya matukio makubwa na kuwa zaidi ya tamasha. Tamasha la Fiesta lilikuwa namba moja leo imebaki stori.

Lakini Nyama Choma imegueka kuwa ‘laifu staili’ au utamaduni na kumbukumbu kwa maelfu ya watu. Harufu ya nyama hewani, vicheko vya totozi na jentromani. Muziki mzuri, washikaji kukutana eneo moja. Imekuwa kiunganishi cha watu kuwa kitu kimoja kila mwaka. 

Hata Nyama Choma Festival ina miaka 15 ‘marodini’. Haijwahi kuyumba wala kufubaa, deile ikifanyika kuna ‘vaibu na testi’ ya tofauti. Kudumu namna hii ndani ya mioyo ya watu, lazima uwe mbunifu na mwendelezo bora na kujua ‘pipo’ zinataka nini. 

Nyama Choma Festival siyo tukio la kawaida ni ‘tradishino’. Na kitu kingine kikubwa kuhusu Nyama Choma ni vile inavyobeba mizuka ya Kibongo zaidi. Utakutana na ‘fuudi lavaz’, ‘influensaz’, mastaa, wasanii, marafiki, familia na kila apendaye kula vizuri na kufurahia maisha. 

Ni kama ‘riyunioni” ya machizi ‘menyu’. ‘Honestli’, katika dunia hii ya ‘trends’ nyingi zinazodedi fasta. Kuona ‘iventi’ au ‘brandi’ ‘ikisavaivu’ kwa miaka 15 huu ni ushindi mkubwa. Inaonesha kuna watu nyuma wana kazi yao tena siyo kwa mazoea bali ni ‘pasheni’ yao. 

Nyama Choma Festival, ni wazi inaonesha Wabongo tunaweza kufanya jambo katika sura zenye kiwango cha kimataifa. Na huku tukibaki na ‘identiti’ yetu ileile ya kiswahili na mtaa wenye mzuka. Nyama Choma kwa sasa wapo katika daraja lilelile la Sauti Za Busara. Kimataifa zaidi.

Tarehe 6-6-2026 inatimia miaka 15 ya moshi wenye harufu za vitoweo, ladha, muziki, urafiki na kumbukumbu zenye uhai. Na bado safari inaendelea na sioni mwisho wake. 
‘Rispekti’ ziende wa ‘oganaiza’, ‘sapotazi’ na kila aliye sehemu ya huu mchongo tangu ‘dei wani’ mpaka leo. Nami nitakuwepo.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *