
Bagamoyo. Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani imenunua Gereda mpya yenye thamani ya Sh1.2 bilioni kwa lengo la kuboresha miundombinu ya barabara na kuondokana na gharama kubwa za kukodisha mitambo hiyo iliyokuwa ikigharimu kati ya Sh800,000 hadi Sh1 milioni kwa siku.
Hatua hiyo imetajwa kuwa mkombozi kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya halmashauri hiyo, huku viongozi wakisema itanufaisha sekta ya uchumi kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao, huduma za kijamii na shughuli nyingine za maendeleo.
Akizungumza leo Mei 14,2026 katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya ya Chalinze, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Leon Mgweno amesema awali walikuwa wakilazimika kukodisha gereda kwa gharama kubwa jambo lililokuwa likipunguza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya barabara.
Amesema kutokana na changamoto hiyo, halmashauri imeamua kutumia mapato ya ndani kununua geader hiyo ili iwe suluhisho la kudumu katika ukarabati na ujenzi wa barabara za ndani.
“Kwa muda mrefu tulikuwa tunatumia fedha nyingi kukodisha gereda kwa siku, lakini sasa tumepata suluhisho la kudumu. Mitambo hii itatusaidia kufungua na kuboresha barabara nyingi za wananchi na kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi,” amesema Mgweno.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze, Ramadhani Possi amesema ununuzi wa gerede hiyo ni sehemu ya mkakati wa halmashauri kuimarisha miundombinu kwa kutumia mapato ya ndani.
Amesema barabara bora zitasaidia kukuza uchumi wa wananchi kwa kurahisisha usafiri wa bidhaa, mazao ya kilimo na huduma za kijamii katika kata mbalimbali za halmashauri hiyo.
“Tunataka kuona wananchi wanapata huduma bora za usafiri wakati wote. Gereda hii itatumika kikamilifu kuhakikisha barabara zinapitika na shughuli za maendeleo zinaendelea bila vikwazo,” amesema Possi.
Baadhi ya wananchi wamepongeza hatua hiyo huku wakitaka ?tambo huo utumike kwa ufanisi katika ukarabati wa barabara za mitaa na vijiji.
Mkazi wa Kata ya Bwilingu, Moreti Manya amesema barabara nyingi zimekuwa zikiharibika hasa kipindi cha mvua, hivyo ujio wa mtambo huo utasaidia kupunguza adha ya usafiri.
“Tunaiomba halmashauri kuhakikisha gereda hilo linafanya kazi kwa wananchi waliokusudiwa ili barabara za mitaa yetu zibaki katika hali nzuri muda wote,” amesema Manya.
Naye mkazi wa Kata ya Vigwaza, Selina Mkomwa amesema wananchi wanatarajia kuona mabadiliko ya haraka katika miundombinu ya barabara baada ya ununuzi wa mtambo huo.
“Barabara nzuri ni msingi wa maendeleo. Tunatarajia maeneo mengi yatapata huduma ya ukarabati kwa wakati tofauti na ilivyokuwa zamani,” amesema Mkomwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ni miongoni mwa halmashauri za Mkoa wa Pwani zilizoundwa kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi baada ya kugawanywa kwa baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Bagamoyo.
Halmashauri hiyo imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, huduma za elimu, afya na maji kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi wake.
