
Kigali. Benki ya NMB Plc imepata ufadhili wa takribani Sh468.1 bilioni kwa ajili ya kuongeza mikopo kwa biashara ndogo na za kati, sekta ya kilimo, wanawake wajasiriamali na biashara zinazoongozwa na vijana nchini Tanzania.
Ufadhili huo unajumuisha Dola 100 milioni za Marekani (Sh260 bilioni) kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa, (IFC), Dola 50 milioni (Sh130 bilioni) kutoka British International Investment, BII na Dola 30 milioni kutoka Norfund, sawa na Sh78 bilioni.
Makubaliano hayo yalisainiwa juzi jijini Kigali, nchini Rwanda, pembezoni mwa Mkutano wa Wakurugenzi Wakuu Afrika, Africa CEO Forum, unaowakutanisha viongozi wa biashara, wawekezaji, taasisi za maendeleo na watunga sera kujadili uwekezaji na mwelekeo wa ukuaji wa uchumi barani Afrika.
Kwa mujibu wa NMB, fedha hizo zitaongeza uwezo wa benki kutoa mikopo ya muda mrefu na yenye muundo unaoendana na mahitaji ya biashara katika sekta za uzalishaji.
Ufadhili huo unalenga kusaidia biashara zenye uwezo wa kukua, hususan zile zinazohitaji mtaji wa uendeshaji, fedha za uwekezaji na uwezo wa kuimarisha minyororo ya thamani.
NMB imeeleza kuwa, sehemu ya ufadhili huo itatolewa kwa dola za Marekani na shilingi ya Tanzania, hatua inayolenga kupunguza changamoto zinazowakabili wakopaji, ikiwamo upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu na athari za mabadiliko ya thamani ya fedha za kigeni kwa baadhi ya biashara.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna amesema makubaliano hayo yanaonesha kuongezeka kwa imani ya taasisi za kimataifa kwa mkakati, uongozi na mchango wa NMB katika maendeleo ya Tanzania.
“Kupata ufadhili huu kutoka IFC, BII na Norfund ni hatua muhimu kwa NMB na uthibitisho wa imani katika mkakati wetu wa ukuaji.
“Mtaji huu wa muda mrefu utatuwezesha kuongeza mikopo kwa biashara ndogo na za kati, sekta ya kilimo, wanawake wajasiriamali na biashara zinazoongozwa na vijana, maeneo ambayo ni muhimu katika kuongeza uzalishaji, ubunifu na ajira,” amesema Zaipuna.
Amesema ufadhili huo unaendana na Mpango Mkakati wa NMB wa mwaka 2026-2030, ajenda 2030, pamoja na vipaumbele vya maendeleo ya Taifa, ikiwamo kukuza uchumi unaoongozwa na sekta binafsi, kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kuchochea ukuaji jumuishi.
Amesema NMB itaendelea kutumia ushirikiano wa kimataifa kupanua huduma za kifedha, kubuni bidhaa zinazojibu mahitaji ya wateja na kuongeza mikopo katika minyororo ya thamani ya kilimo, kuanzia pembejeo, uzalishaji, ukusanyaji, usindikaji, usafirishaji hadi masoko.
Mkurugenzi Mtendaji na Mkuu wa Kanda ya Afrika wa BII, Chris Chijiutomi amesema uwekezaji huo unaendeleza uhusiano wa muda mrefu kati ya BII na NMB, baada ya BII kushiriki katika hati fungani endelevu ya Jamii Bond ya NMB mwaka 2023.
“Ahadi hii mpya inaendeleza ushirikiano wetu wa muda mrefu na NMB Bank. BII inaunga mkono ukuaji jumuishi na thabiti wa Tanzania kupitia juhudi za NMB kutoa suluhisho za kifedha zinazolenga mahitaji ya wafanyabiashara ambao hawajafikiwa au biashara zao hazijafikiwa kikamilifu,” amesema Chijiutomi.
Norfund pia imesisitiza umuhimu wa kuimarisha sekta za ndani, hasa kilimo na biashara ndogo, ili kuongeza ajira, tija na ushiriki mpana wa wananchi katika uchumi.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kuchochea uwekezaji katika sekta ya kilimo na minyororo yake ya thamani, kuongeza thamani ya mazao, kuimarisha uhusiano kati ya kilimo na viwanda, na kufungua fursa zaidi za biashara na ajira.
Hatua hiyo pia inaonesha kuongezeka kwa imani ya taasisi za fedha za kimataifa katika sekta ya fedha ya Tanzania na uwezo wa NMB kuelekeza mitaji katika maeneo yenye tija kwa uchumi.
