Sowah atoweka Simba, ataja sababu za kukacha mazoeziSowah atoweka Simba, ataja sababu za kukacha mazoezi

WAKATI sintofahamu ikiendelea ndani ya Simba kuhusu hatma ya mshambuliaji Jonathan Sowah, yeye mwenyewe amefunguka ishu ya kuondoka nchini na kurejea kwao Ghana huku mgogoro wake na klabu hiyo ukizidi kuchukua sura mpya.

Sowah aliyetua Simba mwanzoni mwa msimu huu, alifanya vizuri akiwa na Singida Black Stars msimu uliopita 2024-2025 alipoitumikia kwa miezi sita na kuacha rekodi ya mabao 13 Ligi Kuu Bara akicheza mechi 14.

SOWA 01

Ubora huo uliifanya Simba kumsajili lakini hakuwa na bahati na klabu hiyo baada ya kuanza kwa spidi ndogo na mwisho akawa hana uhakika wa namba kwenye timu hiyo.

Mshambuliaji huyo amecheza mechi tatu za Ligi Kuu msimu huu kwa dakika 247, akiweka rekodi ya kufunga mabao matatu, hata hivyo katikati mwa msimu alipewa adhabu na Kamati ya Usimamizi wa Ligi kwa kufungiwa mechi tatu, baadaye akafanya utovu wa nidhamu uliosababisha Simba kumsimamisha kwa muda kisha kumpleka kufanya mazoezi na timu ya vijana chini ya miaka 20.

SOWA 02

Hata hivyo, hivi karibuni Mwanaspoti liliripoti kuwa mshambuliaji huyo hakwenda hata siku moja kwenye mazoezi hayo huku ikidaiwa kuwa uongozi wa klabu hiyo haufahamu alipo kwa sasa.

“Sisi hatufahamu alipo, simu zake hazipatikani na rafiki zake pia hawajui alipo, sisi bado tunamlipa kama kawaida, tutajua baadaye itakavyokuwa,” kilisema chanzo kutoka Simba.

SOWA 03

Baada ya taarifa hiyo, Mwanaspoti liliingia kwenye harakati za kumtafuta mshambuliaji huyo ili kufahamu nini kinaendelea, namba zake zote hazikuwa zinapatikana.

Katika juhudi za kuendelea kumtafuta, rafiki yake wa karibu akatoa namba inayopatikana ambapo Sowah akaliambia Mwanaspoti yupo kwao Ghana.

SOWA 04

Akizungumza na Mwanaspoti, mshambuliaji huyo amesema ameamua kuondoka baada ya kuona hakuna msaada wa haraka alioupata kuhusiana na hali yake ndani ya Simba, huku pia mazungumzo kati yake na uongozi wa klabu hiyo yakidaiwa kugonga mwamba.

“Nani amekupa hii namba?” alihoji Sowah kisha akaendelea kusema.

“Mimi nimeondoka, nipo Ghana kwetu, nilikuwa nahitaji msaada wa haraka kuhusu hali yangu, lakini mpaka sasa hakuna ambacho kimeafikiwa kati yangu na uongozi.

SOWA 05

“Nimepambana na kwenda kwenye kamati mbalimbali lakini nimekosa msaada, mwisho nimeamua kuondoka, nipo kwetu sasa, sijui nini kitatokea baadaye lakini nafahamu kuwa sina kosa,” amesema Sowah na kuomba mwandishi akate simu.

Kwa upande wa Simba, chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kimeliambia Mwanaspoti kuwa: “Alipewa nafasi ya kwenda kufanya mazoezi na timu ya vijana lakini hajaenda. Kwa sasa hapatikani hewani na tayari tumewasiliana na wasimamizi wake tukimtaka ajisalimishe haraka kabla ya kuchukuliwa hatua nyingine kubwa zaidi.”

SOWA 04

Simba pia imeweka wazi kuwa pamoja na Sowah kutokuwa sehemu ya kikosi kinachocheza kwa sasa, mshambuliaji huyo bado anaendelea kupokea mshahara wake kama ilivyo kwa wachezaji wengine wenye mikataba ndani ya klabu hiyo.

“Bado ni mchezaji wa Simba na anapokea mshahara wake kama kawaida, ndiyo maana anatakiwa kufuata taratibu za klabu,” kiliongeza chanzo hicho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *