Studio mpya ya Twanga Pepeta, inapokea vipaji vyoteStudio mpya ya Twanga Pepeta, inapokea vipaji vyote

Dar es Salaam. Uzinduzi wa studio mpya ya muziki ya Twanga Pepeta Entertainment ulifanyika Mei 17, 2026 katika eneo la Magomeni Usalama, Mtaa wa Minaki jijini Dar es Salaam, huku viongozi wa bendi hiyo wakieleza kuwa studio hiyo imeanzishwa kwa lengo la kukuza vipaji vya wasanii wa muziki wa aina mbalimbali pamoja na kurekodi matangazo ya sauti kwa ubora wa kisasa.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa sanaa na burudani waliokwenda kushuhudia hatua mpya ya mandeleo ya bendi hiyo kongwe ya muziki wa dansi nchini.

Katika hafla hiyo, viongozi wa Twanga Pepeta walisema studio hiyo itakuwa wazi kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya, taarabu, dansi, singeli, gospel pamoja na watayarishaji wa matangazo ya redio na televisheni, wakieleza kuwa dhamira yao ni kutoa nafasi kwa vipaji vipya na kuhakikisha kazi za wasanii zinarekodiwa kwa viwango bora vya kimataifa.

Mbali na uzinduzi wa studio hiyo, hafla hiyo pia ilitumika kutambulisha rasmi uzinduzi wa albamu mpya ya 16 ya Twanga Pepeta, ambayo inatarajiwa kuzinduliwa Agosti 7, 2026 kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Sambamba na hilo, bendi hiyo pia ilitambulisha vyombo vipya vya muziki vitakavyotumika kuongeza ubora wa maonesho yao jukwaani.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mratibu Mkuu wa uzinduzi huo, Steve Nyerere alisema ujio wa studio hiyo ni mwanzo wa mapinduzi mapya katika muziki wa dansi nchini, huku akiwakaribisha wasanii kutoka maeneo mbalimbali kutumia fursa hiyo kukuza kazi zao za sanaa.

“Twanga Pepeta ni taasisi kubwa ya muziki ambayo imekuwa ikitoa burudani kwa miaka mingi sana, lakini leo tumeamua kwenda hatua nyingine kwa kufungua studio ya kisasa ambayo itatoa nafasi kwa kila msanii mwenye ndoto za kufanya muziki wenye ubora.

Hapa si kwa wanamuziki wa dansi pekee, tunawakaribisha wasanii wa aina zote pamoja na watu wa matangazo ya sauti kuja kufanya kazi zao katika mazingira bora na ya kisasa,” amesema Steve Nyerere.

Ameongeza kuwa, uzinduzi wa albamu hiyo mpya pamoja na vyombo vipya ni sehemu ya maandalizi ya kuirudisha Twanga Pepeta katika ushindani mkubwa wa muziki wa dansi Afrika Mashariki, huku akiahidi mashabiki kupata burudani ya kiwango cha juu katika tamasha la Agosti 7 litakalofanyika Mlimani City.

“Tunataka mashabiki waone kuwa Twanga Pepeta bado ipo imara na inaendelea kujiandaa kwa kizazi cha sasa. Albamu hii ya 16 imeandaliwa kwa ubora mkubwa, vyombo vipya vimeongezwa na tunaamini tamasha la Agosti 7 litakuwa historia nyingine kubwa kwa muziki wa dansi nchini.

“Tunawaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi kuunga mkono kazi hii kubwa ya sanaa,” amesema Steve Nyerere

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *