
Unaweza kumwona mdudu kama kitu kisicho na sababu ya kuishi. Lakini tofauti kubwa ni kwamba mdudu ana maajabu makubwa kuliko binadamu. Pamoja na udogo wake, ana ratiba ya kazi isiyovurugika, ana ulinzi usiotegemea silaha za moto, na ana uzalendo usiomithilika kwenye jamii yake. Kwa mfano mbu anaweza kumnyonya mwanadamu kwa kutumia mrija wake, lakini binadamu ni lazima atengeneze mirija ya rushwa kumnyonya binadamu mwenzie.
Matendo ya nyuki na mchwa yanafanana kwa kiasi kikubwa. Nyuki laki mbili wanaweza kushonana kwenye mzinga mmoja. Mchwa wanazidi hata milioni moja kwa kila kichuguu. Wote wanafanya sensa ya makazi; wanajua nani kafa vitani na nani kajeruhiwa. Ajabu kubwa wanamjua mgeni aliyehamia kwenye chumba cha marehemu. Wanaihisi harufu yake kama sisi tunavyohisi harufu ya kwapa. Kila mmoja ana yake, hivyo ya tofauti inaeleweka.
Mifumo ya wadudu inashabihiana na ya binadamu wa mataifa mengi kasoro Tanzania. Kinachotufanya Watanzania kuwa tofauti na wengine ni utamaduni wao. Wana makabila zaidi ya 200 na kila kabila likiwa na utamaduni wake. Lakini tamaduni hizi zimeungana kiasi cha Mkurya kutoibagua harufu ya Mmakonde wa Newala. Mwera mwenye nyota ya kondoo anaweza kuwa Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Mara, ambao una nyoya ya nge!
Mwanzoni tamaduni za eneo moja zililindwa kutochangamana na makabila tofauti. Kila moja ilijiona kuwa sahihi kwenye matambiko yake bila kuikosanisha na muumba wake. Lakini ikaja nguvu ya kisiasa iliyofuta tofauti za jamii zetu. Hapa sichelei kumtaja muasisi wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mwalimu alitumia changamoto kama fursa. Utofauti wa maisha ya watu ukawa utani. Wahaya waliokula ndizi na kuishi kwa mila zao za kichifu, wakataniana na mahasimu wao Wasukuma waliokuwa wakitumia nguvu nyingi kwenye mashamba na ufugaji wa ng’ombe. Msukuma alimtania mwenzake kwa “ustaarabu” wake wa kula ndizi, maana kwa Msukuma ndizi ni sawa na kupiga mswaki. Mwenzake akamjibu “hangaika na miguvu kwenye ng’ombe na mashamba.”
Wamwera na Wamatumbi ni majirani. Utani wao unatokana na ushindani wa kijamii, mila, na tofauti za lafudhi. Mara nyingi walitaniana kuhusu ujasiri, uvivu, au namna ya kuzungumza. Lakini kwa sababu mabosi wa kimwera waliotoka Dar es Salaam walipaswa kuvuka kwa Wamatumbi katika Mto Rufiji, Wamatumbi wakajichukulia kuwa mabosi wa mabosi hao. Siku wakifunga njia walikula pesa zao zote za likizo.
Wachaga na Wapare nao ni majirani wa maeneo ya Kilimanjaro na Pare. Historia yao ina biashara ya muda mrefu, ndoa, na kushirikiana kiuchumi. Mara nyingi Wachaga hutaniwa kuwa wapenda hela. Mchaga akisikia mlio wa shilingi inayodondoka sakafuni, huzinduka hata kama alikuwa akifanyiwa upasuaji. Lakini naye humtania Mpare kwa ubahili na kupenda kesi. Inasemekana Mpare yu radhi kuuza ng’ombe ili kusimamia kesi ya kuibiwa bakora.
Wazaramo na Wangoni walisumbuana kutokana na tofauti ya maisha ya pwani dhidi ya maisha ya kijeshi ya Wangoni. Wazaramo wanajichukulia kuwa wenyeji wa kitovu cha biashara nchini. lakini Wangoni ni wababe wa vita, na vita bila kuteka vitovu vya biashara haina maana hata kidogo. Ndio maana Wangoni ni watani wa karibu makabila yote ya kibongo. Usicheze na wajukuu wa Chaka Zulu…
Inasemekana tangu enzi za maagano, nchi hii ina alama zake. Mpaka pale dunia ilipotamka kuwa maisha ya mtu wa mwanzo yalikuwa hapa, sisi wenyewe tulishangaa. Wengine wana yao ya kale kule Singidani, lakini kuna wanaoamini kuwa safina ya Nuhu ilitua Kilimanjaro! Mi nasikia tu ati Ngorongoro Crater nayo inahusika. Ebu tuachane na mambo ya kusikia, tuongee lile linalotuweka hapa.
Kuna mahala kama tumepoteza thamani ya Mtanzania wa kawaida. Baada ya kubaguliwa kielimu wakati wa ukoloni, sasa anapambana kusomesha watoto wake kwa machozi, jasho na damu. Kila siku analazimika kulipia bando la karatasi, ada za mitihani na twisheni, nauli za kuwafikisha shule, mchango ya ulinzi, chakula usafi na kadhalika. Lakini kule mwishoni hata mtoto akifanya vizuri kwa kiasi, haoni faida ya kuwahangaikia kiasi hicho.
Watoto wa siku hizi nao wana akili kama mchwa. Wanapima akili wa kukokotoa hesabu za darasani, dhidi ya kuandika ukurasa mmoja wa mistari ya bongofleva. Wanaiona tofauti baina ya mwalimu anayelipwa milioni moja, daktari anayepata milioni mbili pamoja na ya mazingira hatarishi, au mbunge wa darasa la saba anayechukua milioni zote, miksa posho za vikao, za kamati, za safari za kikazi, marupurupu ya usafiri na mawasiliano, bila kusahau kiinua mgongo kizito baada ya majukumu.
Ndio maana vijana wetu wamekuwa na shingo ngumu. Wanawaza pengine wangebaki na milioni kadhaa baada ya kulipa gharama za wapiga picha, wacheza muziki na kadhalika. Vinginevyo basi waunganishe na siasa, maana wanaona jinsi wazee wanavyoachana na taaluma wakawekeza kwenye sìasa. Niseme ukweli, Mtanzania wa leo anajiona kama mfugo anayeongozwa machungani. Thamani yake ionekane na elimu sahihi bado inahitajika.
