Mtihani kwa Tume ya Uchunguzi wa KijinaiMtihani kwa Tume ya Uchunguzi wa Kijinai

Dar es Salaam. Wadau wa kada mbalimbali nchini, wametaja mtihani unaoikabili Tume ya Uchunguzi wa Kijinai wa Matukio ya Ghasia Wakati na Baada ya Uchaguzi wa 2025, kuwa ni kufanikiwa kuliponya Taifa.

Tume hiyo iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Jumatatu ya Mei 18, 2026 na kutangazwa kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Ikulu, inaongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shaaban Lila, akisaidiwa na makamishna Gadi Mjemamas, Awadh Bawazir na Aishieli Sumari, wote majaji wastaafu wa Mahakama Kuu.

Kuundwa kwake, kumetokana na mapendekezo yaliyotolewa na mapendekezo ya Tumeya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya UchaguziMkuu wa Oktoba 2025, iliyoshauri kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi wa Kijinai, kuchunguza na kuwataja waliohusika na matukio hayo ili hatua za uwajibikaji ziweze kuchukuliwa.

Ripoti ya tume hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chade Othman ilikabidhiwa kwa Rais Samia Aprili 23, 2026 ikionesha watu 518 walifariki dunia kwenye vurugu hizo, majeruhi na uharibifu wa mali.

Akizungumza jana Jumanne, Mei 19, 2026 Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie amesema tume hiyo inakabiliwa na mtihani wa kujisafisha, kujijengea imani ya jamii inayoifanyia kazi ili iaminike na matokeo ya kazi yake yalitoe Taifa kwenye mkwamo uliopo.

Amesema kabla na baada ya uchaguzi Taifa limegawanyika na hali hiyo inaendelea kwa sababu, hayo makundi bado hayajakubaliana.

 “Tume hii, mtihani wa kwanza inayokwenda kukutana nao ni kupokewa kwake, bado itakuwa ni tume inayopingwa na kukosolewa na makundi mbalimbali, hivyo ufanisi wa kazi yake na matokeo yake hautaweza kuleta majawabu ambayo jamii itayaunga mkono,” amesema.

Kinachosababisha kazi ya tume hiyo kuwa ngumu na ripoti zake kushindwa kuliponya Taifa, amesema ni kushughulikia matatizo ambayo bado yanahitaji hatua za awali za kukubaliana kwa pande zenye msuguano.

“Kuna mambo bado yanahitaji mjadala wa kukubaliana baina ya makundi mbalimbali yanayotofautiana, hivyo kuna vitu vinavyopaswa kufanyika kabla ya kuundwa kwa tume hii (ya jinai) ili kuliunganisha Taifa. Hii ni kwa sababu pande zinazotofautiana bado zina misimamo mikali kwa pande zote, hivyo hii tume itakwenda kuligawa zaidi Taifa,” amesema.

Hofu ya uwajibikaji na kivuli cha tume ya Jaji  Chande

Mdau wa Haki za Binadamu, Dk Ananilea Nkya amesema mtihani mgumu unaoikabili tume hiyo ni kuwataja watuhumiwa ambao pengine watakuwa watendaji ndani ya Serikali.

Dk Nkya amesema hofu ya jamii ni kwamba, haitaweza kufanya hivyo; na kutokana na hilo anaona watu wengi wataipuuza.

“Tume ya Chande haijasaidia kitu, hii nayo inaanza kazi watu wakiwa na msongo, wamechoka na kuumizwa. Ukiangalia yaliyotokea watuhumiwa wa mauaji wanaweza kuwa sehemu ya viongozi serikalini, jambo ambalo tume hii kwa muundo wake itakuwa vigumu kuliibua,” amesema.

Amesema mtazamo wa wadau unaonesha namna kivuli cha tume ya Jaji Chande kinavyochora matarajio ya jamii na kuipa mzigo tume mpya ya kijinai katika kufikia lengo la kuundwa kwake.

Kiongozi wa Kiroho, Askofu Amon Kinyunyu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Dodoma amesema tume hiyo ina jukumu la kusema ukweli kwa kuwataja wahusika halisi wa matukio hayo, akisisitiza wanapaswa kuanzia pale tume ya Jaji Chande ilipoishia.

“Tume ya Chande ilitusaidia kujua matatizo yaliyotokea, hii ya jinai sasa inapaswa kwenda kuwatambua na kuwataja watu waliohusika na mambo yaliyotajwa na tume ya Jaji Chande ambayo imetoa dodoso, hii sasa ina jukumu la kuiambia jamii waliohusika na kuchukua hatua za vitendo vya uwajibikaji ili kuliponya Taifa,” amesema Askofu Kinyunyu.

Kiu ya uchunguzi wa kimataifa

Naibu Katibu wa Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa ACT- Wazalendo, Shangwe Ayo amesema chama hicho bado kinaamini suluhisho sahihi ni uchunguzi huru wa kimataifa.

“Bado tunaona hali ni ile ile kama zamani. Kama ambavyo hatukuunga mkono tume ya Chande, hatuoni namna tume hii mpya itakavyotusaidia kupata jambo lenye maana.

“Msimamo wetu haujabadilika. Tunaamini ni uchunguzi huru wa kimataifa pekee utakaosaidia kubaini ukweli kuhusu kilichotokea Oktoba 29,” amesema Ayo.

Pia, amesema mchakato wa kimataifa ungesaidia kujenga imani ya umma kwa matokeo yatakayopatikana ili kila mtu aweze kuwa na utulivu na kuridhika na majibu yatakayokuja.

Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Bara, Joseph Selasini ameonya kuwa kutoungwa mkono kwa tume hiyo kunaweza kuongeza mpasuko wa kisiasa.

“Wanajaribu kukwepa uwajibikaji. Tangu tume ya Chande ilipotoa ripoti yake, haikupokewa vizuri na sehemu ya jamii. Walipaswa kutambua hilo. Kipaumbele cha Taifa kinapaswa kurejesha umoja na mshikamano wa kitaifa,” amesema Selasini.

Amesema wakati mwingine tume zinaweza kuwagawa watu zaidi badala ya kuwaunganisha, akifafanua uundwaji wa chombo hicho kutokana na mapendekezo ya tume iliyokataliwa, kunazalisha makundi.

Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa amesema Taifa bado halijafikia mwafaka kuhusu njia bora ya kusonga mbele.

“Kusema ukweli, hadi sasa bado nina mkanganyiko. Taifa bado hatujaelewa kikamilifu tunataka nini na tunapaswa kufanya nini ili kufikia (mwafaka). Inaonekana bado hatujatambua kikamilifu uzito wa yaliyotokea na umuhimu wa kujutia kwa dhati yaliyotokea,” amesema Olengurumwa.

Amesema wananchi wanastahili kupata taarifa kamili zaidi za matokeo ya tume ya Jaji Chande badala ya muhtasari uliotolewa pekee.

Olengurumwa  amesema Taifa linahitaji mchakato mpana na wa wazi zaidi, unaojengwa katika ushirikishwaji wa wananchi, kutafuta ukweli, maridhiano na mageuzi ya taasisi.

“Tunapaswa kufanya jambo ambalo tuna uhakika, litatusaidia kusonga mbele. Tulihitaji hatua nne katika mchakato huu, ambazo ni uwazi na ushirikishwaji mpana wa wananchi katika kuamua nini kifanyike, kutafuta ukweli na uwajibikaji, maridhiano na kushughulikia chanzo cha mgogoro, kwa sababu kushughulikia visababishi hivyo ndiko kutakakomaliza kila kitu,” amesema Olengurumwa.

Jamii isubiri majawabu

Mwanahabari mkongwe na Mchambuzi wa Siasa, Ezekiel Kamwaga amesema tume hiyo ni hatua muhimu katika kufikiwa mwafaka wa kitaifa, kwa kuwa itawabaini wahusika, akiitaka jamii kuipa nafasi ifanye kazi yake na kuipa jamii majawabu.

“Msimamo wangu tangu mwanzo, naunga mkono kuundwa tume hizi, hii ndiyo njia ya kumaliza matatizo kama haya duniani. Tume ya Jaji Lila ni mwendelezo wa Jaji Chande ambaye alisema hii tume ndiyo itatupa majibu ya watuhumiwa na hatua za uwajibikaji wa kisheria.

“Maana yake, tume hii ina kazi ya kuja na majibu hayo, ningependa watu waiache ifanye kazi, ijiridhishe iseme nani wanapaswa kuwajibika kwa namna gani, kwa mujibu wa sheria kutokana na tuhuma zinazowakabili,” amesema Kamwaga.

Mchambuzi wa Siasa wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza), Profesa Ali Makame amesema tume hiyo ina jukumu la kuhakikisha mchakato huo unapata imani ya umma na kutimiza matarajio ya wananchi kuhusu uwajibikaji.

“Tume ina jukumu kubwa la kuhakikisha inapata imani ya wananchi na kufanikisha lengo la kuwawajibisha wale wanaohusika, kama wananchi wengi wanavyotarajia. Ikiwa mchakato huu utaendeshwa kwa usahihi na haki, utasaidia Taifa kurejea kwenye umoja na utulivu wa muda mrefu,” amesema Profesa Makame.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *