Wachambuzi waona mwanga siasa za ushindaniWachambuzi waona mwanga siasa za ushindani

Dar es Salaam. Hatua ya vyama vya upinzani na chama tawala kuendelea na shughuli za kisiasa kwa wakati mmoja katika maeneo tofauti, imeelezwa na wachambuzi wa siasa kuwa inarejesha matumaini ya kurejea kwa siasa za ushindani wa hoja huku wakitahadharisha isitiwe doa.

Kauli hizo za wachambuzi zinakuja baada ya Mei 16, 2026, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuanza ziara na mikutano katika Kanda ya Victoria, kisha Kanda za Serengeti, Kanda ya Kaskazini na kuhitimisha na Kanda ya Kati.

Ziara hiyo imefanyika mwezi mmoja baada ya Mahakama ya Rufaa kukiondolea chama hicho zuio la muda la kufanya shughuli za kisiasa, lililoiweka Chadema kando na majukwaa ya kisiasa kwa takriban miezi nane.

Uamuzi huo uliotolewa Aprili 15, 2026 ulihusu kesi iliyofunguliwa na aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Saidi Issa Mohamed na wenzake wawili.

Wakati Chadema ikiendelea na ziara zake hizo, Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi nacho kimefanya ziara katika Mkoa wa Mara Mei 14 hadi 16.

Aidha, chama hicho kupitia Makamu Mwenyekiti wake Bara, Stephen Wasira kimefanya ziara katika Mkoa wa Kigoma kati ya Mei 15 na 17 mwaka huu.

Kwa upande wa ACT-Wazalendo, chama hicho kiliendelea na shughuli zake jijini Dar es Salaam ambapo Mei 16, 2026 kilifanya kongamano la kujadili mwelekeo na hatma ya nchi.

Nacho Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), sehemu ya viongozi wake ipo mkoani Iringa ikiendelea na kampeni za ubunge wa Isimani kuelekea uchaguzi mdogo wa ubunge unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Kote huko hazijasikika rabsha zozote za vyombo vya dola kuingilia mikutano au shughuli za mapokezi ya viongozi zinazoambatana na maana na kusababisha vurugu.

Licha ya hali hiyo, Chadema imeandikiwa barua na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikitakiwa kujieleza kwa nini isichukuliwe hatua za kusimamishiwa usajili kwa tuhuma za uvunjaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, suala ambalo wachambuzi wanasema lina dalili za kuitia doa hali iliyopo.

Kwa mujibu wa barua ya Msajili ya Mei 13, 2026, tuhuma hizo zinatokana na matamshi yanayodaiwa kuchochea na kuhamasisha vurugu pamoja na matumizi ya lugha za matusi.

Ishara nzuri

Mchambuzi wa siasa, Dk Baraka Mfinanga amesema hatua hiyo inaonyesha taswira nzuri kwa mazingira ya kisiasa nchini na vema ikaachwa iendelee ili kusiingie doa.

Ameeleza kwa kipindi fulani Tanzania ilishuhudia mvutano kuhusu haki ya vyama kufanya mikutano, jambo lililosababisha wananchi wengi kupoteza imani na usawa wa kisiasa.

Amesisitiza hatua ya CCM kuendelea kufanya ziara zake huku Chadema nayo ikifanya mikutano bila kuzuiwa waziwazi katika maeneo mengi, ni ujumbe kwamba kelele za umma kuhusu demokrasia zimeanza kuleta matokeo.

Mchambuzi huyo, amesema hakuna chama kinachoweza kujijengea uhalali wa kudumu ikiwa ushindani wa kisiasa hautakuwa wa wazi.

“Demokrasia inapimwa zaidi wakati wapinzani wanapopewa nafasi ya kuzungumza kuliko wakati chama tawala kinapokuwa na nguvu. Kama wananchi wanaweza kusikiliza pande zote bila hofu, ndipo taifa linaonekana lina imani na mfumo wake wa kisiasa,” amesema.

Amesema funzo kubwa linalopatikana katika hatua hiyo ni kwamba kuzuia mikutano ya kisiasa mara nyingi huongeza nguvu ya kisiasa ya chama kinachozuiwa badala ya kukidhoofisha.

Amefafanua katika historia ya siasa za Afrika, vyama vingi vya upinzani vilipata huruma ya wananchi baada ya kuonekana vinakandamizwa na dola.

Mchambuzi mwingine wa siasa, Dk Elias Mwakalinga, amesema mikutano ya sasa ya vyama vya siasa inaonyesha Tanzania inaanza kuingia katika kipindi ambacho vyama vitapimwa kwa sera na uwezo wa kushawishi wananchi badala ya uwezo wa kupata ulinzi wa dola.

Amesema hilo ni kama hatua muhimu ya kuijenga upya taswira ya ushindani wa kisiasa nchini, hivyo Serikali na mamlaka zake inapaswa kulilea.

Mchambuzi huyo, amesema kwa siku za karibuni kulikuwa na hali ya taharuki, kila mkutano wa upinzani ulionekana kama tishio la kiusalama.

Ameeleza kinachoendelea kinaonyesha kwamba siasa zinaweza kufanyika bila vurugu ikiwa taasisi za dola zitabaki katika nafasi ya usimamizi wa sheria badala ya kushiriki katika mvutano wa kisiasa.

“Kuna somo moja muhimu hapa, kwamba utulivu wa kisiasa haujengwi kwa kufunga midomo ya wapinzani bali kwa kuwapa nafasi ya kuzungumza na wananchi wakaamua wenyewe. Mara nyingi kuzuiwa kwa mikutano huzaa hisia za kunyimwa haki kuliko kulinda amani,” amesema.

Ameeleza kuendelea kwa ziara za CCM sambamba na mikutano ya Chadema kunaleta taswira mpya kwa vijana walioanza kuamini kuwa siasa za ushindani nchini zimepungua.

Dk Mwakalinga anaona kizazi kipya kinahitaji kuona ushindani wa wazi ili kijenge imani na mfumo wa uchaguzi na demokrasia.

Kwa upande wake Said Majjid, mchambuzi mwingine wa siasa, amesema hatua ya vyama vikubwa kufanya mikutano kwa wakati mmoja ni ishara kwamba ushindani wa kisiasa unaanza kurejea, badala ya kubaki kwenye malumbano ya kisheria na kiusalama.

Ameeleza kwa muda mrefu mijadala mingi ya kisiasa ilijikita kwenye haki ya kufanya siasa badala ya maudhui ya sera.

Amesema Chadema kurudi mitaani baada ya kupitia vipindi vya misukosuko kunatoa fundisho kwamba vyama vya upinzani haviwezi kutoweka kwa kuzuiwa kufanya mikutano, kwa sababu mara nyingi mizizi ya chama cha siasa hujengwa zaidi na malalamiko ya wananchi kuliko ratiba za ziara pekee.

Majjid, amesema mazingira ya sasa yanapaswa kuwa mwanzo wa kujifunza kwa taasisi zote, hasa vyombo vya dola, kwamba kazi yao ni kusimamia usalama wa mikutano na si kuonekana vinaamua nani azungumze na nani asizungumze.

“Ukiona chama tawala na upinzani vinazunguka nchini kwa wakati mmoja bila mivutano, hiyo ni ishara ya ukomavu. Lakini ukianza tena kuona upande mmoja unazuiwa, wananchi wataanza kuhoji usawa wa mfumo mzima italeta picha mbaya,” amesema.

Amekwenda mbali zaidi na kueleza hata barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa Chadema ikiituhumu kwa uvunjaji wa sheria, zinapaswa kukoma kwani zinatia doa.

Mwanafunzi wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Zuhura Mwangonde, amesema iwapo hali ya kuruhusu ushindani itaachwa bila kuingiliwa au kudhibitiwa, itaongeza mwamko wa wananchi kushiriki zaidi katika siasa hata chaguzi.

Katika mazingira ambayo upinzani ulikuwa ukikumbwa na vizuizi vya mara kwa mara, ameeleza sehemu ya wananchi ilianza kujenga mtazamo kwamba ushindani wa kisiasa nchini umepungua.

“Mfumo wa vyama vingi hauhitaji vyama viwe vinakubaliana kila kitu, unahitaji viwe na uhuru wa kutofautiana hadharani. Hapo ndipo wananchi wanapata nafasi ya kupima hoja na viongozi,” amesema.

Ameeleza funzo kwa dola na vyama vya siasa ni kwamba marufuku za kisiasa huwa na matokeo ya muda mfupi, lakini madhara yake kwa taswira ya demokrasia yanaweza kudumu kwa muda mrefu.

“Taifa lenye nguvu kisiasa ni lile ambalo hata wapinzani wake wanahisi wana nafasi ya kusikilizwa na wananchi bila hofu,” amesema Zuhura.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *