SMZ yaeleza athari za msimamo mkali, wananchi watakiwa kubadilikaSMZ yaeleza athari za msimamo mkali, wananchi watakiwa kubadilika

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeeleza athari za msimamo mkali ikiwa ni pamoja na kuvurugika kwa usalama wa amani ya nchi, hivyo kuwataka wananchi kuwa makini na makundi yanayoweza kusababisha changamoto hiyo.

Athari nyingine ni kuzorota kwa huduma za kijamii, kuibuka makundi ya uhalifu na silaha, kugawanyika kwa jamii na wataalamu kuikimbia nchi huku ikiathiri moja kwa umoja uchumi wa Taifa na kuvuruga utalii.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Salhina Mwita Ameir ameeleza hayo jana Jumanne, Mei 19, 206 wakati akifunga mafunzo kwa makundi mbalimbali wakiwemo vijana, viongozi wa dini kuelimisha jamii kuhusu madhara ya misimamo mikali inavyoweza kuathiri amani na maendeleo.

Mafunzo hayo yametolewa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa kushirikiana na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Amani na Maendeleo (UNPDF), ambapo imeelezwa misimamo mikali ina athari kubwa kwa mtu mmoja mmoja na jamii hadi Taifa.

“Athari ni kubwa sana, amani ya nchi inavurugika, mipango ya maendeleo inasimama hii inatokana na kwamba wataalamu tunaokuwa tunawategemea wanakimbilia nchi zingine na kuzinufaisha ilihali  walisomeshwa kwa gharama kubwa,” amesema Mwita.

Amewataka wafuatilie viashiria vinavyoweza kusababisha misimamo mikali na kuvitatua mapema.

Naye Ofisa wa UNDP Ofisi ya Zanzibar, Elia John amesema wataendelea kuisaida Serikali kuboresha mambo hayo ili kuhakikisha kuna maendeleo endelevu.

“Tunaendeleza jitihada kubwa na kuleta utulivu kuhakikisha kwamba hali iliyopo inaendelea, kuimarisha hali ya amani idumu na hii itasaidia mipango ya baadaye kudumisha amani kwa maendeleo endelevu ya taifa,” amesema

Kwa upande wake Sheikh kutoka ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Thabit Nouman Jongo amesema wamejifunza namna misimamo mikali inavyoleta athari kwani wameoneshwa jinsi mtoto wa miaka sita alivyo na ujasiri wa kuchinja watu, hivyo watakuwa mabalozi kueleza katika misikiti na madrasa yao.

“Huko kwenye madrasa wanaochukua mawe wanatia kwenye kanzu ni vijana wadogo miaka 12 hadi 14, ndio wanafanya mambo wasiyoyajua na matokeo yake wengi wanapata misukosuko,” amesema Sheikh Jongo.

Amesema,  “wakati mwingine wazazi wakiambiwa watoto wao ndio kafanya hivi wanakataa, kwa hiyo tuna kazi kubwa kupeleka ujumbe huu kwa jamii na kubadilisha.”

Sheha wa Shehia ya Mboriborini, Mzee Haji Mussa amesema waliofundishwa yanahusu uzalendo, kijana kuipenda nchi yao hivyo wanakwenda kuhamasisha kwenye shehia zao.

Fauzia Musa kutoka Shehia ya Sogea amesema wanaomba mafunzo yaendelee ili jamii ielewe kupunguza msimamo mkali kwa vijana, wazee na watoto.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *