Ndugu wa wasichana waliotoweka Arusha, wamwangukia Rais Samia awasaidieNdugu wa wasichana waliotoweka Arusha, wamwangukia Rais Samia awasaidie

Arusha. Sakata la kutoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa wasichana wawili, Kareen Didas (23) na Nakivona Toroka, maarufu ‘Rahma’ (22), limechukua sura mpya, baada ya ndugu kuamua kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan, aingilie kati kuongeza nguvu katika upelelezi wa kuwatafuta.

Familia inakuja na ombi hilo, wakati ambao Jeshi la Polisi linamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za kupotea kwa wasichana hao, likisisitiza uchunguzi unaendelea kupata taarifa zaidi.

Wasichana hao wanadaiwa kutoweka Juni 20, 2025 mkoani Arusha baada ya kuhudhuria sherehe ya kupongezana kufuatia kumaliza mitihani ya mwaka wa kwanza wa chuo.

Akizungumza jijini Arusha, Baba wa Kareen, Didas Tarimo amesema familia hiyo imetoka Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, kufuatilia jalada la mtoto wao, lakini hadi sasa hawajaona maendeleo yoyote ya kuridhisha.

Amesema wanaamini Rais Samia akiingilia kati na kutoa tamko kwa wasaidizi wake wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu na vyombo vya ulinzi na usalama itasaidia kuharakisha uchunguzi.

“Kwa muda wote huu tumekuwa tukisota kutoka nyumbani Kahama hadi polisi Arusha kufuatilia suala hili, lakini bado hatuoni mwanga wa kumpata mtoto wetu, zaidi ni maelezo ya danadana tu,” amesema.

Amesema anachotamani kujua ni uhalisia wa kilichojificha nyuma ya pazia kuhusu suala hilo, kwani mkewe tangu alipopata taarifa amepooza na kulazwa kutokana na mshtuko.

Dada wa Kareen, Elizabeth Didas, amesema familia imekuwa ikiahidiwa kuwa uchunguzi unaendelea tangu walipofungua jalada mwaka jana, lakini hakuna matokeo yanayoonekana.

“Tunajiuliza huu ni uchunguzi wa aina gani ambao hauna majibu ya wazi, yaani kila siku tunaelezwa kuwa upelelezi unaendelea, lakini hakuna kinachoonekana,” amesema.

Amesema wanaamini askari wanaosimamia uchunguzi huo wanahitaji kuongezewa nguvu ili kusaidia kufanikisha kazi hiyo.

“Sisi tunaomba Serikali kuu iingilie kati sakata hili kwa sababu tunaona bado kuna uzito mdogo unaowekwa kwenye maisha ya ndugu yetu. Tuna imani Serikali inaweza kusaidia kuwapata watoto wetu,” amesema.

Kauli ya Polisi

Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, amesema bado kuna mtu mmoja anayeshikiliwa kwa ajili ya uchunguzi kuhusiana na kutoweka kwa wasichana hao.

“Bado tunamshikilia kijana Godwin Ndossi kwa ajili ya upelelezi wa tukio hili. Kikubwa ndugu wawe watulivu kwani kuna taarifa nyingi ambazo tunazifanyia kazi, na ukweli kuhusu walipo wasichana hao utabainika,” amesema.

Mama alipooza

Elizabeth, amesema tangu taarifa za kupotea kwa Kareen zilipowafikia, mama yao alianza kuugua mara kwa mara hadi baadaye kupooza kulikomlaza kitandani hadi sasa.

Mama huyo, Victoria Shao, anadaiwa kupata tatizo hilo Agosti mwaka jana, baada ya kuanguka ghafla akiwa nyumbani katika shughuli zake za ufugaji.

“Mama aliwahishwa hospitalini na madaktari walieleza kuwa alikuwa amezidiwa na mawazo hali iliyosababisha kiwango cha sukari kupanda,” amesema.

Amesema mama yao alikosa amani kwa kuwa hakujua alipo mwanaye, wala hali yake.

“Mama alisema angepata ahueni kama angejua mtoto wake yuko hai au amefariki kuliko kuendelea kuishi bila taarifa yoyote,” amesema.

Tukio lilivyokuwa

Awali, taarifa za kupotea kwa wasichana hao zilianza kusambaa mitandaoni Mei 2, 2026 huku mfanyabiashara, Godwin Ndossi, akitajwa kuwa aliwaalika kwenye sherehe ya usiku.

Wasichana hao, Kareen Didas (23) na Nakivona Toroka, maarufu  Rahma (22), wanadaiwa kuhudhuria sherehe hiyo Juni 20, 2025 katika eneo la Shangarai, wilayani Arumeru, na tangu siku hiyo hawakuonekana tena.

Tukio hilo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi Tengeru na kupewa jalada namba TEG/RB/342/2025.

Kareen, alikuwa akiishi Shangarai wilayani Arumeru, akijishughulisha na biashara ndogo ndogo huku akisoma uhasibu kupitia Open University kwa njia ya mtandao.

Kwa upande wa Nakivona, alikuwa mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha mwaka wa kwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *