Ghetto Kids kuandika historia Kombe la Dunia 2026Ghetto Kids kuandika historia Kombe la Dunia 2026

Uganda. Kundi la dansi kutoka Uganda, Ghetto Kids, linatarajia kuandika historia mpya baada ya kuthibitishwa kuwa litatumbuiza pamoja na nyota wa muziki, Shakira katika fainali ya Kombe la Dunia 2026. 

Kupitia ukurasa wao wa Ghetto Kids, kundi hilo limeweka video ya Shakira akitangaza rasmi kuwa tayari amewaalika kushiriki kwenye halftime show ya fainali hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa.

“Hatimaye! Malkia Shakira amethibitisha. Mungu ni Mkuu. Tutaonana kwenye 2026 FIFA World Cup! Hii ni kwa ajili ya Africa na Uganda!” Ujumbe ulioandikwa na Ghetto Kids. 

Katika video hiyo, Shakira amesema amekuwa akifuatilia video mbalimbali za mashabiki wanaocheza wimbo wake mpya wa Kombe la Dunia uitwao Dai Dai.

“Mnahitaji kujua kuwa nataka halftime show ya fainali iwe ya kipekee na isiyosahaulika kwa wote,” amesema Shakira.

Mwimbaji huyo kutoka Colombia, ameeleza kuwa tayari amewaalika Ghetto Kids kutoka Uganda kushiriki naye jukwaani, huku akiwahamasisha watu wengine kuendelea kutuma video zao za ubunifu wa kucheza wimbo huo.

“Tayari nimewaalika Ghetto Kids kutoka Uganda, lakini ningependa sana kuona creations na videos zenu zote, hivyo endeleeni kuzituma kwa sababu nitakuwa nazifuatilia kwa karibu sana,” amesema Shakira.

Hatua hiyo imepokelewa kwa furaha kubwa na mashabiki wengi wa Afrika Mashariki, huku wengi wakieleza kuwa ni mafanikio makubwa kwa kundi hilo ambalo limeendelea kuipeperusha bendera ya Uganda na Afrika kupitia vipaji vyao vya dansi katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa.

Kombe la Dunia la FIFA 2026 linatarajiwa kuwa la kihistoria kwa sababu kwa mara ya kwanza litashirikisha timu 48, kuchezwa katika nchi tatu ambazo ni Marekani, Canada na Mexico huku fainali yake itakuwa na halftime show (burudani wakati wa mapumziko) kama ilivyo kwenye Super Bowl.

Mashindano hayo yataanza Juni 11, 2026 na fainali itachezwa Julai 19, 2026 katika uwanja wa MetLife huko New Jersey, Marekani. Wasanii watakaotoa burudani katika fainali hiyo ni pamoja na Shakira, Madonna na kundi la muziki kutoka Korea BTS.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *