Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema inachukua hatua madhubuti kudhibiti ujenzi holela pembezoni mwa miji ili kuzuia ongezeko la gharama za kupeleka huduma za msingi na miundombinu katika maeneo yasiyopangwa.
Hayo yameelezwa leo, Alhamisi Mei 21, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe, katika Jukwaa la 13 la Miji Duniani (WUF13) linalofanyika jijini Cairo, Misri.
Amesema Serikali imeamua kuweka mkazo katika upangaji wa miji kabla ya ukuaji holela haujazalisha changamoto kubwa za kijamii na kiuchumi.
Profesa Shemdoe, amesema miji mikubwa ya Tanzania ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Arusha inaendelea kupanuka kwa kasi kuelekea maeneo ya pembezoni, hali inayohitaji mipango madhubuti ya matumizi ya ardhi na utoaji wa huduma muhimu.
Waziri huyo, ameeleza ukuaji wa miji usiozingatia mipango husababisha kuibuka kwa makazi yasiyo rasmi, kuongezeka kwa changamoto za ajira na ugumu wa kufikisha huduma muhimu kama maji safi, umeme, barabara na mifumo ya usafi wa mazingira.
“Ukuaji wa miji bila mipango ya mapema husababisha makazi yaliyotawanyika na kuongeza gharama za baadaye za kupeleka miundombinu. Ni rahisi na nafuu zaidi kupanga maeneo kabla hayajajengwa kuliko kurekebisha baada ya watu kuhamia,” amesema.
Katika hatua za kukabiliana na changamoto hiyo, amesema Serikali imezindua miongozo mipya ya upangaji wa miji, udhibiti wa uendelezaji wa makazi na uhifadhi wa maeneo ya kijani ili kuhakikisha ukuaji wa miji unakuwa endelevu na unaozingatia mazingira.
Aidha, amesema Serikali imeanza kutumia mifumo ya kidijitali pamoja na teknolojia ya taarifa za kijiografia (GIS) katika kurasimisha makazi ya pembezoni mwa miji na kupanga matumizi bora ya ardhi kupitia ugawaji wa viwanja vilivyopimwa.
Profesa Shemdoe ametaja utekelezaji wa Programu ya Tanzania ya Kupandisha Kiwango cha Miundombinu na Ushindani wa Miji (TACTIC) inayotekelezwa katika miji 45 nchini, akisema programu hiyo inalenga kuboresha barabara, masoko, mifereji ya maji ya mvua pamoja na udhibiti wa mafuriko.
Pia, amesema Mradi wa Maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) Awamu ya Kwanza na ya Pili umeendelea kusaidia ujenzi wa miundombinu inayohimili athari za mabadiliko ya tabianchi, hususan katika maeneo yanayokabiliwa na mafuriko ya mara kwa mara.
Amesema Serikali pia inawekeza katika kukuza uchumi wa miji ya kati na pembezoni kupitia ujenzi wa masoko ya kisasa 28, vituo vya usindikaji wa mazao ya kilimo pamoja na maendeleo ya Ukanda wa Kiuchumi wa Kwala.
Hatua hizo, amesema zinalenga kusogeza huduma na fursa za ajira karibu na wananchi ili kupunguza msongamano wa shughuli za kiuchumi katika Dar es Salaam na kuzuia kuendelea kwa ukuaji holela wa makazi.
“Tunataka kujenga miji jumuishi, salama na yenye uwezo wa kuhimili changamoto za tabianchi huku tukihakikisha ukuaji wa miji unachochea maendeleo ya wananchi badala ya kuzalisha migogoro ya huduma na miundombinu,” amesema.
Ameongeza kuwa ujenzi wa masoko makubwa zaidi ya 15 pamoja na uboreshaji wa sekta isiyo rasmi, hususan kwa vijana na wafanyabiashara wadogo, ni sehemu ya mkakati mpana wa taifa wa kuimarisha uchumi wa miji na kupunguza changamoto ya ajira.
Kupitia mkakati huo, Tanzania inalenga kuijenga mifumo ya miji inayopangwa mapema, yenye huduma bora na inayoweza kukidhi mahitaji ya ongezeko la watu bila kuibebesha serikali gharama kubwa za kurekebisha athari za ujenzi holela katika siku zijazo.
