Washtakiwa watano kortini wakidaiwa kuiba Dola 58,000 kwenye akaunti ya marehemuWashtakiwa watano kortini wakidaiwa kuiba Dola 58,000 kwenye akaunti ya marehemu

Dar es Salaam. Watu watano, wakiwamo wafanyakazi wawili wa Benki ya CRDB, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka manne, yakiwamo kughushi nyaraka na kuiba Dola 58,000 za Marekani (Sh140 milioni) kutoka katika akaunti ya marehemu.

Washtakiwa hao ni Jacqueline Mwibule (41), mfanyakazi wa benki na mkazi wa Tabata (Dar es Salaam), Eliya Mwendi (44), mfanyabiashara na mkazi wa Kibaha (Pwani) na Joachim Kimaro (44), mfanyakazi wa benki na mkazi wa Bunju (Dar es Salaam).

Wengine ni Festo Mwendi (46) na Leonard Lugumisa (46), wote ni wafanyabiashara na wakazi wa Kimara (Dar es Salaam).

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani leo, Mei 22, 2026 na kusomewa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi namba 11177 ya mwaka 2026.

Kabla ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Mkazi Mkuu Bilal Ahmed aliwaeleza washtakiwa hao kuwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka nchini.

Pia, shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa wote, halina dhamana, hivyo wataendelea kusalia rumande hadi upelelezi utakapokamilika

Hakimu Ahmed baada ya kutoa maelezo hayo, upande wa Jamhuri uliwasomea mashtaka yao.

Washtakiwa wanadaiwa kuiba dola za kimarekani 58,000 sawa na zaidi ya Sh140 milioni, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pendo Temu akishirikiana na Fatma Waziri, amedai shtaka la kwanza ni kuongoza genge la uhalifu, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Oktoba 16 na Oktoba 17, 2025 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kwa makusudi walitenda kosa la uhalifu na kutakatisha fedha.

Shtaka la pili ni wizi, kati ya Oktoba 16 na Oktoba 17, 2025 katika Benki ya CRDB tawi la Magomeni Wilaya ya Kinondoni (Dar es Salaam), washtakiwa kwa pamoja waliiba Dola 58,000 za Marekani (Sh148 milioni).

Wanadaiwa kuiba fedha hizo katika akaunti ya namba 0252293130300 inayomilikiwa na marehemu Christine Mulokozi iliyopo katika benki hiyo.

Shtaka la tatu ni madai ya kughushi, katika tarehe hizo na eneo hilo, washtakiwa kwa njia ya udanganyifu walitengeneza risiti ya benki kuonesha Mulokozi ameidhinisha na kutoa fedha za Dola za Marekani 58,000 kutoka akaunti yake iliyopo katika benki hiyo, wakati wakijua ni uongo.

Shtaka la nne ni kutakatisha fedha, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa walijipatia Dola 58,000 za Marekani ( Sh148 milioni) wakati wakijua fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la wizi.

Baada ya kusomewa mashtaka yao, upande wa mashtaka ulidai upelelezi bado haujakamilika na waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Ahmed aliahirisha kesi hadi Juni 4, 2026 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamepelekwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *