Baba Levo, Abdul Nondo watunishiana misuliBaba Levo, Abdul Nondo watunishiana misuli

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo, Abdul Nondo amempa siku saba Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando maarufu ‘Baba Levo’, kumwomba radhi la sivyo atamfungulia kesi ya kumdai Sh500 milioni kwa kumchafua na kumdhalilisha.

Kauli hiyo imemwibua Baba Levo akisema kauli zinazotajwa hakuzitoa hewani, hivyo yuko tayari wakutane mahakamani akiwa na mwanasheria wake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Mei 23, 2026 , Nondo amesema amefikia hatua hiyo baada ya mbunge huyo kwa nyakati tofauti kutamka na kusambaza uongo dhidi yake,  kuwa alijitekaa wakati mahakama ilishamsafisha dhdi ya tuhuma hizo.

Hata hivyo, madai hayo yamepingwa na Baba Levo akidai alichokisema yeye ni kunukuu taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi kuhusiana na taarifa za yeye (Nondo) kutekwa.

“Hizi taarifa za yeye kujiteka sijazitoa hewani, ni Jeshi la Polisi ndilo lilisema, sasa yeye nilitegemea akalishitaki jeshi hilo, ananigeukia mimi, ‘any way’ muache tukutane mahakamani nikiwa na mwanasheria wangu,” amesema Baba Levo.

Pamoja na kujibu hivyo, pia mbunge huyo amesema hadi sasa hajapata barua rasmi kutoka kwa mwanasheria wa Nondo dhidi ya madai hayo.

Kwa nyakati tofauti, Abdul Nondo amewahi kudai kukumbwa na matukio ya kutekwa, ikiwemo la Machi 7, 2018, alipotelekezwa maeneo ya kiwanda cha Pareto, Mafinga mkoani Iringa.

Wakati huo alikuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mwenyekiti wa Taasisi ya Utetezi wa Wanafunzi Tanzania (TSNP).

Tukio jingine linalodaiwa kumkumba Abdul Nondo ni la Desemba 1, 2024 lililomkuta katika Stendi ya Mabasi ya Magufuli, Mbezi Louis jijini Dar es Salaam, ambapo alidai kutekwa na watu zaidi ya wanne waliomtesa na kumuumiza kabla ya kumtelekeza katika ufukwe wa Coco, jijini Dar es Salaam.

Katika tukio hilo, alisaidiwa na waendesha bodaboda kufikishwa Makao Makuu ya ACT Wazalendo, Magomeni, kabla ya kupelekwa Hospitali ya Aga Khan kwa matibabu, ambako alilazwa kwa zaidi ya wiki moja.

Akizungumzia madai yake, Nondo amedai Baba Levo amekuwa akitoa kauli na kusambaza madai kuwa alijiteka, kauli alizosema ni za uongo, zinamchafua na kumdhalilisha mbele ya jamii na Watanzania kwa ujumla.

Nondo amesema amedhamiria kufungua kesi ya kashfa na udhalilishaji dhidi ya Baba Levo, na tayari amemwagiza wakili wake kuanza mchakato huo mara moja.

Ameeleza kuwa hatua hizo zilianza Mei 20, 2026 baada ya kumtumia Baba Levo barua ya madai ikieleza kusudio la kufungua kesi dhidi yake.

Kwa mujibu wa Nondo, mojawapo ya masharti yaliyowekwa katika barua hiyo ni kumtaka mbunge huyo, kuomba radhi hadharani.

Pia, amesema Baba Levo anatakiwa kuahidi umma wa Watanzania kuwa hataendelea kusambaza taarifa za uongo, bali atazingatia ukweli, uaminifu na uhakika katika taarifa anazochapisha mitandaoni na kwenye vyombo vya habari.

“Aidha kutokana na maumivu makubwa aliyonisababishia, pamoja na kuchafua heshima na utu wangu katika jamii kupitia maneno ya uongo, kashfa na udhalilishaji dhidi yangu, nimemwagiza wakili wangu amelekeze Baba Levo kulipa Sh500 milioni kama fidia ya madhara yaliyotokana na tabia yake hiyo,” amesema Nondo.

Ameongeza kuwa iwapo Baba Levo hatatekeleza masharti hayo ndani ya siku saba kuanzia Mei 22, 2026 hadi Mei 30, 2026, atafungua rasmi kesi mahakamani, wakimtaka awasilishe ushahidi na mashahidi wa kuthibitisha madai yake kuwa Nondo alijiteka mara mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *