Yanayowakuta watumiaji wa viagra kuongeza nguvu za kiumeYanayowakuta watumiaji wa viagra kuongeza nguvu za kiume

Dar es Salaam. Matumizi ya dawa za kuongeza nguvu za kiume maarufu Viagra na Vega 100, yameendelea kuenea kwa siri miongoni mwa vijana nchini, huku baadhi yao wakikumbwa na madhara ya kiafya na kisaikolojia.

Baadhi ya vijana wanaotumia dawa hizo, wanasema wanalazimika kuzitumia kwa tamaa ya kutaka kuthibitisha uwezo wao wa kimapenzi, kutafuta sifa mbele ya wenza wao au kulipiza kisasi katika mahusiano, bila kutambua madhara tarajiwa.

Mmoja wa vijana hao mkazi wa Temeke (Dar es Salaam), aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, amesema aliwahi kutumia dawa hiyo kwa lengo la kumkomoa mwanamke aliyekuwa akimsumbua kimapenzi kwa muda mrefu.

Kijana huyo, anasema mwanamke huyo alimzungusha muda mrefu huku akimuomba fedha mara kwa mara kabla ya kukutana naye, hivyo alipopata nafasi alitumia dawa hizo kufidia mateso aliyopitia.

“Nilichoka nikamuacha lakini baadaye nikasikia anatoka na mtu mwingine, ndipo nilipoamua kurudi kwa nguvu zaidi. Nikajiandaa kabisa, nikawa na pesa sehemu za starehe na dawa zangu,” amesema.

Baada ya kutumia dawa hizo, amesema alijihisi kuwa na nguvu kupita kiasi na alifanya tendo kwa muda mrefu kuliko uhalisia wake.

“Sitakuja kusahau siku hiyo. Tendo lilidumu kwa muda mrefu sana hadi yule mwanamke akazimia. Nilihisi hofu kubwa nikajua labda nimemuua, nikaanza kuomba msaada kwa watu waliokuwa karibu,” amesema.

Kwa Shela Omary, anayeishi Wailes wilayani Temeke, hali ilikuwa tofauti. Yeye alikuwa na mwanaume mwenye umri mkubwa na hakujua kuwa ili ashiriki naye tendo alitumia dawa hizo kwanza kuongeza nguvu za kiume.

Kuna siku, amesema wakiwa katikati ya tendo, mwanaume alikakamaa, akapoteza nguvu za mwili na kuanza kutoa sauti nzito zilizomtisha.

“Mimi nilishtuka sana. Nilidhani labda amepandisha majini au kuna jambo la ajabu limemtokea. Nilihofu sana hadi nikakimbia eneo lile,” amesema.

Baadaye alikuja kubaini kuwa mwanaume huyo alikuwa amepata dalili zinazofanana na kupooza baada ya kutumia dawa hizo.

Abdallah Sima, amesema aliwahi kutumia dawa hizo baada ya kushawishiwa na maelezo aliyokuwa akiyasoma kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwezo wa kuongeza nguvu za kiume.

Amesema baada ya kuzitumia alianza kupata ganzi kwenye sehemu zake za siri pamoja na kusimama kwa uume mara kwa mara kwa muda wa karibu wiki nzima.

“Nilikuwa sipati raha tena kwenye tendo. Nilihisi ganzi na hali ilikuwa inanitesa sana. Nilijutia kutumia dawa hizo,” amesema.

TMDA yaonya

Kutokana na kuongezeka kwa matumizi na madhara ya dawa hizo, Mei 20, 2026, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania ilitoa tahadhari dhidi ya matumizi ya dawa ya Vega 100 inayodaiwa kuuzwa kiholela katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua hiyo inalenga kulinda afya ya wananchi dhidi ya matumizi ya dawa ambazo ubora, usalama na ufanisi wake haujathibitishwa.

TMDA iliwahi pia kutoa tahadhari kuhusu dawa hiyo Septemba 11, 2023 wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi ilipoitembelea.

Zatafutwa kwa wingi

Licha ya kupigwa marufuku au kuwa hazijasajiliwa, muuza duka la dawa jijini Dodoma, Leila Jongo amesema dawa ya Vega 100 bado inatafutwa kwa wingi kutokana na bei yake kuwa nafuu na uwezo wake wa kufanya kazi haraka.

Amesema zipo dawa nyingine zilizosajiliwa kwa matumizi hayo ambazo huuzwa kati ya Sh2,000 hadi Sh7,000 kutegemea aina ya dawa na kiwango chake.

“Tunashauri watu wapime afya zao kwanza kabla ya kutumia dawa hizi kwa sababu zinaweza kusababisha madhara kwa watu wenye shinikizo la damu, kisukari au matatizo mengine ya kiafya,” amesema.

Amesema pamoja na TMDA kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, baadhi ya watu bado wanaendelea kuziuza kwa siri kutokana na mahitaji makubwa yaliyopo mitaani.

Leila amesema wauzaji wanaokutwa na dawa ambazo hazijasajiliwa wanaweza kutozwa faini inayofikia asilimia 30 ya thamani ya mzigo unaokamatwa, lakini hatua hiyo bado haijamaliza biashara hiyo.

Mtazamo wa kisaikolojia

Mtaalamu wa saikolojia, Dk Jabir Mussa amesema ongezeko la matumizi ya dawa hizo linaonyesha namna vijana wengi wanavyokuwa na hofu kuhusu uwezo wao wa kingono.

“Wengi wanaamini nguvu za kiume ndiyo kipimo cha uanaume wao. Hali hiyo inawasukuma kufanya maamuzi ya hatari bila kufikiria madhara yake,” amesema.

Amesema mitandao ya kijamii, simulizi za marafiki pamoja na maudhui yanayosambazwa mtandaoni yamechangia kuwajengea vijana matarajio yasiyo halisi kuhusu mahusiano ya kimapenzi.

Dk Mussa, amesema baadhi ya vijana wanaotumia dawa hizo mara kwa mara hujikuta wakipoteza kujiamini wanapokutana na wenza bila dawa, hali inayoweza kusababisha utegemezi wa kisaikolojia na kuathiri afya ya akili pamoja na mahusiano yao ya kawaida.

Ametoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuzungumza kwa uwazi na vijana kuhusu afya ya uzazi na madhara ya matumizi holela ya dawa, badala ya kuwaacha wapate taarifa kupitia vijiweni au kwa marafiki wasiokuwa na uelewa wa kitaalamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *