Dar es Salaam. Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia program mpya ya kurahisisha mawasiliano inayojulikana kama Max imezinduliwa.
Programu hio yenye uwezo wa kufanya kazi vizuri hata kwenye maeneo yenye mtandao dhaifu. Teknolojia yake inayojulikana kama NoLACE, kwa mujibu wa watengenezaji, huboresha ubora wa mawasiliano kwa kupunguza kelele za usuli, kudumisha uwazi wa sauti, na kurejesha mawasiliano hata pale mtandao unapokatika kwa muda.
Programu hii mpya ya ujumbe wa Kirusi (MAX) imezinduliwa Nchini Tanzania, ambapo Wananchi wanatarajiwa kupata fursa ya kujisajili kwenye mfumo huo ikiwa ni Programu ya Mawasiliano ya Ujumbe iliyotengenezwa nchini Urusi.
Akizungumza katika uzinduzi huo ambao umefanyika Jijini Dar es salaam, Mkuu wa kampuni ya Kapi7 Tours & Safaris Limited, Kapilima Hassan amesema
“MAX ni suluhisho bora kwa mawasiliano ya moja kwa moja ndani na nje ya Urusi, si kwa watu binafsi pekee bali pia kwa wafanyabiashara wanaokumbana na changamoto za mtandao dhaifu. Ubora wa sauti na video ni wa kuaminika na wazi.”
Aidha, MAX ina msaidizi wa akili bandiaaliyejengewa ndani anayeitwa GigaChat, ambaye anaweza kutafsiri ujumbe, kunakili maudhui kutoka kwenye sauti kwenda maandishi, na kusaidia kutengeneza maudhui mbalimbali, hivyo kurahisisha mawasiliano kati ya watumiaji wasiojua lugha ya Kirusi.
Programu hii pia imeboreshwa ili kufanya kazi vizuri kwenye simu za bei nafuu, jambo linaloifanya iwe rafiki kwa watumiaji wengi zaidi hasa katika nchi zinazoendelea.
MAX inapatikana kwa watumiaji kutoka maeneo mbalimbali duniani ikiwemo Asia, Afrika, Mashariki ya Kati na Amerika Kusini, ambapo wanaweza kuwasiliana kwa urahisi kupitia ujumbe na simu.
