Tanga. Asilimia 70 ya wagonjwa wanaohitaji huduma za matibabu ya moyo kutoka Kanda ya Kaskazini wanashindwa kufika katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kutokana na changamoto za gharama za usafiri na malazi, hali inayochangia wagonjwa wengi kushindwa kupata matibabu kwa wakati.
Kutokana na changamoto hiyo, Hospitali ya Rufaa ya KCMC imeanza ujenzi wa Taasisi ya Moyo kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa Kanda ya Kaskazini, ambapo taasisi hiyo inatarajiwa kusaidia kati ya asilimia 40 hadi 60 ya wagonjwa ambao kwa sasa hulazimika kwenda JKCI jijini Dar es Salaam kupata huduma hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian, amesema ujio wa taasisi hiyo ni hatua kubwa katika kuboresha huduma za afya na kupunguza adha kwa wananchi wa mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
“Leo tunatoa taarifa kwa wananchi wa Tanga na wadau mbalimbali kwamba KCMC wamekuja na mradi mkubwa wa ujenzi wa Taasisi ya Moyo ambayo itakuwa na uwezo mkubwa kama ilivyo JKCI na itasaidia sana wananchi wa Kanda ya Kaskazini kupata huduma karibu yao,” amesema Batilda.
Batilda amesema Serikali ya mkoa kwa kushirikiana na KCMC imeandaa hafla ya chakula cha jioni itakayofanyika Mei 30 mwaka huu katika Hoteli ya Tanga Beach, ikiwa ni sehemu ya harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya vifaa vya taasisi hiyo.
“Tunawakaribisha wafanyabiashara, wananchi na wadau wote wa maendeleo kuungana nasi katika kuchangia jitihada hizi zinazolenga kuimarisha sekta ya afya na kuunga mkono maono ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma za afya nchini,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt Batilda Burian akizungumza na waandishi wa habari juu ya chakula cha jioni na harambee kwa wadau wa mkoa wa Tanga kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa taasisi ya moyo Kanda ya kaskazini katika hospitali KCMC Mkoa wa Kilimanjaro .Picha na Mbonea Herman.
Amesema kwa mujibu wa takwimu zilizopo, kati ya asilimia 40 hadi 60 ya wagonjwa wanaopata huduma katika Taasisi ya Moyo ya JKCI wanatoka Kanda ya Kaskazini, jambo linaloonesha umuhimu wa kuwepo kwa taasisi hiyo katika eneo la KCMC.
“Wananchi wetu watapunguza gharama kubwa za usafiri na malazi, lakini pia watapata huduma bora kwa karibu zaidi. Hii ni hatua muhimu katika kupeleka huduma za kibingwa karibu na wananchi,” amesema Batilda.
Aidha, amesema tayari Sh22 bilioni zimepatikana kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo kupitia wadau mbalimbali, huku kiasi cha Sh3 bilioni kikihitajika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.
Kwa upande wake, Meneja Miradi wa Kitengo cha Magonjwa ya Moyo KCMC, Emanuel Bianchi, amesema hadi sasa ujenzi wa Taasisi ya Moyo umefikia asilimia 40 na unatarajiwa kugharimu jumla ya Sh25 bilioni hadi kukamilika kwake.
“Tayari tumepata bilioni 22 kwa ajili ya ujenzi lakini bado tunahitaji bilioni tatu kwa ajili ya vifaa tiba. Kupitia harambee hii tunawashirikisha wananchi na wadau mbalimbali kuona kwamba taasisi hii ni mali yao,” amesema Bianchi.
Amesema kukamilika kwa taasisi hiyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto zinazowakabili wagonjwa wengi wa moyo ambao hushindwa kufuata matibabu katika Hospitali ya Moyo ya JKCI kutokana na gharama kubwa za usafiri na malazi.
“Huduma hii ikikamilika itakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Kanda ya Kaskazini na itaongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa nchini,” amesema.
Mradi huo unatajwa kuwa sehemu ya juhudi za Serikali na wadau wa afya kuhakikisha huduma bora za matibabu ya moyo zinapatikana karibu na wananchi, sambamba na kukuza utalii wa matibabu nchini.
