
Babati. Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba anatarajia kuzindua mbio za Manyara Tanzanite marathon ili kuchangia fedha za ujenzi wa jengo la mama na mtoto na huduma za watoto njiti kwenye Mkoa wa Manyara ili kuokoa maisha yao.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga akizungumza na Mwananchi Digital Mei 26, 2026 amesema Waziri Mkuu Mwigulu anatarajia kuzindua mbio hizo Agosti 22, 2026 zikiwa na kauli mbiu ya ‘Hatua moja okoa maisha ya mtoto’.
Sendiga amesema mbio hizo za riadha ya Manyara Tanzanite Marathon 2026 zitawezesha kupatikana kwa fedha hizo na kufanikisha uboreshaji wa huduma za watoto wachanga na njiti.
“Lengo ni kuboresha huduma za watoto wachanga na njiti ikiwemo kununua vifaa tiba, kujenga jengo la watoto wachanga na njiti katika hospitali ya wilaya Hanang, kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi na kuzuia magonjwa yasiyoambukiza na kuutangaza mkoa kwa utalii,” amesema.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akipambana na kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto, wao kama mkoa wanaunga mkono juhudi hizo muhimu katika jamii ili kuwasaidia akina mama wanaopata ujauzito isiwe sababu ya kifo pia watoto wachanga na njiti waishi.
Sendiga amesema Sh886 milioni zinatarajiwa kukusanywa katika mpango huo na zitaelekezwa katika vituo mbalimbali vya afya ili kuboresha utoaji wa huduma.
“Nawaomba wadau wote wa maendeleo, makampuni binafsi, wafanyabiashara, wanamichezo na watu binafsi, kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo za hisani,” amesema Sendiga.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Andrew Method amesema wastani wa watoto njiti 3,000 huzaliwa kwa mwaka kwenye eneo hilo.
Dk Method amesema kukamilika kwa majengo hayo kutakuwa nafuu kwa wanawake hao wajawazito, watoto wachanga njiti wataweza kuhudumiwa vyema
Mmoja kati ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani, Japhari Matimbwa amesema wana Manyara wanapaswa kuunga mkono hatua hiyo ili kupambana na changamoto hiyo ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto na watoto wachanga njiti.
“Hapa Mirerani kabla ya kupatikana kwa jengo la mama na mtoto, Dk Emmanuel Mushi alifanikisha kuandaa mashine ya kuhifadhi watoto njiti kupitia juhudi zake binafsi, hatua hiyo itakuwa nzuri,” amesema.
