Dar es Salaam. Mwonekano wa miguu ya msanii wa Singeli nchini, Dulla Makabila, umezua gumzo kwenye mitandao ya kijamii na kuibua hisia tofauti kwa baadhi ya mashabiki wake.
Hayo ni baada ya picha na video zake kusambaa zikimuonyesha akiwa kwenye maandalizi ya video ya wimbo wake mpya ‘Kidonda’. Dulla alionekana akiwa amevaa mavazi ya kimila ya Kimasai yaliyosababisha sehemu kubwa ya miguu yake kuonekana wazi huku ikiwa na makovu, na kupelekea baadhi ya watu kuhoji kama msanii huyo ana changamoto ya kiafya.
Akizungumza na Mwananchi, Dulla Makabila amesema hana tatizo lolote la kiafya na kwamba miguu yake ipo sawa kama ilivyo kwa binadamu wengine.
“Miguu yangu haina shida yoyote, ipo sawa tu. Watu wanaongea sana bila kujua ukweli,” amesema Dulla.
Msanii huyo pia alionyesha kushangazwa na jinsi watu walivyolichukulia suala hilo. Akisisitiza kuwa si jambo la kiafya kama inavyodhaniwa mitandaoni.
Hata hivyo, sakata hilo lilichukua sura mpya baada ya Dulla Makabila kueleza kukerwa na baadhi ya wasanii wa vichekesho, akidai wamekuwa wakimzungumzia kwa namna isiyofaa mitandaoni.
“Kama hao wasanii wa komedi ndio usinitajie kabisa kwa sasa mimi nawaangalia komedi wa Kenya na wengine nje huko,”amesema.
Aidha baada ya Haji Manara kumuunga mkono Dulla katika kazi yake mpya aliyoachia msanii huyo amesema kwa sasa wako sawa.
“Hakuna tatizo lolote kati yangu na Haji Manara. Tuko sawa kwa muda mrefu,”amesema
Ikumbukwe Januari 24, 2024 Haji Manara alifunga ndoa na aliyewahi kuwa mke wa Makabila, ZaiyLissa na kupelekea wawili hao kuingia kwenye mgogoro. Hata hivyo ndoa hiyo pia haikudumu ikavunjika
Akizungumzia wimbo wake mpya Kidonda Makabila amesema umebeba simulizi ya maisha yake halisi, akidai ulitokana na maumivu ya kuachwa na mpenzi wake.
