Ardhi yaja na vipaumbele vya kumaliza migogoro ya ardhiArdhi yaja na vipaumbele vya kumaliza migogoro ya ardhi

Dodoma. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetaja vipaumbele vinane katika utekelezaji wa bajeti ya Sh210.3 bilioni huku utatuzi wa migogoro ukitajwa kila eneo.

Waziri wa Wizara hiyo, Dk Leonard Akwilapo ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 28, 2026 wakati akiwasilisha bajeti yake mbele ya Bunge na akataja maagizo ya Waziri Mkuu katika utatuzi wa migogoro ya ardhi mijini na vijijini.

Waziri ametaja vipaumbele vilivyoangaziwa mwaka huu ni kuongeza kasi ya upangaji, upimaji, umilikishaji na usajili wa ardhi mijini, vijijini na maeneo ya kimkakati, kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji na kuimarisha mifumo ya Tehama katika utunzaji wa kumbukumbu, utoaji wa huduma, ukusanyaji wa maduhuli na upatikanaji wa taarifa za ardhi na uthamini.

Vipaumbele vingine ni kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kwenye Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na kuhakikisha uwepo wa nyumba bora, ukuaji wa sekta ya milki na maendeleo ya makazi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Tutaimarisha mipaka ya Kimataifa na kuendeleza miji ya mipakani, kuimarisha upatikanaji wa ramani ili kuwezesha uandaaji wa mipango ya Kitaifa na matumizi mengine, kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa vipaumbele,” amesema Dk Akwilapo.

Dk Akwilapo amesema Wizara itatumia kila mbinu na mikakati katika kumaliza migogoro ya ardhi kwa kutumia kamati maalumu ambazo zimeshaanza kuundwa kwa ajili ya kusimamia maagizo hayo, huku akisisitiza suala la ukusanyaji wa maduhuli ikiwemo kodi kwa wapangaji kuwa halitakuwa jambo la hiari.

Amesema katika mwaka 2026/27, Wizara imepanga kukusanya Sh300 bilioni kutokana na kodi ya pango la ardhi, ada na tozo zinazohusiana na sekta ya ardhi akisema lengo hilo litafikiwa kwa kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuendelea kusambaza miundombinu na mifumo ya Tehama katika ofisi za ardhi za mikoa na halmashauri.

“Tunafanya hivyo ili kurahisisha utoaji wa huduma za ardhi; kuendelea kushirikiana na Tamisemi kufuatilia halmashauri ambazo hazijakamilisha utekelezaji wa miradi ya KKK, kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati,” amesema Dk Akwilapo.

Amefafanua kuwa katika mkakati wa kupunguza migogoro, kwa mwaka 2025/26, Wizara ilipanga kuandaa na kusajili Hatimiliki 500,000, Hati za Hakimiliki ya Kimila 520,000, Hati za Sehemu ya Jengo 1,000 na Vyeti vya Ardhi ya Kijiji 100.

Hata hiyo, amelieleza Bunge kuwa, Mei 15,2026 Wizara imeandaa na kusajili Hatimiliki 107,683 sawa na asilimia 21.54 ya lengo, Hati za Hakimiliki ya Kimila 99,762 sawa na asilimia 19.19 ya lengo, Vyeti vya Ardhi ya Kijiji 148 sawa na asilimia 148 ya lengo na Hati za Sehemu ya Jengo 914 sawa na asilimia 91.4 ya lengo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *