KONA YA MSTAAFU: Mstaafu anapoijenga nchi inayoishia kuwa na mishahara miwili tofautiKONA YA MSTAAFU: Mstaafu anapoijenga nchi inayoishia kuwa na mishahara miwili tofauti

Mstaafu wetu anakumbuka sana mwaka ulee wazee wetu walipochanganya michanga ya nchi mbili ili kuziunganisha kuwa nchi moja. Alikuwa ‘denti’ wa shule ya msingi lakini alieleweshwa vyema maana ya kuwa nchi mbili zilizoungana na kuwa nchi moja. Bara na Visiwani.

Miaka ya mwishoni ya sitini na ya mwanzoni ya sabini ikamdhibitishia hivyo, hasa pale Ilipofika wiki ya Pasaka vikundi vya ngoma, taarabu, netiboli ambayo sasa ni marehemu na timu za mpira za Simba, Yanga, Good Hope na nyinginezo ziliposhuka visiwani kusherehekea Pasaka. Wakasherehekea vyema visiwani humo. Si nchi ilikuwa moja?

Mwaka uliofuata ikawa zamu ya vikundi vya huko visiwani, akina Vikokotoni, Miembeni, vya taarabu na vya kandanda vilikuja Dar kupambana na vikundi vya Dar vilivyokuwa vikiwakilisha vikundi vya Bara kwenye michuano hiyo ya kirafiki katika kile tulichoamini ni kuudumisha undugu wetu.

Hata miaka ile ya mwishoni mwishoni mwa 60 tulipoanzisha ‘Azimio la Arusha’ lilikuwa ni kwa ajili ya kutuongoza na kutufanya tujione tulikuwa ndugu kweli tuliokuwa tukiishi nchi moja. Amani iliyoje!

Mambo yakaanza kuwa mengi pale wakubwa zetu walipotuletea kilichofahamika kama ‘Azimio la Zanzibar’. Badala ya kuwa wote ni ‘ndugu’ kama alivyotuaminisha Marhum Baba wa Taifa, tukajikuta tukiaminishwa sasa kuwa kulikuwa na ‘Ndugu’ na kulikuwa na ‘Waheshimiwa’; watu wawili tofauti!

Yale ya tamthiliya ya Shamba la Wanyama ya mwandishi wa Kingereza George Orwell akitumia wanyama kama mfano wa ‘Binadamu wote ni sawa lakini wengine wapo sawa zaidi ya wengine’, yakaanzia hapo na kushika kasi hapa hapa.

Kwa mujibu wa Azimio la Zanzibar’ ikawa ni haki sasa kwa waheshimiwa kujenga na kumiliki siyo makazi ya kuishi wao wenyewe tu, bali sasa hata kujenga na kumiliki nyumba za kupanga na mahoteli.

Hata matibabu yakawa tofauti. Ndugu akiumwa ugonjwa mbaya wa ‘kansa’ anaishia ‘Ocean Road’ lakini mheshimiwa akiumwa mafua au kikohozi tu anakimbizwa fasta India, Ujeruman au Uingereza. Tukaanza kuona wote tulivyo sawa lakini wachache miongoni mwetu wakawa sawa zaidi kuliko sisi ndugu.

Sasa tunafikia mahali pa waheshimiwa kulipwa shilingi milioni, rudia, milioni 14 na marupurupu na marapurapu mengineyo kwa mwezi, rudia hapo, kwa mwezi ukiwa ni mshahara wa miezi kadhaa wa mwalimu au dakitari.

Ndio haya haya ya mheshimiwa huyu akistaafu baada ya miaka mitano, rudia hapo, baada ya miaka mitano ya kazi ngumu ya kuunga mkono hoja kwa kupiga makofi meza badala ya kupiga kofi shavu la asiyeshauri mishahara ya madaktari na walimu iongezwe…

…Ndio, yale yale ya kumlipa mheshimiwa kiinua mgongo cha shilingi 300 milioni baada ya miaka mitano ya kazi ngumu ya kuunga mkono hoja, na kumlipa mstaafu wa kima cha chini Shilingi 39 milioní za kazi ngumu ya kuijenga nchi mpaka kuifikisha hapa ilipofika! 

Inamshangaza sana ndugu mstaafu kwamba hakuna hata mheshimiwa mmoja anayesimama na kutoa hoja ya kuwataka wenzie waunge mkono hoja yake ya wao kutaka mishahara ipungunguzwe na iende kwa wastaafu’ wa kima cha chini ili angalau wapokee oensheni ya shilingi 1 milioni kwa mwezi ?

Inawezekana kweli mtu akalipwa shilingi…mama wee… milioni 14 na marupurupu na marapurapu yake kwa mwezi kwa kukaa kwenye kiti chema Domdom, lakini haiwezekani kupunguza mshahara wake ili kumlipa pensheni ya shilingi moja milioni tu kwa mwezi kima cha  chini mstaafu aliyeijenga nchi kwa jasho kwa kuchimba mitaro na kubeba zege, tunaloambiwa kuwa halilali! 

Mbona kwa wastaafu’ wa kima cha chini limelala? Jamani, tugawaneni keki ya Taifa tuliyohusika kuipika!

0754 340606 / 0784 340606

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *