
Arusha. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Arusha imefanikiwa kudhibiti uuzaji wa viwanja vitatu vyenye thamani ya zaidi ya Sh3 bilioni kinyume na taratibu.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo amesema wamefanikiwa kudhibiti uuzaji huo baada ya kupata taarifa na kufanya uchambuzi wa mifumo yao uliobaini kuwepo kwa mianya ya rushwa katika mchakato wa kuanzia umilikishaji wa viwanja hadi uuzaji wake vilivyopo Kata ya Levolosi jijini Arusha.
Viwanja vilivyohusika ni Kiwanja Namba 1 Kitalu “D” pamoja na Viwanja Namba 5 na Namba 7 Kitalu “F”, ambavyo kwa pamoja vina thamani ya takribani Sh3 bilioni.
“Katika uchunguzi wetu uliofanywa na wataalamu wetu tulibaini kuwepo kwa nyaraka zenye taarifa za uongo zilizowasilishwa katika Ofisi za Halmashauri ya Jiji la Arusha na Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Arusha.”
Amesema nyaraka hizo za uongo zilifanikisha uhamisho wa umiliki wa viwanja hivyo kwa wamiliki wapya kutoka kwa warithi halali kinyume cha taratibu.
Amesema kuwa baadhi ya nyaraka hizo zilionyesha thamani ya kila kiwanja kuwa Sh500 milioni kinyume na uhalisia wa thamani halisi ambayo ni Sh1 bilioni kwa kila kiwanja.
“Baada ya kubaini dosari hizo, Takukuru kwa kushirikiana na Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi pamoja na Halmashauri ya Jiji la Arusha ilifanikiwa kurejesha hati zote tatu katika hali ya awali ikiwemo kurejesha umiliki kwa msimamizi halali wa mirathi.”
Aidha, baada ya marekebisho hayo kufanyika, Kiwanja Namba 1 Kitalu “D” kiliuzwa kwa utaratibu halali kwa thamani ya Sh2 bilioni na kufanikisha Serikali kupata mapato ya Sh90 milioni kupitia kodi na ada mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Takukuru Mkoa wa Arusha imesema imeendelea kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, maji na barabara.
Kwa kipindi hicho, miradi minane yenye thamani ya zaidi ya Sh3.62 bilioni ilifanyiwa ukaguzi ili kuhakikisha ubora wa utekelezaji wake pamoja na thamani ya fedha iliyotumika.
Pia taasisi hiyo imeongeza juhudi za elimu kwa umma ambapo zaidi ya wananchi na wadau 17,000 walifikiwa kupitia semina, mikutano ya hadhara, vipindi vya redio, maonesho pamoja na klabu za wapinga rushwa.
Kwa upande wa uchunguzi na mashtaka, Takukuru Arusha ilipokea jumla ya malalamiko 94 katika kipindi hicho ambapo zaidi ya asilimia 70 yalihusu vitendo vya rushwa.
“Kesi 18 ziliendeshwa mahakamani huku Jamhuri ikifanikiwa kushinda kesi 10 na kuokoa fedha za umma zenye thamani ya zaidi ya Sh205 milioni.”
Wakizungumzia taarifa hiyo, Theresia Mollel mkazi wa Arusha ameipongeza Takukuru kwa utekelezaji huo na kusema kuwa bado kuna matukio mengi ya rushwa mitaani ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi.
“Hiyo ni hatua nzuri lakini bado kwenye huduma za kijamii rushwa ni kubwa, tunaomba maofisa hao wawe pia wanatembelea maeneo ya huduma za kijamii kama shule, afya na maeneo mengine ya kijamii kubaini vitendo hivyo zaidi,” amesema.
