Wadau wataja mbinu za kurejesha imani ya wananchi kwa PolisiWadau wataja mbinu za kurejesha imani ya wananchi kwa Polisi

Dar es Salaam. Wachambuzi wa masuala ya siasa na sheria nchini wamesema Jeshi la Polisi linahitaji mabadiliko ya kina ili kurejesha imani ya wananchi, wakisisitiza umuhimu wa kulifumua ili kuimarisha ufanisi na uwajibikaji wake.

Wamesema mabadiliko hayo yanapaswa kuanzia katika mifumo ya utendaji, mawasiliano na wananchi pamoja na namna chombo hicho kinavyoshughulikia kero za jamii.

Ushauri huo umetolewa siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Camilius Wambura kuangalia namna jeshi hilo linavyojenga imani kwa wananchi, sekta binafsi na jumuiya za kimataifa zilizopo nchini.

Wadau hao wamependekeza kuimarishwa kwa dhana ya Polisi Jamii ili kurejesha ushirikiano wa karibu kati ya polisi na wananchi, hatua inayotarajiwa kusaidia kuongeza uaminifu na kupunguza migogoro.

Matukio mbalimbali kwenye hafla ya kuhitimisha Mafunzo ya Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi, kozi namba 1 ya mwaka 2025/2026, Kurasini Jijini Dar es Salaam Mei 28, 2026.

Aidha, wamesema Jeshi la Polisi linapaswa kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine za Serikali na kijamii ili kupunguza mrundikano wa kero zinazojitokeza katika jamii ambazo si za kiusalama moja kwa moja.

Wamesema ushirikiano huo utaepusha Jeshi la Polisi kubeba mzigo wa kushughulikia kero za wananchi ambazo zilipaswa kutatuliwa na idara nyingine, ikiwemo mabaraza ya ardhi na maofisa ustawi wa jamii.

Mapendekezo ya wadau hao yamelenga kulifanya Jeshi la Polisi kuwa taasisi inayowaaminisha wananchi wanapokuwa na shida.

Pia, wamesema mapendekezo yaliyomo katika Ripoti ya Tume ya Haki Jinai iliyowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan Julai 2023 yanapaswa kufanyiwa kazi.

Alichosema Rais Samia

Rais Samia akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya maofisa wa polisi Mei 28, 2026, alirejea utafiti uliochapishwa na Shirika la Afrobarometer hivi karibuni, ukihusisha wananchi wa Afrika na imani kwa Jeshi la Polisi ambapo kwa Tanzania ni asilimia 12 pekee ya wananchi walikubali kuwa wakiwa na shida watakimbilia Jeshi la Polisi.

Kutokana na utafiti huo, mkuu huyo wa nchi alisema taarifa hizo si za kuzibeza, bali ni kuangalia changamoto zipo wapi hadi wananchi wajibu hivyo, na kisha zifanyiwe kazi.

Si jambo la muda mfupi

Akitoa mapendekezo yake, Mchambuzi wa Masuala ya kijamii Dk Aidan Msafiri amesema kurudisha imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi si jambo la muda mfupi.

“Jambo la kwanza linalopaswa kufanyika ni kuimarisha maadili ya Jeshi la Polisi kwani yameporomoka kwa kipindi cha miaka 20 sasa, kabla ya kujenga imani,” amesema.

Jambo lingine analopendekeza Dk Msafiri ni polisi kujikita katika kutoa huduma kwa raia badala ya kuwa chombo cha kulinda viongozi, kwa kuwa ndiyo sababu ya wananchi kujitenga nao na kutowakimbilia wanapopata shida.

“Jeshi la Polisi linapaswa kufumuliwa na kuundwa kwa mfumo utakaokuwa rafiki kwa wananchi, wananchi wajione wana nafasi ya kutoa ushirikiano na taarifa za siri kwa Polisi,” amesema.

Hatua nyingine aliyoitaja ni jamii kuimarisha malezi ya watoto kwani eneo hilo limekuwa na anguko kubwa.

“Shule zimekuwa ni biashara si eneo la malezi ya watoto, dini nayo malezi yameshuka na hata kwenye jamii, ni muhimu kuwekeza eneo la malezi,” amesema.

Mtazamo huo hauko mbali na wa William Maduhu, wakili katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambaye amesema ili kujenga imani ya Jeshi la Polisi kwa wananchi ni lazima kubadilisha mitalaa ya jeshi hilo.

Matukio mbalimbali kwenye hafla ya kuhitimisha Mafunzo ya Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi, kozi namba 1 ya mwaka 2025/2026, Kurasini Jijini Dar es Salaam Mei 28, 2026.

Amesema mazingira ya kazi ya sasa ya Jeshi la Polisi ni tofauti na nyakati za mkoloni ambapo utaratibu huo ndio unatumika sasa, yaani kuamrisha na kutumia nguvu.

“Ni lazima tuangalie maadili yao, yapo malalamiko mengi ya Polisi kubambikia watu kesi, mtu mwenye maadili hawezi kufanya hivyo. Jambo lingine tulifumue jeshi hili liwe linatoa huduma, lisiwe la kutumia nguvu, hii itaongeza imani kwa wananchi,”amesema.

Wakili Maduhu amependekeza kwenye mitalaa ya mafunzo ya Polisi kuingizwe masuala ya haki za binadamu na kuepuka kutumia njia za kuumiza wananchi kupata ukweli wa jambo, bali watumie mbinu za kisasa za uchunguzi.

Mbali na mapendekezo hayo, Wakili Maduhu amesema imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi imeshuka kutokana na kuwepo kwa askari wasio waaminifu.

“Upo ubambikiaji wa kesi, mtu anakamatwa na kupewa kesi, hata ripoti ya Tume ya Haki Jinai ilieleza hayo, watu wamekimbilia mifumo isiyo rasmi kuliko mifumo rasmi ili kupata haki,” amesema.

Kwa upande mwingine, Mchambuzi wa Masuala ya Siasa Profesa Ali Makame amesema mara nyingi mambo ya kijamii yanahusishwa na Jeshi la Polisi, jambo linaloleta mkanganyiko kuhusu mambo ambayo polisi wanapaswa kufanya.

“Polisi waendelee kusimamia shughuli zilizopo kwenye majukumu yao na kuielewesha jamii namna ya kupambana na changamoto walizonazo na wapi pa kuzipeleka,” amesema.

Jambo lingine, Profesa Makame amependekeza Jeshi la Polisi lishuke chini kwenye jamii ili wananchi wawe karibu nalo ili matatizo yanayoibuka yakiwa chini yao wayashughulikie haraka.

Amesema utafiti wa Afrobarometer si wa kubezwa kwani ndani ya jamii ndio kuna watu na matatizo ndiko yanakoibuka, lakini wananchi wameshindwa kutofautisha shughuli zinazofanywa na jeshi hilo na taasisi zingine.

“Mtu anaweza kugombana na mke akakimbilia polisi sasa unakuta malalamiko ndani ya taasisi hiyo ni mengi, sasa matatizo mengine hayapaswi kushughulikiwa na polisi bali ustawi wa jamii,” amesema na kuongeza:

“Sasa ni vyema Jeshi la Polisi litengeneze ushirikiano na taasisi zinazoshighulika na masuala ya kijami kwa ukaribu,” ameeleza.

Amesema ushirikiano huo utaifanya Jeshi la Polisi, kuwa wakala matatizo yasiyohusika nayo na kuyatawanya idara zinazohusika, akitolea mfano migogoro ya ndoa, mirathi na ardhi.

Mbinu hiyo anasema kusaidia ukaribu baina ya wananchi na Jeshi la Polisi.

 “Wananchi wanahitaji uelewa ili wawe sehemu ya kufanikisha madai na malalamiko ya jinai, ambayo mara nyingi wanalalamika polisi hawafanyi vyema,” amesema.

Profesa Makame amesema kazi na majukumu ya Jeshi la Polisi yanaweza kutofautishwa na majukumu ya kawaida ya jamii.

Amesema matatizo mengi yanayotokea kwenye jamii ni ya kijamii Zaidi, kuliko ya jinai.

“Mambo mengi kati ya hayo ni yale yanayotokana na mahusiano ambayo yanaibua changamoto nyingi, sehemu ya kutafuta suluhu ya changamoto hizo hazitambuliki kwa uwazi, mtu anakimbilia Polisi kwa suala la kijamii na madai,” amesema.

Kilichoelezwa Tume ya Haki Jinai

Mwenyekiti Tume ya Haki Jinai, Jaji Mstaafu, Othman Chande wakati akiwasilisha ripoti yake Julai 2023 mbele ya Rais Samia alitaja vitendo vinavyoondoa imani ya wananchi kwa Polisi na namna ya kuirejesha.

Baadhi ya vitendo hivyo ambavyo wananchi walilalamikia ni kutopata huduma bora na kwa wakati.

Jaji Chande alipendekeza Jeshi la Polisi kufanyiwa tathmini ya kina, itakayowezesha jeshi hilo kufanyiwa marekebisho makubwa, kuundwa upya na kuondoa kasoro za kiutendaji zilizopo.

Matukio mbalimbali kwenye hafla ya kuhitimisha Mafunzo ya Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi, kozi namba 1 ya mwaka 2025/2026, Kurasini Jijini Dar es Salaam Mei 28, 2026.

“Pia, Jeshi la Polisi libadilishiwe sheria, muundo na fikra na kuwa Polisi Tanzania ili kutoa taswira jeshi hilo kuwa chombo cha kuhudumia raia.

Pendekezo lingine alilotaja Jaji Chande, ni ubadilishaji wa mitalaa na mafunzo ya polisi kutoka dhana ya jeshi hadi kuhudumia wananchi.

“Tumependekeza kuimarishwa Polisi Jamii na kuanzishwa programu nyingine ya kulisogeza karibu na jamii, na madawati ya malalamiko ya jamii katika Wizara ya Mambo ya Ndaniyaimarishwe,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *