Msajili arudi na rungu jingine ChademaMsajili arudi na rungu jingine Chadema

Dar es Salaam. Ni kama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inazunguka ndani ya mtego uliowekwa na Msajili wa Vyama vya Siasa baada ya kuandikiwa tena barua ya ofisi hiyo ikitakiwa kujieleza kwa nini isisimamishiwe usajili kutokana na kukiuka masharti ya Sheria ya vyama vya siasa.

Rungu hili la msajili linakuja ikiwa ni wiki chache tu tangu Mei 7, 2026, Msajili akikitaka Chadema kujieleza kwa nini kisichukuliwe hatua za kisheria, ikiwemo kusimamishwa au kutozwa faini kwa madai ya ukiukaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

Baada ya Chadema kudai hivi karibu tayari imejibu barua hiyo ya Msajili, leo Mei 29, 2026 Mwananchi imeshuhudia barua nyingine ya Msajili ya Mei 26, 2026 ikiitaka Chadema kujieleza kwa nini isichukuliwe hatua kwa kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa.

Adhabu ya Msajili dhidi ya Chadema ilipata zuio la muda kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Babati mkoani Manyara.

Leo Mei 29, 2026 Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza akizungumza na Mwananchi amesema barua waliyoiandikia Chadema hawajakiuka amri ya mahakama kwa kuwa hili ni tukio jipya.

“Hiyo ni barua yetu tumewaandikia, wengine wanasema tumekiuka amri ya mahakama hapana, amri ya mahakama ilikuwa ya barua ya  mwanzo hili ni tukio lingine halihusiani na like hili ni jambo jipya kabisa,” amesema.

Kulingana na barua hiyo iliyosainiwa na Naibu Msajili  huyo imeeleza kuwa “Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inatumia fursa hii tena kuwataka Chadema  kuwasilisha maelezo kuhusu utekelezaji wa masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 (Toleo la Urekebu la Mwaka 2023) katika shughuli za chama chenu,” ameeleza.

Msajili katika barua hiyo ameeleza kuwa katika mitandao ya kijamii zipo video zikiaonesha Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa Joseph Mbilinyi, akiongea lugha/maneo ya matusi, kashfa na dhihaka dhidi ya wanasiasa wenzake katika mkutano wa hadhara wa chama hicho.

 Kitendo hicho Msajili amelitaja kama  ukiukwaji wa Kifungu cha 9(2) na 19(2)(f) vya Sheria ya Vyama vya Siasa. Maneno hayo pia yanakiuka Kanuni ya 8(a) ya Kanuni za Kuratibu Mikutano ya Hadhara ya Vyama vya Siasa za Mwaka 2023 (TSN. 209).

Nyahoza amenukuu maneno yaliyotakwa na Mbilinyi kwenye mkutano huo wa hadhara kuwa”…wamekuja na slogan saizi wanazunguka, never, never, never! matako yenu…”

Mbali na hayo, ametaja tukio lingine ambalo lipo kwenye mitandao ya kijamii  vilevile, katika mitandao ya kijamii ikimuonyesha Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini  Samwell Welweli akiongea maneo ya kuchochea watu kuwa na uadui na kupambana na Jeshi la Polisi, badala ya kuheshimu na kufuata sheria za nchi.

Suala hilo pia Msajili amelitaja suala ni ukiukwaji wa kifungu cha 9(2) na 19(2)(1) vya Sheria ya Vyama vya Siasa.

“Bwana Samweli Welwell aliongea maneno yafuatayo, nanukuu, “Tuendelee kusogea, tuendelee kusogea, huko mlioko huko, msiogope polisi, polisi hawatuwezi, simnakumbuka ya tarehe 29 jamani,” ameandika Msajili.

Jambo lingine Msajili ametaja video nyingine ya Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema Taifa, Godbless Lema, mjumbe  akiongea maneno ya kashfa na kijeli katika mkutano wa hadhara.

Suala hilo Msajili amelitaja kuwa ni ukiukwaji wa kifungu cha 9(2) na 19(2)(f) vya Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni ya 8(a) ya Kanuni za Kuratibu Mikutano ya Hadhara ya Vyama vya Siasa za Mwaka 2023.

“Lema, aliongea maneno yafuatayo, nanukuu”…Hamtaki kusemwa achia madaraka rudi kwa mke wako ukae na mke wako…”ameeleza Msajili kupitia barua yake kwa Chadema ikiongeza.

Msajili huyo ameandika kulingana kifungu cha 7 cha Sheria ya Vyama vya Siasa, kifungu cha 39(2)(a) cha Sheria ya Vyama vya Siasa kama kilivyorekebishwa na kifungu cha 19 cha Sheria Namba 3 ya Mwaka 2024 na kwa mujibu wa kifungu cha 45 cha Sheria ya Vyama vya Siasa kama kilivyorekebishwa na kifungu cha 21 cha Sheria Sheria Namba Namba 3 ya Mwaka 2024 na Kanuni ya 11(2) ya Kanuni za Kuratibu Mikutano ya Hadhara ya Vyama vya Siasa za Mwaka 2023, ametoa maelekezo kwa Chadema.

Maelekezo hayo ni chama hicho kuwasilisha maelezo  kwa nini usajili wake usisimamishwe au  kutozwa faini kwa kukiuka masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa ikiwemo masharti ya usajili au kupewa adhabu kwa mujibu wa Kanuni ya 11 ya Kanuni za Kuratibu Mikutano ya Hadhara ya Vyama vya Siasa za Mwaka 2023.

“Maelezo yenu yawasilishwe Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa siyo zaidi ya tarehe 08 Juni 2026 saa tisa na nusu alasiri. Nimekutumia video hizo kwa njia ya baruapepe ya chama na yako binafsi na WhatsApp,”ameandika Msajili.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imewasihi Chadema  tunarudia kuwasihi Chadema kufuata masharti ya Katiba ya Tanzania  ya Mwaka 1977 na Sheria za nchi katika kutekeleza shughuli zenu za kisiasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *