
Mbunge mwandamizi wa Lebanon amesema kuwa harakati ya Hizbullah itaendeleza operesheni zake za kijeshi dhidi ya vikosi vya utawala dhalimu wa Israel.
Hassan Fadlallah, mjumbe wa kambi ya Uaminifu kwa Muqawama katika Bunge la Lebanon, amesema kuwa “uvamizi wa damu” unaoendelezwa na Israel unalenga kukalia ardhi kwa mabavu na kuwafukuza watu makazi yao.
Kauli yake imekuja wakati jeshi katili la Israel likiongeza mashambulizi katika ukanda wa kusini, likilenga vituo vya afya na maeneo ya makazi ya raia, hatua ambayo mashirika ya kibinadamu yanaonya kuwa ni ishara ya kupanuka kwa vita.
Fadlallah amesema: “Tunakabiliwa na uchokozi wa kikatili wa Israel unaolenga kuikalia ardhi yetu na kutufukuza. Hakuna njia nyingine isipokuwa muqawama (mapambano ya silaha) na kusimama imara.”
Mashambulizi hayo yanaotekelezwa na utawala wa Israel ymevuruga makubaliano tete ya usitishaji vita. Israel imekuwa ikitekeleza mashambulizi ya anga pamoja na uvamizi wa nchi kavu ambao umesukuma vikosi vyao kuelekea kaskazini ya Mto Litani kwa mara ya kwanza katika miongo kadhaa.
Fadlallah amesema Hizbullah inapambana na jeshi lililo na silaha za kisasa. Amesisitiza kuwa lengo la muqawama ni “kumchosha” adui kupitia mbinu za kuvizia na kuwazuia wasijikite kikamilifu katika ardhi ya Lebanon.
Wakati Fadlallah akizungumza, ndege za kivita na ndege zisizo na rubani (drones) za Israel zilikuwa zikishambulia maeneo ya kusini, ikiwemo mji wa Nabatieh na miji ya Kfar Roumnan, Shoukine, na Ain Qana. Shambulio moja lililenga kituo cha afya katika mji wa Deir Qanoun al-Nahr, muundo wa mashambulizi ambao umezua shutuma kutoka kwa mashirika ya kimataifa ya matibabu.
Takwimu kutoka Wizara ya Afya ya Lebanon zinaashiria kulengwa kwa makusudi kwa wahudumu wa huduma za afya. Kulingana na rekodi za Wizara ya Afya ya Lebanon, tangu Machi 2, angalau wahudumu wa afya 42 wameuawa katika mashambulizi ya Israel. Aidha tangu wakati huo Israel imeua Walebanon wasiopungua 3,300 na kujeruhiwa wengi zaidi ya 10,000.
Fadlallah amesema kuwa Marekani inatoa kinga ya kisiasa na kijeshi kwa utawala vamizi wa Israel, akieleza kuwa uhalifu wa Israel unafanyika kwa “taa ya kijani kutoka Marekani na kimya chenye shaka kutoka kwa serikali ya Beirut.”
Pia amesema serikali ya Lebanon inatumia mazungumzo yanayoendelea kama “jukwaa la kisiasa” kwa ajili ya adui.
Fadlallah amebaini kuwa Israel inajaribu kurudia kusini mwa Lebanon ile ile mbinu ya kuikalia kwa mabavu milima ya Golan iliyoipora kutoka Syria.
