
Mtandao wa Madaktari wa Sudan umeripoti kuwa wanamgambo wenye mfungamano na Kikosi cha wapiganaji wa RSF kimewaua takriban raia 27, wakiwemo wazee, katika mashambulizi dhidi ya vijiji kadhaa magharibi mwa Bara katika jimbo la Kordofan Kaskazini.
Taasisi hiyo ya tiba yenye makao yake Cairo imeeleza kuwa mashambulizi hayo yalifanywa siku ya Alhamisi katika eneo la al-Murrah, na kuyataja kama “jinai mpya inayolenga raia wasio na silaha katika maeneo ambayo ulinzi wa jeshi.
Sudan imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu Aprili 2023, wakati mvutano wa muda mrefu kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF ulipozuka na kuwa mzozo mkubwa ambao umeua mamia kwa maelfu ya watu na kupelekea mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao.
Eneo la Kordofan limekuwa mojawapo ya viwanja vikuu vya vita, huku mapigano yakishtadi katika pande kadhaa, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani.
RSF na wapiganaji waitifaki wao wanadhibiti sehemu kubwa ya eneo la magharibi la Darfur, pamoja na baadhi ya maeneo ya Kordofan katika mpaka na Sudan Kusini, maeneo yenye utajiri wa mafuta na migodi ya dhahabu.
