Iran yakemea vikali tishio la Marekani la kuiwekea Oman vikwazo

Msemaji wa wizara hiyo, Esmaeil Baghaei, ametoa kauli hiyo baada ya Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, kutoa tishio hilo.

Baghaei amesema matamshi hayo ya vitisho  ni “jaribio la kushinikiza dola huru mwanachama wa Umoja wa Mataifa, na ishara nyingine ya kufilisika kwa maadili ndani ya mfumo wa utawala na utungaji sera wa Marekani.”

Amesisitiza kuwa kutishia kuiwekea Oman vikwazo kwa kisingizio kisicho na msingi ni kitendo kisicho halali kabisa na kinachokwenda kinyume na misingi ya msingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa pamoja na sheria za kimataifa.

Afisa huyo ameongeza kuwa jumuiya ya kimataifa inapaswa kujibu kwa uwajibikaji dhidi ya mwenendo wa aina hiyo ili kuzuia kuhalalishwa taratibu kwa ukiukaji wa kanuni za sheria za kimataifa.

Siku ya Jumatano, Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa “atailipua” Oman iwapo ingekubali kushirikiana na Iran katika udhibiti wa Mlango Bahari wa Hormuz.

Akijibu kauli hizo, Baghaei amesema  Iran ina mshikamano na nchi rafiki na ndugu ya Oman na kuongeza kuwa tishio hilo limetolewa dhidi ya nchi ambayo “daima imekuwa na nafasi chanya, yenye ufanisi, na ya kuwajibika katika amani na usalama wa kikanda; ambayo kwa miaka mingi imekuwa mpatanishi katika michakato ya kidiplomasia, na imejitahidi kuhudumia amani na uthabiti wa eneo hili.”

Msemaji huyo amebainisha kwamba tishio kama hilo “si tu kwamba linakiuka kanuni ya marufuku ya kutishia au kutumia nguvu, bali pia ni dalili nyingine hatari ya kuzoeleka kwa uasi wa sheria na uonevu katika mahusiano ya kimataifa.”

Iran na Oman kwa sasa zinafanya mazungumzo kuhusu mfumo mpya wa usafiri wa majini kupitia Mlango Bahari wa Hormuz.

Iran ilifunga mlango huo kwa maadui wake na washirika wao kufuatia kuanza, tarehe 28 Februari wakati Marekani na Israel zilipoanzisha vita haramu dhidi ya nchi hii.

Baadaye ilianza kutekeleza udhibiti mkali zaidi baada ya Trump kutangaza mzingiro haramu dhidi ya meli na bandari za Iran, hatua iliyoendeleza uchokozi huo na kukiuka masharti ya usitishaji vita.

Mnamo tarehe 20 Mei, mamlaka ya Iran inayosimamia Mlango Bahari wa Hormuz katika Ghuba ya Uajemi ilifafanua eneo la usimamizi na uangalizi wa njia hiyo ya maji.

Hadi sasa, Jeshi la Majini la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetoa vibali vya kupita kwa makumi ya meli kwa ajili ya kuvuka njia hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *