TIMU za wanawake za Arsenal na Manchester United zimeanza kufuatilia huduma ya kiungo mshambuliaji wa RB Leipzig ya Ujerumani, Lisa Baum ambaye ana asili ya Tanzania na Ujerumani.
Licha ya kuwa na uraia wa nchi hizo mbili kiungo huyo hajawahi kuitumikia Twiga Stars licha ya kukiri mara kadhaa anatamani siku moja kuichezea, hadi sasa ameichezea timu ya Taifa ya Ujerumani U-23.
Nyota huyo chipukizi ni mmoja wa wachezaji wanaowindwa zaidi dirisha hili la usajili baada ya kuvutia vigogo mbalimbali wa Ulaya kutokana na kiwango chake bora akiwa na RB Leipzig msimu huu.
Baum, 19, ameonyesha kiwango kikubwa msimu wake wa kwanza akiwa Leipzig tangu alipojiunga na klabu hiyo akitokea Hamburger SV.
Kiwango chake kimeifanya Leipzig kuvimba dirisha hili na huenda ikawa moja ya timu zitakazonufaika na uhamisho wa nyota huyo endapo itaamua kumuuza.
Ripoti mbalimbali kutoka Ulaya zinaeleza mabingwa wa Ulaya, FC Barcelona Femení, ni miongoni mwa timu zinazofuatilia kwa karibu maendeleo ya mchezaji huyo anayesifika kwa kasi, uwezo wa kupiga chenga na kucheza katika maeneo mbalimbali ya ushambuliaji.
Mbali na Barcelona, pia Olympique Lyonnais Féminin, Manchester United Women, Bayern Munich Women pamoja na London City Lionesses zimetajwa kuonyesha nia ya kupata saini yake.
Kati ya hizo inaelezwa Arsenal ambayo ilimaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi ya Wanawake England ikiwa na pointi 51 nyuma ya mabingwa wapya Man City, ndiyo timu iliyoko mbele zaidi na siriazi kwenye uhamisho huo.
Msimu wa 2025/26, Baum alikuwa miongoni mwa wachezaji walioibeba Leipzig kufanya vizuri kwenye Ligi ya Wanawake ya Bundeslinga akicheza mechi 24 kati ya 26 za ligi kwa dakika 2296 akifunga mabao sita na asisti tano. Takwimu hizo zimechangia timu hizo kupambania saini yake.
Iwapo atakamilisha dili lolote kati ya timu hizo katika dirisha lijalo, Baum anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji wa kike wa Kijerumani watakaovunja rekodi za ada za usajili.