Dar es Salaam. Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza ametinga makao makuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yaliyopo Mikocheni, Dar es Salaam, kwa ajili ya kikao maalumu na uongozi wa chama hicho.

Nyahoza akiwa ameambatana na maofisa wa sheria wa ofisi ya Msajili wamewasili makao makuu ya chama hicho asubuhi ya leo Jumatatu, Juni 1, 2026 na kupokewa na viongozi mbalimbali wa Chadema ikiwemo Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, na wajumbe wengine wa kamati kuu.

Hiki ni kikao cha kwanza cha ana kwa ana kati ya pande hizo mbili baada ya Chadema kutoka katika kipindi cha sintofahamu ya kisiasa.

Ni muda mrefu, pande hizo zimekuwa zikibadilishana kauli kupitia vyombo vya habari na mawasiliano ya barua huku kila upande ukimtuhumu mwenzake kwa mambo mbalimbali.

Kwa upande wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Chadema imekuwa ikituhumiwa kwa muda mrefu kwa madai ya kukiuka masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019.

Miongoni mwa tuhuma hizo ni viongozi wa chama kutoa kauli zinazotafsiriwa za matusi au zinazokwenda kinyume na misingi ya sheria na Katiba ya nchi.

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza (wapili kulia) akiwa kwenye kikao na viongozi wa Chadema,jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga

Kwa upande wa viongozi wa Chadema wamekuwa wakiikosoa ofisi ya msajili, kwa kile wanachodai ni matumizi mabaya ya mamlaka na kuendesha mikakati inayolenga kukidhoofisha chama hicho, pamoja na kufanya maamuzi ambayo hayana manufaa kwa umma.

Kabla ya kikao hicho, Nyahoza alinukuliwa na chombo kimoja cha habari akieleza angekutana na viongozi wa Chadema leo saa tano asubuhi kwa ajili ya kujadiliana masuala ya kisheria.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari, Mnyika amesema ziara ya Nyahoza na timu yake haikulenga kuelimishana kuhusu sheria, bali kujadili masuala mawili muhimu.

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa,Sisty Nyahoza (wapili kulia) akiwa kwenye kikao na viongozi wa Chadema, jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga

“Amekuja kuona muundo wa dawati la jinsia ndani ya chama na namna linavyofanya kazi. Pili, amekuja kufahamu mchakato wa utekelezaji wa sera ya jinsia na ushirikishwaji wa jamii.

“Umma uelewe ujio wa Ofisi ya Msajili katika makao makuu ya chama hauna uhusiano wowote na barua ambazo wamekuwa wakituandikia wakitaka tujieleze kuhusu kauli mbalimbali za viongozi wetu,” amesema Mnyika.

Amesema hakuna sababu ya kupotosha umma, Ofisini ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu madhumuni ya ziara hiyo.

“Kimsingi, Chadema ndiyo iliyoialika Ofisi ya Msajili kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, kifungu cha 10(c), kinachohusu uundwaji wa madawati ya jinsia na utekelezaji wa sera husika.

Tumeona ni vyema kuwapa nafasi hiyo, ingawa tunaendelea kuwa na mtazamo kwamba ofisi hiyo imekuwa ikitoa taarifa zinazopotosha,” amesema.

Mnyika amesema ziara hiyo inatokana na barua iliyotumwa na Ofisi ya Msajili Aprili 28, 2026 kwa makatibu wa vyama vya siasa, ikieleza dhamira ya kutembelea vyama hivyo kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa masuala ya jinsia kwa mujibu wa sheria.

“Baada ya kupokea barua hiyo, tuliwajibu muda waliopendekeza haukuwa mwafaka kwetu. Tulipendekeza Juni 1, 2026, ambayo ni leo, kuwa siku ya kukutana. Hivyo, ujio wao hauna uhusiano wowote na barua nyingine ambazo wamekuwa wakitutaka kujieleza kuhusu kauli za viongozi wetu,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *