
Morogoro. Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema hakuna ruzuku ya mafuta kwa sasa kwa kuwa bei kwenye soko la dunia imeanza kushuka kutoka Dola za Marekani 122 milioni hadi kufikia Dola 87 milioni kwa pipa moja, hivyo bei ya mafuta nchini itashuka.
Msigwa ameyasema hayo leo Juni Mosi, 2026 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mkoani Morogoro, ambapo amesema matarajio ni kwamba bei hiyo ya mafuta itaendelea kushuka na ikishuka kwenye soko la dunia hata hapa nchini pia itashuka.
Akijibu swali la mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni Cha Abood, Mohamed Issa kwenye mkutano na waandishi wa habari aliyeuliza nini mpango wa Serikali katika kudhibiti kupanda kiholela kwa nauli za mabasi makubwa na daladala, ambapo katika majibu yake amewataka wananchi kutoa taarifa kwenye mamlaka husika ikiwemo Latra (Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini) endapo watalipishwa nauli tofauti na zilizotangazwa.
“Mafuta yakipanda baadhi ya watu wanadhani ni kosa la Serikali, sio kosa la Serikali nchi yetu haina mafuta tunaagiza kutoka nje, bei itakayonunuliwa huko ndio itakayofanya bei ipande ama ishuke yanapofikishwa hapa kwetu,” amesema Msigwa
Aidha amesema kuwa kama nchi ikiamua kung’ang’ania kupunguza bei ya mafuta katika kipindi hiki itajikuta inakosa dawa, inakosa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya barabara, itakosa fedha zinazosaidia watoto kupata elimu na mambo mengine kwa ajili ya ustawi wa wananchi.
“Sio kwamba Serikali haitambui changamoto hiyo, tunatambua ila tunaliangalia jambo hili kwa uangalifu kwa sababu unaweza ukakimbilia kuweka ruzuku kwenye mafuta ukaathiri huduma nyingine za wananchi,” amesema Msigwa.
Pamoja na hayo, amesema bei za nauli zinadhibitiwa na Latra na sheria ipo na dereva ama kondakta yeyote atakayetoza nauli tofauti na zile zilizotangazwa na mamlaka hiyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Swali jingine Ia mwandishi wa habari wa Channel Ten, Jimmy Mengele aliyetata kujua ni lini Serikali itapanua barabara ya Morogoro – Dar es Salaam ambayo kwa sasa inaonekana kuwa finyu lakini pia upi mpango wa Serikali katika kutengeneza barabara za katika ya mji wa Morogoro ambazo zimekuwa na mashimo.
Akijibu swali hilo Msigwa amekiri kuwa barabara nyingi hapa nchi zimeathiriwa na mvua nyingi za masika zilizonyesha mwaka huu, hata hivyo Serikali kupitia wakala wa barabara nchini Tanroads na wakala wa barabara vijijini Tarura wameanza kuboresha miundombinu hiyo.
Kuhusu mafuriko yanayotokea mara kwa mara katika kata ya Kihonda na Lukobe Manispaa ya Morogoro, Kilosa, Kilombero na Mvomero Msigwa amesema Serikali imekuwa na mipango mbalimbali ya kujenga mabwawa ambayo yatasaidia kuondoa changamoto hiyo ya mafuriko.
Hata hivyo amesema mipango ya Serikali ya Mkoa wa Morogoro ni kuzibua mitaro na mifereji iliyopo katikati ya mji Ili kudhibiti mafuriko.