Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuanza ziara ya kitaifa ya siku tatu nchini Urusi kuanzia Juni 3 hadi 5, 2026, ambapo atafanya mazungumzo rasmi na Rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin, pamoja na kushiriki katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF 2026).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Bakari Machumu, usiku wa Juni 1, ziara hiyo ni ya kihistoria kwani itakuwa ya pili kufanywa na Rais wa Tanzania nchini Urusi tangu alipozuru nchi hiyo mwaka 1969 Baba wa Taifa, Julius Nyerere.

Katika ziara hiyo, Rais Samia na mwenyeji wake Putin wanatarajiwa kufanya mazungumzo katika Ikulu ya Kremlin, jijini Moscow, yakilenga kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na Urusi katika sekta mbalimbali za kimkakati, zikiwamo biashara na uwekezaji, elimu, sayansi na teknolojia, nishati, madini, kilimo na miundombinu.

Ziara hiyo inafanyika wakati Tanzania ikiendelea kutekeleza kwa kasi ajenda ya diplomasia ya uchumi inayolenga kuvutia uwekezaji, kuongeza biashara ya kimataifa na kufungua fursa mpya za maendeleo kupitia ushiriki katika majukwaa makubwa ya kimataifa.

Akiwa nchini Urusi, Rais Samia atakuwa miongoni mwa viongozi wa dunia watakaohutubia katika SPIEF 2026, jukwaa linalowakutanisha wakuu wa nchi, viongozi wa biashara, wawekezaji, taasisi za fedha na wataalamu wa sera kujadili mwenendo wa uchumi wa dunia na fursa za ushirikiano wa kimataifa.

Ushiriki wake katika mkutano huo unatarajiwa kutoa fursa kwa Tanzania kuwasilisha mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, pamoja na kuonyesha mageuzi ya mazingira ya biashara, maendeleo ya maeneo maalumu ya kiuchumi, ujenzi wa uchumi wa viwanda na fursa zilizopo katika sekta za nishati, madini, miundombinu na utalii.

Mbali na kushiriki SPIEF 2026, Rais Samia pia atahudhuria Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi litakalowakutanisha viongozi wa biashara, wawekezaji na taasisi za kukuza uwekezaji kutoka mataifa hayo mawili.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kongamano hilo litajadili namna ya kuongeza kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Urusi ambacho kwa sasa kinafikia Dola za Marekani milioni 307.5 kwa mwaka, sambamba na kufungua fursa mpya za uwekezaji na uhamishaji wa teknolojia.

Aidha, Tanzania na Urusi zinatarajiwa kusaini mikataba kadhaa ya ushirikiano katika maeneo ya elimu ya juu, sayansi na teknolojia, uwekezaji pamoja na teknolojia ya habari na mawasiliano.

Katika hatua nyingine, Rais Samia anatarajiwa kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu (Honoris Causa) na RUDN University kwa kutambua mchango wake katika uongozi, mageuzi ya elimu, kuimarisha diplomasia ya Tanzania na kuitangaza nchi kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *