Unguja. Watu wanne wamefikishwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa makosa matano ya kusafirisha kuuza na kuhifadhi dawa za kulevya Zanzibar.

Washtakiwa hao, Alexandru  Rizescu (23), Raia wa Romania, Ali Said Abdallah (53), Feisal Masoud Said (31) na Mussa Burhan Musoma (49), wamefikishwa mahakamani leo Juni 2, 2026 mbele ya Jaji Said Hassan Said.

Akiwasomea mashtaka yao mahakamani hapo katika kesi ya jinai namba 28/26 IR 24/26, Wakili wa Serikali Mkuu, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Ayoub Nassor Sharif amedai washtakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya Desemba 2025 na Januari 29 2026 katika maeneo tofauti Unguja.

Katika kosa la kwanza, amedai linamkabili Alexandra na Ali Said ambao katika muda usiojulikana kwenye bandari ya Malindi, walipatatikana wakisafirisha maboksi 132 ya shisha kutoka China, ambapo ndani yake kulikuwa na viambata vya dawa za kulevya aina ya kokeini yenye uzito wa gramu 750.069 jambo ambalo ni kosa kisheria.

Katika kosa la pili kwa mshtakiwa namba moja na namba mbili, walikutwa bandari ya Malindi wakisafirisha maboksi 220 kutoka China kwa kutumia usafiri wa majini unaomilikiwa na kampuni ya Slim Trading Ltd. Boksi hizo zilikuwa za shisha zikiwa na viambata vya dawa za kulevya aina ya Lysergic acid diethylamide (LSD) yenye uzito wa gramu 996.358.

Kosa la tatu linalowahusu mshtakiwa wa kwanza, wa pili na watatu, amesema Januari 29, 2026 saa 7:30 mchana maeneo ya Shangani mjini Unguja, bila halali yoyote walipatikana wakiuza dawa za kulevya aina ya kokeini yenye uzito wa gramu 750 kwenye duka la Shop “N” Go ambayo imechanganywa katika shisha zilizokuwa zinauzwa kwenye duka hilo.

Katika kosa la nne linawakabili mshtakiwa wa kwanza hadi wa tatu, ni kupatikana na zana za kutayarisha dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 22 (1) cha Sheria ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, sheria namba nane ya mwaka 2021 kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria namba tano ya mwaka 2024.

“Washatakiwa wote watatu katika maeneo ya Shangani duka lenye jina Shop “N” Go, nyote kwa pamoja mlipatikana na mashine 49 zinazotumika kusagia dawa za kulevya, jambo ambalo ni kosa kisheria,” amedai.

Pia, kosa la tano linawahusu washtakiwa wote watano ambapo Januari 29, 2026 maeneo ya Mpendae, walipatikana wakiwa wamehifadhi pisi 560 za shisha zenye viambata vya dawa za kulevya aina ya Lysergic Acid Diethylamide (LSD) katika ghala lililopo Mpendae jambo ambalo ni kosa kisheria.

Hata hivyo, washtakiwa wamekana makosa hayo na kurudishwa rumande hadi kesi yao itakapotajwa tena Novemba 10, 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *