Dodoma. Tume ya Taifa ya Mipango imesema mafanikio ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 yatategemea ushiriki wa wadau mbalimbali, ikiwamo sekta binafsi, mashirika ya kiraia na wananchi, kwa kuwa dira hiyo ni ya Taifa na si ya Serikali pekee.
Akizungumza leo Jumanne Juni 2, 2026 jijini Dodoma katika mkutano wa wadau wa mashirika ya kiraia uliojadili maandalizi ya utekelezaji wa Dira 2050, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango anayeshughulikia Mipango ya Kitaifa, Dk Mursali Milanzi amesema maandalizi hayo yanalenga kuhakikisha utekelezaji wa dira unaanza kwa ushirikiano mpana kuanzia Julai Mosi, 2026.
Amesema Tume imekuwa ikishirikisha wadau mbalimbali katika uandaaji wa mipango ya Taifa na kwa sasa inafanya kazi kwa karibu na taasisi ya Policy Innovation Lab Africa (PIL-A) kuweka mazingira yatakayowezesha utekelezaji wa dira hiyo kwa ufanisi.
“Dira hii si ya Serikali, ni ya nchi. Ndiyo maana tunahitaji wadau wote kuwa sehemu ya utekelezaji wake. Serikali imeandaa mazingira kupitia wizara, idara na taasisi zake, lakini tunahitaji pia mchango wa sekta binafsi na mashirika ya kijamii,” amesema Dk Milanzi.
Mkurugenzi wa taasisi ya Policy Innovation Lab Afrika (PAL-A) Carolyn Kandusi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa mashirika ya kiraia kwenye utekelezaji wa Dira 2050 Jijini Dodoma leo Juni 2, 2026 Jijini Dodoma. Picha na Rachel Chibwete
Ameeleza kuwa mkutano huo ni hatua ya awali ya kuwaunganisha wadau kabla ya kuanza rasmi kwa utekelezaji wa dira, ili kila mmoja aelewe nafasi na wajibu wake katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya nchi kwa miaka 25 ijayo.
Amesema mashirika ya kiraia na wadau wengine wa maendeleo wamekuwa wakifanya ubunifu unaotoa matokeo makubwa katika sekta mbalimbali za kijamii, hivyo ubunifu huo unapaswa kuunganishwa katika utekelezaji wa dira ili kuongeza tija na kupunguza gharama za utekelezaji.
“Tunataka kuona si Serikali pekee inayotekeleza dira, bali pia wadau wengine. Hivyo ni muhimu kujua nani anafanya nini ili mwisho wa siku tuweze kupima mchango wa kila mdau katika kufanikisha dira,” amesema.
Dk Milanzi amesema jukumu la Tume ni kuratibu juhudi za wadau wote ili kuhakikisha wanatekeleza malengo ya taifa kwa mwelekeo mmoja badala ya kufanya kazi kwa kujitegemea.
Aidha, amesema Serikali imeandaa mkakati wa mawasiliano wa Dira 2050 utakaotumika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu maudhui ya dira na nafasi yao katika utekelezaji wake.
“Tutatumia njia mbalimbali kuwafikia wananchi. Tutawaeleza kwamba dira imekamilika, tutawaonyesha nafasi yao katika utekelezaji wake na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu kwa kuwa wao ndiyo waliotoa maoni yaliyotumika kuandaa dira hii,” amesema.
Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Policy Innovation Lab Africa (PIL-A), Carolyn Kandusi, amesema ni muhimu mashirika ya kiraia kuhakikisha miradi na shughuli zake zinaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi.
Amesema mashirika hayo tayari yana mchango mkubwa katika sekta za elimu, afya, mazingira, ajira kwa vijana na maendeleo ya uchumi, hivyo kuna umuhimu wa kuunganisha juhudi hizo na vipaumbele vya Taifa.
“Serikali inaendelea kufanya kazi kubwa ya kujenga uchumi wa nchi kuelekea azma ya kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050. Sisi kama wadau wa maendeleo tunaona kuna haja ya kuhakikisha kazi tunazofanya zinaendana na mwelekeo huo wa Taifa,” amesema Carolyn.
Amebainisha kuwa moja ya changamoto zinazoweza kujitokeza ni taasisi mbalimbali kufanya kazi kwa kujitegemea bila uratibu wa pamoja, hali inayoweza kusababisha kurudiwa kwa shughuli zinazofanana na kupunguza ufanisi wa matumizi ya rasilimali.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa wadau wa mashirika ya kiraia unaohusu kujadili mchango wa mashirika hayo kwenye utekelezaji wa Dira 2050 Jijini Dodoma leo Juni 2, 2026.
Carolyn amesema mkutano huo umelenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu vipaumbele vya Taifa, nafasi ya kila mdau na namna ya kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema hadi mwaka 2025 sekta ya kiraia tayari imewekeza zaidi ya Sh1 trilioni katika miradi mbalimbali ya afya, elimu, mazingira, uwezeshaji wa vijana, ajira na ukuaji wa uchumi,
“Tukiwa na ushirikiano mzuri zaidi na mfumo ulio wazi wa uratibu, mchango wa sekta ya kiraia katika maendeleo ya taifa utakuwa mkubwa zaidi kuliko ulivyo sasa,” amesema Carolyn.