Mixx kwa kushirikiana na Hisense imeendelea na uzinduzi wa kampeni yake ya “Kila Muamala ni Bao la Ushindi” visiwani Zanzibar, baada ya uzinduzi rasmi uliofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx, Angelica Pesha, alisema kampeni hiyo imezinduliwa wakati ambao hamasa ya Kombe la Dunia inaendelea kuongezeka miongoni mwa Watanzania, ambao wengi wana mapenzi makubwa na mchezo wa mpira wa miguu.

“Mpira wa miguu una uwezo wa kuunganisha watu kwa namna ya kipekee. Kuelekea Kombe la Dunia, tumeona ni wakati sahihi wa kusherehekea pamoja na wateja wetu kwa kuwapa fursa ya kushinda zawadi zinazoweza kubadili maisha,” alisema Pesha.

Aliongeza kuwa kampeni hiyo pia inalenga kuhamasisha matumizi ya huduma za fedha kidijitali huku ikitoa motisha kwa wateja kupitia zawadi mbalimbali zitakazotolewa katika kipindi chote cha kampeni.

“Kila muamala unaofanyika unaweza kuwa mwanzo wa ushindi mkubwa kwa wateja wetu wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” alisema.

Kupitia kampeni hiyo, Mixx inatoa zawadi za Sh1milioni kila siku, zawadi za vifaa vya kielektroniki kutoka Hisense, ikiwemo televisheni ya inchi 55, spika za muziki pamoja na majokofu ya milango miwili.

Katika zawadi kubwa zaidi za kampeni hiyo, washindi watano watasafirishwa kwenda Mexico kushuhudia mechi za Kombe la Dunia mubashara huku gharama zote zikigharamiwa kikamilifu. Aidha, mshindi mmoja wa droo ya mwisho wa kampeni ataibuka na kitita cha Sh50 milioni.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Mars Communications Ltd, wasambazaji wa vifaa vya Hisense nchini, Tahera Karim, alisema ushirikiano kati ya Hisense na Mixx unalenga kuwapa Watanzania thamani zaidi kupitia zawadi za teknolojia ya kisasa.

“Tunafurahi kushirikiana na Mixx katika kampeni hii inayowawezesha Watanzania kushinda zawadi zenye thamani kubwa huku wakitumia huduma wanazozihitaji kila siku. Kupitia Hisense, tunatoa bidhaa za teknolojia ya kisasa zinazoboresha maisha ya watumiaji, na tunaamini kampeni hii itawagusa watu wengi zaidi Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” alisema.

Kwa wakazi wa Zanzibar, kampeni hiyo inafungua fursa mpya za ushindi kupitia miamala ya kawaida ya kila siku huku ikiongeza hamasa ya Kombe la Dunia kwa maelfu ya watumiaji wa huduma za Mixx visiwani humo.

Fainali za Kombe la Dunia zinatarajiwa kuanza Juni 11 na kumalizika Julai 19 zikifanyika kwenye nchi za Mexico, Canada na Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *