Mshambuliaji wa Ureno, Cristiano Ronaldo atakuwa miongoni mwa nyota 26 watakaoliwakilisha taifa lao katika Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico.

Ronaldo alianza kuitumikia Ureno kwa mara ya kwanza Agosti 20, 2003 alipokuwa na miaka 18 na alianza kucheza Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika Fainali za 2006 zilizofanyika Ujerumani.

Nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo akionekana kusikitika baada ya timu yake kutolewa na Morocco katika Fainali za Kombe la Dunia 2022 Qatar. Picha na Mtandao

Bahati mbaya inayomkabili

Tangu aanze kushiriki Fainali za Kombe la Dunia, nyota huyo wa Ureno hadi sasa amefunga mabao nane katika Fainali tano zilizopita za Kombe la Dunia alizoichezea Ureno katika mechi 22.

Hata hivyo, nuksi inayomuandama Ronaldo ni ya kutoifungia Ureno katika hatua za mtoano katika mashindano hayo makubwa duniani.

Mshambuliaji huyo alishindwa kufanya hivyo kwa mara ya kwanza 2006 ambapo Ureno ilifanikiwa kufika hatua ya nusu fainali.

Ronaldo alishindwa kufunga katika mechi za hatua ya 16 Bora na robo fainali ambazo Ureno ilizitupa nje Uholanzi na England.

Pia alishindwa kufanya hivyo katika mechi ya nusu fainali ambayo Ureno ilitolewa na Ufaransa kwa kichapo cha bao 1-0 lililofungwa na Zinedine Zidane.

Vilevile katika Fainali za 2010 zilizofanyika Afrika Kusini, Ronaldo hakuweza kutamba baada ya Ureno kutupwa nje ya mashindano katika hatua ya 16 bora ilipotolewa kwa kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Hispania ambao ndio walitwaa ubingwa wa mwaka huo.

Nyota wa Ureno, Cristiano Ronaldo akionekana kusikitika baada ya timu yake kutolewa katika hatua ya makundi katika Fainali za Kombe la Dunia 2014 Brazil. Picha na Mtandao

Katika Fainali za 2014 zilizofanyika Brazil, Ronaldo alishindwa kuisaidia Ureno kupenya katika hatua ya 16 bora baada ya timu yake kuishia katika hatua ya makundi ikikusanya pointi nne pekee katika kundi G lililokuwa na timu za Marekani, Ghana na Ujerumani.

2018 katika Fainali zilizofanyika Russia, ulikuwa mwaka wa mafanikio kwa Ronaldo baada ya kufanikiwa kupachika idadi ya mabao manne katika hatua ya makundi.

Hiyo ilikuwa ni idadi kubwa ya mabao katika mashindano hayo kwani hakuwahi kufunga zaidi ya bao moja katika mashindano hayo hapo kabla.

Ronaldo alifunga mabao matatu katika mechi iliyoisha kwa sare ya 3-3 dhidi ya Hispania kisha bao lingine akafunga katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Morocco.

Hata hivyo, katika mechi ya hatua ya 16 bora mshambuliaji huyo alishindwa kuonyesha makali yake, Ureno ilipotolewa kwenye mashindano na Uruguay baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-1.

Katika mchezo huo mabao yote mawili ya Uruguay yalifungwa na Edinson Cavani, bao pekee la Ureno lilipachikwa na Pepe.

Mambo yaliendelea kuwa mabaya katika Fainali za 2022 zilizofanyika Qatar ambapo Ronaldo alifunga bao moja pekee katika mechi tano.

Katika hatua za mtoano, Ureno iliishia robo fainali na mshambuliaji huyo hakuweza kufunga bao katika mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Switzerland pamoja na ule wa robo fainali ilipotolewa na Morocco kwa kichapo cha 1-0.

Katika fainali za mwaka huu Ureno imepangwa katika kundi K pamoja na Mataifa ya DR Congo, Colombia na Uzbekistan.

Iwapo Ureno itafanikiwa kupenya katika hatua za mtoano, huenda ikaja kushuhudiwa kwa mara ya kwanza Ronaldo akishangilia bao katika hatua hizo tangu alipoanza kucheza michuano hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *