
Dar es Salaam. Hali ya sintofamu imeanza kujitokeza ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kusini, baada ya kufanya uteuzi wa wajumbe wa kamati za kudumu unaolalamikiwa na baadhi ya viongozi na kuibua mgawanyiko.
Hata hivyo, Kaimu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini, Ponera Belchomas alisisitiza kuwa uteuzi wa kamati hizo umefuata taratibu zote zinazotakiwa, wenye malalamiko wana mambo yao binafsi.
Sintofahamu hiyo imekuja ikiwa imepita miezi mitano hali kama hiyo ilipojitokeza katika Kanda ya Nyasa hatua iliyolazimu ofisi ya katibu mkuu wa Chadema kuingilia kati na kutoa maelekezo ya kubatilisha uteuzi uliofanywa, jambo ambalo inadaiwa hadi sasa halijatekelezwa.
Kiutendaji Chadema ina kanda 10 za Pwani, Unguja, Pemba, Serengeti, Nyasa, Kusini, Kaskazini, Kati, Victoria na Magharibi. Hata hivyo, ili kanda hizo zitekeleze majukumu yake kwa ufanisi, zinahitaji kamati za kudumu ambazo ndio injini.
Chanzo cha tatizo
Akisimulia chanzo cha mkasa huo, mmoja wa wajumbe wa kamati ya utendaji Kanda ya Nyasa, Haji Swalehe ameliambia Mwananchi Mei 16, mwaka huu walikuwa na kikao cha kuteua kamati za kanda kilichofanyika mkoani Ruvuma.
“Hiki kikao kilikuwa ana kwa ana lakini hatukufikia mwafaka, baadaye ikatulazimu tufanye kikao tena kwa mtandao. Hata hivyo, wajumbe sita kati ya wanane hawakuridhia uteuzi wa kamati kwa kuwa kuna vitu havikuwa sawa,” alisema na kuongeza;
“Hata hivyo, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Kanda (Belchomas Ponera) alipitisha majina ya uteuzi kwa nguvu na nyaraka alisaini yeye badala ya katibu wa kanda,” anasema Swalehe.
Kwa mujibu wa Swalehe, Kanda ya Kusini kuna kamati tisa ambazo ni pamoja na ya fedha na rasilimali, mafunzo, uenezi, sheria na haki za binadamu, Chadema Msingi, wagombea, sera, ilani na utafiti, Tehama na Chadema famili.
Anafafanua kuwa wakati kikao kinaendelea cha uteuzi taarifa zilivuja, kabla ya walioteuliwa hawajathibitishwa, wengi walijua nafasi zao, jambo ambalo walilipazia sauti kwa kusema ni hatari katika mchakato huo.
“Tulipogundua taarifa zinavuja na kikao kilipositishwa, tulipotoka kikao mmoja wa wajumbe ambaye jina lake lilipendekezwa kwa nguvu ya Ponera, alimshambulia kwa ngumi mmoja wa viongozi wa Chadema Mkoa wa Ruvuma,”
Swalehe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Mtwara, anadai kuwa mjumbe huyo mteule alimpiga kigogo wa Chadema wa Ruvuma akimtuhumu kuwa ndio chanzo cha yeye jina lake kupingwa na wajumbe wengine wa kamati ya utendaji.
Baada ya hapo wajumbe sita kati ya wanane walikubaliana mchakato uanze upya kwa kuwa haukukidhi vigezo kwa mujibu wa taratibu na kanuni za chama hicho kwa madai majina ya wateule yalipitishwa kibabe.
“Tunachoangalia baadhi ya majina baada ya kuyapitia na kupanga kamati zao, ilipaswa kuyapitia tena kisha kuthibitisha, lakini hivi vitu vyote havikufanyika. Ponera aliamua kiubabe na kuweka na kuongeza watu anaowataka yeye,” anasema.
Alichojibu Ponera
Akizungumza na Mwananchi Ponera alisema, “Taratibu zote zilifuatwa, labda kama wao wana mambo yao binafsi, maana kwenye siasa mambo mengi. Tumefanya uteuzi huo kwa maslahi mapana na chama si mtu mmoja, kama wanavyodhani na walioteuliwa ndio wanaofanya kazi za chama katika ngazi mbalimbali za chini,” anaeleza Ponera.
Anasema kwa vile wamelifikisha jambo hilo kwenye ofisi ya katibu mkuu, wanasubiria kuona namna ofisi itakavyotoa uamuzi kwa kadri itakavyoonekana inafaa, huku akisisitiza mchakato huo umefuata utaratibu wote.
Watinga Ofisi ya Katibu Mkuu
Kutokana na sintofahamu hiyo, alisema Juni Mosi, mwaka huu, waliandika barua kwenda ofisi ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kupinga mchakato huo.
Hata hivyo, kwa nyakati tofauti Mwananchi lilimtafuta Mnyika kujua kama barua hiyo ya malalamiko ilishafika mezani kwake, lakini simu yake iliita bila kupokelewa.
Siyo huyu pekee, hata alipotafutwa msaidizi wake, Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa pia simu zake ziliita bila kupokelewa.
Mwananchi halikuishia hapo, lilimtafuta Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, Brenda Rupia, pia simu yake haikupatikani si kwa kawaida au kwa njia ya mtandao.
Pamoja na jitihada hizo, taarifa zilizopo zinadai kuwa barua hiyo ilishafika katika ofisi ya katibu mkuu na wahusika walishajulishwa.
Kwa mujibu wa Swalehe, barua hiyo walioandika kwenda kwa Mnyika, inahusu kupinga uteuzi wa kamati za kudumu za Kanda ya Kusini na waliziainisha sababu za kuupinga uteuzi huo uliofanywa na Ponera.
Mjumbe mwingine wa kanda hiyo, Mustapha Ngonyani anaungana na Swalehe alidai kwamba mchakato wa uteuzi ulikuwa na dosari hali iliyosababisha baadhi ya wajumbe kususa.
“Ule mchakato una dosari na inasemekana yale majina yaliletwa na mtu mmoja tu, sasa si utaratibu wa Chadema kuna vitu vilikiukwa katika suala lile, tulishauri uteuzi usitishwe kwanza ili kupunguza maneno, si busara kutumia nguvu, ndio maana tunaiomba ofisi ya katibu mkuu iamuru mchakato urudiwe ili haki itendeke,” anasema Ngonyani.
Iliwahi kutokea Kanda ya Nyasa
Januari Mosi, 2026, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi alifanya uteuzi wa makatibu na wenyeviti wa kamati za kudumu za kanda hiyo, jambo linalopingwa na wajumbe wa kamati ya utendaji wa kanda hiyo wakidai kwamba utaratibu haujafuatwa.
Pia, wajumbe hao walidai kuwa hata mchakato wa kamati utendaji kupokea mapendekezo ya sekretarieti na kuleta majina ya wajumbe na makatibu wa kamati, haukufutwa.
Kutokana na hilo, wajumbe hao waliwasilisha malalamiko yao katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama hicho ili kufanyiwa kazi na kuondoa sintofahamu iliyoibua mvutano wa pande hizo mbili.