Timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’, jana imepoteza mchezo wa Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U-17) baada ya kukubali kipigo cha mikwaju ya penalti 4-2 kutoka kwa Senegal.
Hata hivyo, Licha ya kupoteza pambano hilo bado Serengeti Boys imeonyesha kiwango bora katika fainali hizo zilizofanyika Morocco. Haikuwa bahati kuingia katika fainali hiyo kutokana na uwezo waliouonyesha vijana hao kwa kuzitupa nje timu bora katika hatua za mtoano.
Serengeti Boys ilifanikiwa kupenya katika hatua za mtoano baada ya kuvuna pointi sita katika kundi C ambalo ilipangwa na timu za Msumbiji, Angola na Mali.
Katika hatua za mtoano vijana hao waliitupa nje Algeria katika hatua ya robo fainali kwa mikwaju ya penalti 4-3, wakifanya hivyo tena katika hatua ya nusu fainali walipoiondosha Misri kwa mikwaju ya penalti 4-3.
Haikuwa kazi rahisi kwa Serengeti Boys kuwaondoa vigogo hao wa soka la Afrika, bali yalikuwa ni maandalizi bora ya muda mrefu yaliyofanywa ili kuhakikisha vijana hao wanafanya vizuri. Haya hapa mambo manne yanayoweza kuwalinda na kuwatengeneza Serengeti Boys wengine;
1. Kuboresha miundombinu bora ya kukuzia vipaji
Uwekezaji katika akademi za kisasa, viwanja vya mazoezi na vituo vya maendeleo ya vijana vitakavyowawezesha wachezaji kupata mazingira bora ya kujifunza na kukuza vipaji vyao.
Senegal imewekeza katika vituo vya maendeleo ya vijana na ndiyo sababu imeendelea kuzalisha wachezaji wanaocheza katika ligi mbalimbali za Ulaya.
Faida yake ni kwamba timu ya taifa itakuwa na wachezaji walioandaliwa katika mazingira yanayofanana na yale ya soka la kimataifa.
Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’. Picha na Maktaba
2. Kujenga ushirikiano na akademi za Kimataifa
Lengo ni kutoa fursa kwa wachezaji waende kupata marisho bora katika akademi za Ulaya. Ushirikiano na akademi za kimataifa utasaidia kuleta maarifa mapya ya ufundishaji, sayansi ya michezo, afya na usimamizi wa maendeleo ya wachezaji.
Kupitia ushirikiano huo, vijana wa Tanzania wanaweza kupata nafasi za mafunzo, majaribio na hata ufadhili wa kucheza katika nchi zenye mifumo bora ya soka.
Mfano ni akademi ya Right to Dream ya Ghana, kupitia ushirikiano wake na klabu mbalimbali duniani, imezalisha wachezaji wanaocheza Ulaya. Pia Ivory Coast inanufaika kwa miaka mingi kupitia ushirikiano wa akademi mbalimbali na klabu za Ulaya zinazosaidia kukuza vipaji vya wachezaji wake.
Kiungo wa Serengeti Boys, Issa Chole (kushoto) akiwa amebeba tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano, kulia ni nahodha wa timu hiyo akiwa na tuzo ya Timu yenye Nidhamu katika Fainali za AFCON U17 2026.
3. Kuimarisha ligi za vijana
Kufanya hivi kutasaidia kuendeleza vipaji na kuibua vipya lakini pia kuwapa vijana fursa ya kutoka nje ya nchi kwenda katika ligi zenye ushindani. Vipaji haviwezi kukua kwa mazoezi pekee, vinahitaji ushindani wa mara kwa mara. Ligi za vijana zinawapa wachezaji nafasi ya kutumia kile wanachojifunza mazoezini katika mazingira halisi ya mchezo.
Ligi imara ya vijana pia huwapa makocha nafasi ya kufuatilia maendeleo ya wachezaji kwa muda mrefu badala ya kutegemea mashindano ya muda mfupi.
Aidha, ligi hizi huwa sehemu muhimu kwa skauti na Klabu kutambua vipaji vipya. Kadiri ushindani unavyoongezeka, ndivyo kiwango cha wachezaji kinavyoongezeka.
Mfano Afrika Kusini, Klabu nyingi kubwa zina ligi na mashindano ya vijana yanayoendeshwa kwa utaratibu mzuri unaochangia kuibua vipaji vinavyoingia moja kwa moja kwenye timu za wakubwa.
Vilevile Misri ina mashindano ya vijana yanayosaidia Klabu kupata wachezaji wa kuendeleza katika timu za wakubwa.
4. Kuandaa makocha bora
Makocha ndiyo walimu wa soka. Hata kama nchi ina vipaji vingi, bila makocha wenye elimu na ujuzi wa kisasa vipaji hivyo vinaweza kushindwa kufikia uwezo wake kamili.
Makocha wanahitaji mafunzo ya mara kwa mara kuhusu mbinu za ufundishaji, saikolojia ya michezo, maendeleo ya vijana, sayansi ya mazoezi na matumizi ya teknolojia katika soka.
Makocha bora huzalisha wachezaji bora. Nchi nyingi zilizofanikiwa katika soka la vijana zimeanza kwa kuwekeza kwanza katika elimu ya ukocha.
Senegal imeendelea kuandaa makocha wenye leseni za viwango vya juu ili kuhakikisha vipaji vinavyogunduliwa na kuendelezwa kwa njia sahihi
Kwa Tanzania, kuandaa makocha wengi wenye leseni na maarifa ya kisasa kutasaidia kujenga kizazi cha wachezaji wenye uwezo wa kushindana katika viwango vya juu na hatimaye kuimarisha timu ya Taifa.