Dar es Salaam. Takribani miezi 11 baada ya kuondolewa kwenye uwaziri na kushindwa kurejea katika siasa za uchaguzi, Ummy Mwalimu amerejeshwa serikalini kupitia mlango mwingine muhimu, baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mshauri wake wa masuala ya afya ya uzazi, mama na mtoto.

Uteuzi huo unaotegemea zaidi uzoefu wake wa muda mrefu katika sekta ya afya kuliko nafasi ya kisiasa, unatafsiriwa na wachambuzi kuwa una ujumbe wa pande mbili; kuendelea kuitumia hazina ya maarifa aliyojijengea akiwa Waziri wa Afya, huku ukiwa pia ishara ya kuziba mpasuko wa kisiasa uliojitokeza baada ya kuachwa katika mchakato wa uteuzi wa wagombea wa ubunge wa CCM mwaka jana.

Kwa mtazamo huo, kurejea kwa Ummy ndani ya mfumo wa Serikali kunafufua mjadala kuhusu nafasi ya utaalamu, sambamba na namna mamlaka ya uteuzi yanavyoweza kuwahifadhi katika uongozi watu wanaoonekana bado wana mchango muhimu hata wanapokosa nafasi kupitia mchakato wa kisiasa.

Mbunge huyo wa zamani wa Tanga Mjini, aliondolewa miongoni mwa mawaziri Agosti 14, 2024 wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya mabadiliko ya viongozi na nafasi yake ikachukuliwa na hayati Jenista Mhagama.

Baada ya kuondolewa serikalini, Ummy alisalia na ubunge wa Tanga Mjini hadi Agosti 2025, muda ambao Bunge lilivunjwa kupisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.

Hata hivyo, safari yake ya kisiasa ilikumbana na changamoto nyingine. Licha ya kuongoza kura za maoni za CCM kwa kupata kura 5,750 za wajumbe akiwania tena ubunge, jina lake halikupitishwa na vikao vya maamuzi vya chama hicho vinavyoongozwa na Rais Samia.

Badala yake, CCM ilimteua Kassim Mbaraka kuwa mgombea wake wa ubunge katika jimbo hilo, hatua iliyomwacha Ummy nje ya nafasi za uongozi wa kisiasa na Serikali, kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010 alipopata ubunge wa viti maalumu.

Baada ya kukaa nje ya uongozi kwa takribani miezi 11, Ummy amerejea ndani ya mfumo wa Serikali Juni 2, 2026, alipoteuliwa na Rais Samia kuwa mshauri wake.

Wachambuzi wa siasa na utawala wanaona uteuzi huo kuwa na uzito unaozidi nafasi aliyopewa.

Uzoefu umembeba

Akizungumzia uteuzi huo, mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala, Dk Hamis Msuya amesema unaonyesha kuwa uzoefu na utaalamu wa mtu vinaweza kuwa na thamani kubwa kuliko nafasi ya kisiasa anayoshikilia kwa wakati husika.

Amesema kwa miaka mingi Ummy amejijengea taswira ya kiongozi aliyebobea katika sekta ya afya, hususan kwenye masuala ya afya ya uzazi, afya ya mama na mtoto pamoja na usimamizi wa mifumo ya utoaji huduma za afya.

Kwa mujibu wa Dk Msuya, mara nyingi viongozi wanapoondoka katika nafasi za kisiasa huonekana kana kwamba mchango wao umefikia mwisho. Hata hivyo, uteuzi wa Ummy unaonyesha kuwa Serikali inaweza kuendelea kunufaika na maarifa na uzoefu wa viongozi hao hata wanapokuwa nje ya nafasi zinazotokana na uchaguzi.

“Nadhani ujumbe mkubwa hapa ni kwamba Serikali imeamua kutenganisha siasa na utaalamu. Ummy amekuwa sehemu ya maboresho mengi yaliyofanyika katika sekta ya afya kwa kipindi cha miaka kadhaa.

Dk Msuya amesema nafasi ya mshauri wa Rais inaweza kumpa Ummy fursa ya kujikita zaidi katika masuala ya kisera na kimkakati kuliko ilivyokuwa wakati wa uwaziri, ambako majukumu ya kila siku ya kiutendaji yalikuwa makubwa zaidi.

Ujumbe wa kisiasa

Hata hivyo, kwa upande mwingine, mchambuzi wa siasa, Said Majjid, amesema uteuzi huo unaweza kutazamwa pia kama ishara ya siasa za maridhiano na usimamizi wa nguvu za kisiasa ndani ya chama tawala.

Amesema katika vyama vikubwa vya siasa ambavyo vina makundi, masilahi na matarajio tofauti ya viongozi, mara nyingi uongozi wa juu hulazimika kutafuta njia za kuhakikisha viongozi wenye ushawishi hawaachwi pembeni kwa muda mrefu kiasi cha kujenga hisia za kutengwa.

“Kumrejesha Ummy katika mfumo wa uongozi kunaweza kuwa njia ya kudumisha mshikamano na kuzuia kuibuka kwa malalamiko yanayoweza kuathiri umoja wa chama,” amesema.

Majjid amesema pia kuwa kadiri uchaguzi mkuu wa mwaka 2030 unavyokaribia, viongozi wakuu wa kisiasa huwa na mwelekeo wa kujenga mazingira ya utulivu ndani ya vyama vyao.

Katika mazingira hayo, amesema uteuzi wa viongozi waliokuwa nje ya mfumo unaweza kutafsiriwa kama mkakati wa kupunguza idadi ya watu wanaoweza kuwa kitovu cha makundi mbadala ya kisiasa au vyanzo vya migawanyiko ya ndani.

Naye mchambuzi wa siasa, Profesa Anania Mkwizu, amesema si jambo la kawaida kwa mwanasiasa aliyekosa nafasi ya ubunge na kubaki nje ya mfumo wa uchaguzi, kurejeshwa haraka katika nafasi za uongozi.

Kwa mtazamo wake, uteuzi wa Ummy unaonyesha kuwa kuaminiwa na kuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu ya umma, kunaweza kuwa msingi wa kuendelea kupata nafasi za uongozi, hata baada ya kushindwa katika mchakato wa kisiasa.

“Kisiasa, uteuzi huu unaonyesha kuwa Rais Samia bado anaona kuna kitu kwa Ummy. Wapo waliotafsiri kuondolewa kwake kwenye mchakato wa uchaguzi kama mwisho wa safari yake ya kisiasa, lakini uteuzi huu unaonyesha picha tofauti,” amesema.

Profesa Mkwizu amesema uteuzi huo ni ishara kuwa ndani ya mfumo wa uongozi bado kuna nafasi ya kutumia watu wenye uzoefu na uwezo bila kujali matokeo ya mchakato mmoja wa kisiasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *