Waislamu wa Canada wameitaka serikali kupambana na chuki dhidi ya Uislamu nchini humo kupitia mageuzi ya kina na hatua madhubuti.

Baraza la Kitaifa la Waislamu wa Canada limesema katika taarifa yake siku ya Ijumaa kwamba chuki dhidi ya Uislamu nchini humo imekuwa tatizo lililokita mizizi na la kimfumo, na kwamba Canada bado ina kiwango cha juu zaidi cha mashambulizi ya kikatili dhidi ya Waislamu miongoni mwa nchi za G7.

Taarifa hiyo imesisitiza haja ya dharura ya serikali kuingilia kati ili kupambana na hujuma dhidi ya Waislamu zinazoongezeka nchini, ikiashiria mapungufu yanayoshuhudiwa katika sera za serikali kuhusu suala hilo.

Baraza la Kitaifa la Waislamu wa Canada limesema kwamba limeandaa mwongozo unaoelezea mapungufu katika sera za Ottawa kuhusu ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu.

Taarifa hiyo pia imeitaka serikali ya Canada kufanya mageuzi kamili ya kitaasisi, kuanzisha mifumo madhubuti ya uwajibikaji na kuchukua hatua madhubuti za kuwalinda Waislamu nchini Canada.

Imeeleza kuwa shambulio lililolenga familia ya Kiislamu katika mji wa London, Ontario mwaka wa 2021, ambalo lilisababisha vifo vya wanafamilia wanne, ni kielelezo cha mojawapo ya mifano maarufu zaidi ya kuongezeka uhalifu wa chuki dhidi ya Waislamu nchini humo.

Mnamo Juni 6, 2021, mshambuliaji aligonga kwa gari familia ya Waislamu ya watu watano iliyokuwa ikitembea kando ya barabara, na kuwaua wanawake wawili, mwanamume na msichana, huku mwanafamilia mmoja, mvulana wa miaka tisa, akinusurika na kupatwa majeraha mabaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *